Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
“Nimepoteza ardhi zaidi ya nusu heka, sina makazi ya kudumu,na hivi sasa nipo na familia yangu ya watu watano, tunajihifadhi katika chumba kimoja kilichopo karibu na eneo la nyumba yangu ilipomoka”
Ni kauli ya Stephen Joel mkazi wa Kijiji Cha Malampaka kata ya Malampaka wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu ambaye amekosa makazi baada ya mvua kubwa ya upepo, iliyoambatana na mawe kunyesha na kusababisha nyumba za wananchi kubomoka pamoja na mapaa ya nyumba zao kuezuliwa.
Februari 17,mwaka huu, jumla ya wakazi 51 wa kijiji hicho walikosa mahala pa kujifadhi baada ya mvua kubwa kunyesha iliyoambatana na upepo na kuezua mapaa ya nyumba na shule.
Stephen anasema kuwa ilikuwa Februari 17, mwaka huu majira ya saa 9:00 mchana mvua kubwa ilinyesha kwa dakika 30 na kusababisha nyumba kuanguka huku zingine mapaa yakiezuliwa.
“Tangua asubuhi hali ya hewa haikuwa kama tulivyozoea, siku hiyo hakukuwa na juu na kadri muda ulivyokwenda kulikuwa giza na ilipofika saa 9 mchana mvua ilianza kunyesha bila kuacha kwa dakika 30 na kusababisha maji kujaa kila kona huku kukiwa na upepo mkali uliosababisha nyumba kuanguka.
“Kabla ya kuanza kunyesha kwa mvua, tulisikia taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) nikiwa kwenye kilabu cha pombe jambo ambalo nililifurahia kwa ajili ya kuandaa mashamba kwani mimi ni mkulima wa pamba, mpunga na vitunguu.
“Lakini sikutarajia kama mvua ingekuwa kubwa kama ambavyo TMA ilitabiri awali kuwa baadhi ya mikoa ingepata mvua juu ya wastani na mingine chini ya wastani hivyo imetusababisha hasara kwani imekuwa juu wastani zaidi hata hivyo ipo haja ya kujifunza na kuchukua hatua mapema kwa taarifa zinazotolewa na TMA kwani wakazi wanaoishi mabondeni ndio wameathirika zaidi,” anasema.
Pamoja na kuwepo kwa maafa lakini pia kuna faida kwao kwa kuwa muda mrefu walikosa mvua hivyo itasaidia katika kilimo cha mpunga kwani kimekuwa tegemeo kwako.
MABADILIKO TABIA NCHI
Mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa changamoto katika zama,kupungua kwa misitu,mabadiliko ya utaratibu wa mvua na kuongezeka kwa kiwango cha maji ya bahari kunaweza kuongeza shinikizo la kiuchumi,kisiasa na kijamii na kuathiri maendeleo ya jamii.
Kutokana na mafuriko yanayoweza kutokea yanaweza kuleta athari kubwa ikiwa ni pamoja na jamii iliyoishi
maeneo hayo kupoteza mali zao ikiwemo mifugo,vyakula pamoja na mazao hivyo ni vyema serikali, wananchi na vitengo vya majanga vikachukua tahadhari mapema.
Jaccob Daud mkazi wa Shinyanga ambaye hivi karibuni mvua ilinyesha na kusababisha hasara anasema kuwa, mazao yaliyokuwa mashambani ukiwemo mpunga, mahindi, alizeti vilisombwa na maji na baadhi kufukiwa na udongo hatua iliyowaathiri kiuchumi.
“Hatuna mazao, hatuna vyakula maana mahindi, mpunga na hata mbazi tulizozitegemea zilisombwa na maji na sasa hata ardhi ambayo tulikuwa tunaitegemea kwa makazi nayo imethirika kutokana na mafuriko hayo hivyo hatuwezi hata kuiendeleza,” anasema.
Anasema kuwa, alilazimika kukimbilia kijiji cha jirani kwa ndugu zake na kuomba hifadhi baada ya nyumba yake kukumbwa na mafuriko.
“Sina nilichookoa vitu vyote vilisombwa na maji, tulitoka nam nguo tu ambazo tulikuwa tumevaa.
Hakika sitaisahau siku hiyo maana ilikuwa ni usiku na sikuwa na pa kwenda,” amesema.
MIFUMO YA HALI YA HEWA
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) ilitoa muhtasari wa mifumo ya hali ya hewa pamoja na mwenendo wa hali ya hewa kwa Februari, 2023 na kutoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa mwezi Machi, 2023 ambapo katika kipindi cha Machi 2023, vipindi vya mvua vilitarajiwa kuendelea katika maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka.
Katika uboreshani wa miundombinu na kuendana teknolojia na matakwa ya kimataifa TMA iliondoa vifaa vyote vinavyotumia zebaki kwa kununua vifaa 15 vya kidigitali vya kupima mgandamizo wa hewa na vifaa 25 vya kidigitali vya kupima joto hewa.
Kaimu Mkurugenzi wa TMA,Dkt.Ladislus Chang’a anasema kuwa mbali ya kufanyika kwa maboresho hayo ambayo yametokana na manunuzi ya vifaa vya kisasa vya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na manunuzi ya vifaa vya kisasa vya hali ya hewa vitakavyofungwa katika njia ya kuruka na kutua ndege katika viwanja vya ndege vya Abedi Karume-Zanzibar,JNIA-Dar es Salaam,KIA-Kilimanjaro na Songwe.
KUONGEZEKA KWA VIWANGO VYA USAHIHI
Anasema kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kwa ujumla vimeongezeka na kufikia asilimia 88.5, ambapo katika msimu wa mvua za Vuli 2022, viwango vya usahihi vilikuwa asilimia 94.1.
“Viwango hivi ni juu ya kiwango cha usahihi wa utabiri kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) cha asilimia 70. Ongezeko hili la usahihi wa utabiri unazifanya huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini kuwa za uhakika na kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta zote za kiuchumi na kijamii nchini zinazotegemea hali ya hewa.
“Kuongezeka kwa usahihi wa utabiri kumetokana na jitihada za serikali kuwekeza katika kusomesha wataalam wa hali ya hewa, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kuandaa utabiri pamoja na kuongezeka kwa mtandao wa vituo vya kupima hali ya hewa,’ anasema.
Anasema kuwa mamlaka imeendelea kutoa utabiri wa msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa usahihi na ubora hivyo kuchangia kupunguza athari kwa watu na mali zao.
“Mfano Oktoba 2021 TMA ilitoa utabiri wa msimu wa mvua za Vuli kuwa chini ya wastani. Utabiri huo uliziwezesha Mamlaka mbalimbali kufanya maamuzi stahiki na kusaidia kuepusha madhara makubwa ambayo yangeweza kutokea,” anasema.
TAARIFA ZA HALI YA HEWA NA UTUNZAJI MAZINGIRA
Katika kufikia mafanikio TMA imeendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) katika kutekeleza majukumu ya sekta ya hali ya hewa kwa shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwemo kufuatlia mabadiliko ya hali ya hewa yanayopelekea mabadiliko ya tabia nchi.
Vituo vya kupima uchafuzi wa hewa (air pollution monitoring 20 vilinunuliwa na kufungwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuona kwa kiasi gani shughuli za kibinadamu zinavyoharibu mazingira.
UBUNIFFU WA WATUMISHI
Monica Mutoni ni ofisa uhusiano wa TMA,anasema kuwa ubunifu katika TEHAMA umefanikisha kuundwa kwa mifumo mbalimbali iliyorahisisha shughuli za uendeshaji na utoaji wa huduma.
Baadhi ya mifumo hii ni “Meteorological Aviation Information system (MAIS)” ambao imeendelea kuboreshwa na unatumika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa usafiri wa anga; “Marine Meteorological Information System (MMIS) ambao unatumika katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu pamoja na “Digital Meteorological Observatory (DMO)”, mfumo ambao unatumika katika kurekodi taarifa za uangazi, kuzituma Kituo Kikuu cha Utabiri wa hali ya hewa.
“Mifumo hii ya TEHAMA pia imeiwezesha mamlaka kutoa huduma mahsusi kwa sekta mbalimbali zikiwemo za madini, usafiri wa barabara, ujenzi na utalii.
“Mifumo mingine iliyobuniwa na wataalam wa mamlaka ni ile ya mawasiliano ya data kutoka vituoni hadi Kituo Kikuu cha Utabiri na usajili wa vituo vya hali ya hewa na “Regional Specialized Meterorological Center- Dar es Salaam-RSMC Portal” kwa ajili ya Kituo cha Kanda cha kutoa mwongozo wa utabiri kwa Nchi za Ukanda wa Ziwa Victoria,” anasema.
Monica anasema kuwa kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa kukarabati vituo saba vya hali ya hewa vilivyopo katika mikoa ya Singida, Songwe, Mpanda, Shinyanga, Songea, Mahenge na Tabora pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kilichopo Kigoma ulifanyika.
Pia kukidhi Viwango vya Ubora vya Kimataifa katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga na hivyo anga la Tanzania kuendelea kuaminika kuwa salama.
“Katika kipindi cha miaka miwili, Mamlaka ilifanyiwa ukaguzi wa kimataifa na Kampuni ya Certech ya Canada juu ya utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa ubora wa huduma “Quality Management Systems(QMS)” kwa mwaka 2021 na 2022 ambapo ukaguzi wa mwaka 2022 ulifanyika kuanzia tarehe 14 hadi 21 Januari 2023.
“Katika kaguzi hizo ubora wa huduma zinazotolewa na Mamlaka katika sekta ya usafiri na usalama wa anga zilionekana kukidhi mahitaji ya wadau, jambo ambalo liliwezesha mamlaka kuendelea kushikilia cheti cha ubora wa huduma tajwa cha ISO 9001:2015,” anasema.
TMA ilitekeleza vizuri dhamana ilizopewa kikanda na kimataifa na kufanikiwa kuitangaza vizuri TMA na Tanzania kimataifa. Wataalamu kumi na moja (11) wa TMA walioteuliwa kuhudumu katika vikosi kazi mbalimbali vya Kamisheni za WMO walishiriki vyema na kutoa mchango wa kitaalamu katika shughuli za vikosi kazi hivyo.
Kutokana na ushiriki mzuri, TMA iliendelea kuaminiwa ambapo Dkt. Hamza Kabelwa ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati ya WMO ya Uchakataji wa Data na Utabiri wa Hali ya Hewa “Standing Committee on Data Processing for Applied Earth System Modelling and Prediction (SC-ESMP)” huku Dkt. Pascal Waniha, ambaye ni Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Ufundi katika Mamlaka aliteuliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza wa kikosi kazi cha utekelezaji wa programu ya WMO “Task Team on Global Basic Observing Network (TT-GBON)”.
Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilikuwa mwenyeji wa kongamano la 15 la watumiaji kutoka Bara la Afrika wa data na huduma zitolewazo na Shirika la Satelati za hali ya hewa la Umoja wa Ulaya “The 15th EUMETSAT User Forum in Africa (15th EUFA)” ambapo lilifanyika kwa mafanikio na kuitangaza TMA na Tanzania kimataifa katika nyanja mbalimbali kama vile vivutio vya utalii na Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa cha Kigoma.
Dkt. Mafuru Kantamla Kaimu Meneja Kituo Kikuu Cha Utabiri TMA anasema katika msimu wa mvua za masika mwaka huu takribani mikoa 11,inatarajia kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani huku mikoa minne ikitarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Mikoa hiyo 11 inayotarajiwa kupata mvua wastani hadi chini ya wastani ni pamoja na Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga,Simiyu, Mara,Arusha Manyara,Kilimanjaro, Tanga pamoja Kisiwa cha Pemba huku maeneo machache ya Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha Mafia, kaskazini mwa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja vikitarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Anasema kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa katika kipindi cha msimu, mvua za wastani hadi juu ya wastani zitanyesha katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani (katika visiwa vya Mafia), Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na Kisiwa cha unguja.
Anasema ongezeko la mvua katika maeneo hayo linatarajiwa kuanza mwezi Mei, 2023 hususani katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini.
“Mvua za Masika zinatarajiwa kuanza kunyesha Machi katika maeneo Mengi na zinatarajiwa kumalizika katikati ya wiki ya nne ya mwezi Mei 2023 huku muendelezo wa mvua za nje ya msimu ukitarajiwa mwezi J Juni 2023 katika maeneo machache ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini” anasema.
“Katika maeneo ya ukanda wa Ziwaa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma mvua zinatarajia kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi machi 2023 na kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Mei.
huku katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani katika visiwa vya Mafia, Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na kisiwa cha unguja mvua zinatarajia kuanza wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi na kuisha Juni,2023.’’ Ameongeza.
Amesema katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro mvua iznatarajiwa kuanza kunyesha wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi 2023 na kumalizika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei 2023,’’
ATHARI
Akizungumzia athari zinazoweza kutokea Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dkt.Chang’a anasema, mvua chache zenye mtawanyiko usioridhisha kwa maeneo yanatarajiwa kunyesha mvua za wastani hadi chini ya wastani, kunaweza kusababisha upungufu wa unyevu kwenye udongo na upatikanaji wa maji kwa shughuli za kilimo.
“Shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama kawaida isipokuwa kwa baadhi ya maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chache zenye mtawanyiko hafifu yanaweza kukumbwa na upungufu wa unyevu wa udongo na upatikanaji wa maji kwa shughuli za kilimo” anasema.
Ameongeza kuwa, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinazotarajiwa zinaweza kuathiri upatikanaji w maji safi na salama na hivyo inaweza kusababishi mgonjwa ya mlipuko.
USHAURI
Aidha mkurugenzi TMA amezishauri menejimenti za maafa kufuatilia kwa karibu taarifa za tahadhari na kushirikiana kuchukua hatua za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa yanayoweza kujitokez.