Sakata la kufungia mita za kupimia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam limechukua sura mpya baada ya kupata vielelezo vinavyoonyesha kuwa Kamishna wa Wakala wa Vipimo, Magdalena Chuwa aliyesimamishwa kazi kupisha uchunguzi alitengeneza mkoroganyo mkubwa.
Chuwa alizigonganisha taasisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), bila kuwashirikisha, lakini yeye ameliambia JAMHURI kuwa hakuwashirikisha kwa kuwa nao wao walikuwa hawamshirikishi.
Barua za majibizano zenye kuonyesha mjadala uliotia shaka kama hawa watu wangeendelea kufanya kazi pamoja ua kulikuwapo msukumo wa aina yake kutoka kwa waagizaji wa mafuta, zinaonekana wazi katika barua za mawasiliano kati ya viongozi wanaoongoza taasisi hizo nyeti kama TRA, TPA na TBS.
Gazeiti la JAMHURI katika uchunguzi wake wa miaka miwili juu ya kusitishwa kwa matumizi ya mita za mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam na Tanga, umebaini kuwa maslahi binafsi yalitawala zaidi kuliko maslahi ya nchi na uzalendo.
Barua ya Chuwa kwa TPA
Sarakasi za mita hizi kusitishwa zilianza kwa barua ya Chuwa yenye Kumb. Na. BA/84/221/01/26 ya Februari 2, 2011 iliyositisha matumizi ya mita za kupima mafuta yanayoingia nchini.
Barua hiyo ilisema: Flow meters zilizofungwa mwaka 2005 na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), katika Bandari ya Dar es Salaam zimethibika kuleta usumbufu kwa baadhi ya wadau na malalamiko hayo yanasababisha mivutano isiyo na tija.
Kwa bahati mbaya sana, mita hizo zimeonyesha hazina ubora wa kutenda kazi tangu zilipofungwa kwani imethibitika baada ya mwaka mmoja tu.
Juhudi za kuzitengeneza Oktoba 2006 na Januari mwaka 2007 zilishindikana. Pia ukarabati uliofanyika Mei, 2007 na baadaye ikabainika Julai, 2008 kuwa hazifai.
Kama haitoshi, ofisi yangu iliendelea kupokea malalamiko kutoka kwa wadau kuhusiana na mapunjo ya mita hizo katika kuingiza mafuta. Kutokana na hali hiyo na kwa sababu za kiufundi, tulilazimika kusitisha matumizi ya mita hizo.
Utakumbuka Februari, 2009 tuliishauri TPA kuhakikisha kwamba wahandisi na mafundi wote, lazima wathibitishwe na Kamishna wa Wakala wa Vipimo kwa mujibu wa sheria na taratibu ili kupunguza baadhi ya makosa.
Aprili 2009, Bandari (TPA) walijaribu kuleta ‘neno siri’ katika wakala wa vipimo kwa malengo ya kudhibiti hujuma katika kuingiza mafuta, lakini haikusaidia kwa kuwa mita zenyewe hazikuwa na ubora na uwezo wa kufanya kazi kusudiwa na TPA walipoamua kufanya hivyo, wakala haukujulishwa.
Ukweli huo pekee ulitosha kuthibitisha mita hizo hazikuwa na ubora, hivyo kuathiri ubora wa mafuta na wadau kupunjwa kwa sababu za muda wa kuingia mafuta na safari ndefu huko walikotoka hivyo kuonekana hazifai.
Uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na WMA hivi karibuni katika uingizaji wa mafuta na kuangalia ubora wake umebaini na kuthibitisha kuwa kuna dosari ya ubora wa mafuta kutoka melini hadi kuingia kwenye matangi.
Flow meters zilizofungwa KOJ zimefungwa kwa kiwango cha joto sentigredi 15 na si 20 ambayo ingefuta malalamiko ya wadau kama ambavyo taratibu wa utozaji kodi za TRA zinavyosema na wapokeaji.
Kadhalika imebainika kwamba mita hizo ni maalumu kwa ajili ya kupakia mzigo wa mafuta, si kupima kwa ajili ya kushusha mzigo. Mkanganyiko huo umesababisha usumbufu kwenye ushushaji kutokana na kasi ndogo ya kutoa mafuta hivyo kuongeza gharama za fedha na muda vinavyochangiwa na foleni ndefu.
Kutokana na yaliyoainishwa hapo juu na kifungu cha 15 (b) na 18 (2) vikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 23 (a) pamoja na kanuni zake za Sheria Na. 340, natamka kwamba, mita zifuatazo 16 hazifahi kwa matumizi ya kibiashara na hivyo, hazipaswi kutumika kwa ajili ya biashara kuanzia leo.
Kuendelea kutumia mita hizi, itakuwa kinyume cha sheria iliyorejewa hapo juu na hivyo kutenda uhalifu.
Barua hiyo nakala yake ilitumwa kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Kamishna Mkuu wa TRA, Mkurugenzi mkuu wa Ewura, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni za Biashara ya Mafuta (TAOMAC), Dar es Salaam.
Bandari wajibu mapigo
Baada ya agizo hilo la Mama Chuwa, Bandari walieleza mshituko wao na kutilia shaka iwapo uamuzi huo ulifikiwa kwa masilahi ya taifa au binafsi na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Ephraim Mgawe aliandika barua kali kwa Chuwa yenye Kumb. Na. DG/.0/1/01 ya Machi 8, 2011 akisema:
Tafadhali rejea barua yako yenye Kumb. Na. BA/84/01/265 ya Februari 2, 2011 juu ya mada tajwa. Nimepitia barua yako kwa mshtuko mkubwa na kutoamini ujumbe wake. Nimeshindwa kuelewa, msimamo dhidi ya ukweli na matukio yanayohusiana na suala hili kwamba;
a) Juni 15, 2010 ulitoa cheti cha ubora kwa miezi 12 juu ya suala unalolizungumzia ambacho kinaishia Juni 14, 2011, lakini kwa mshangao sasa unasitisha mita zilezile hata kabla ya kipindi ulichotoa (cha ubora wa mita) hakijaisha.
b) Sijawahi kupata ripoti yoyote ya ukaguzi kutoka kwako, mweledi, juu ya ubovu unaosemwa kwa mita hizi. Hii inapingana na matakwa yako ambapo unatakiwa kabla ya kuzifuka ulipaswa kufanya uchunguzi, kuandaa ripoti na kushauri marekebisho ama vinginevyo.
c) Wakala wako ni sehemu ya timu ambayo imekuwa ikishiriki katika kuratibu utendaji wa mita za mafuta pale KOJ tangu mwaka 2005. Uamuzi wako binafsi wa kusitisha mita bila kushauriana na wadau wengine wa timu (TRA, TBS na TPA), unaacha maswali mengi.
Pamoja niliyotangulia kusema, sasa nataka kufafanua mambo ya msingi, uliyoyasema katika barua yako kama ifuatavyo:-
i) Uhusika wa wakala wa vipimo (WMA)
Wakala wako amekuwa akishiriki katika mradi huu kwa njia mbalimbali:
a) Mara tu zilipofungwa mita mwaka 2005, wakala wako ulikaribishwa na ulishiriki katika kuthibitisha mita na ulitoa cheti cha ubora (kielelezo A).
b) Kila mwaka umekuwa ukithibitisha mita hizo na kutoa cheti cha ubora kuanzia mwaka 2006 mpaka 2010.
c) Wakala wako ulishiriki mafunzo ya wiki mbili juu ya marekebisho na kuthibitisha mita za KOJ Novemba, 2009 yaliyoendeshwa na mtengenezaji wa mita kwa gharama za TPA jijini Dar es salaam (orodha ya mahudhurio, kiambatanisho C).
d) Februari, 2009 wakala wako ulitoa leseni kwa makandarasi na mafundi mchundo ambao wanawajibika kukarabati mita.
e) Wakala wako pekee, ndiyo wenye neno la siri linalokuwezesha kuingia katika mfumo wa flow meters na kubadili vipimo wakati wa kupima au kuthibitisha mita za mafuta. Kwa muda wote, umekuwa ukiweka vipimo na neno la siri bado ni hai.
f) Tangu 2009, mita zote zinafanya kazi kwa uwezo wake wote. Hakuna mita iliyopata hitilafu kwa wakati huo. Kutokana na kuongezeka kwa meli za mafuta, mita zimekuwa zikifanya kazi kwa saa 24 kwa siku.
Hivyo inashangaza kuona kwamba hata hutambui kwamba mita zimekuwa zikifanya kazi tangu wakati huo.
Ni kinyume cha maadili na inasumbua kuona kwamba umekuwa ukipokea ‘malalamiko kutoka kwa wadau juu ya mita kutofanya kazi vizuri’, lakini hujawahi kamwe kuijulisha Bandari malalamiko hayo.
Kufungia kwako mita, kumeegemezwa katika sababu mbili ambazo ni usomaji tofauti wa mita dhidi ya vipimo vingine na kwamba mita za KOJ ni kwa ajili ya kupakia tu.
i) Kusoma tofauti
Mita za mafuta za KOJ zinafanya kazi kati ya nyuzi joto 0-65. Hivyo, mita zinasoma joto halisi kwa kutumia ving’amuzi vya joto ambavyo vimeunganishwa na mabomba.
Hesabu za ujazo zinafanywa na chini ya nyuzijoto 20. Nimeshtushwa kuona barua yako inasema mita zimefungwa kwa nyuzijoto 15 ambayo unashutumu kuwa inatumika kupigia hesabu ujazo. Hii uliipata wapi?
Nimethibitisha kwamba mita zimefungwa chini ya nyuzijoto 20 kutoka kwa mshauri mtaalamu (COWI) na mtengenezaji wa mita, FMC Energy system (Kielelezo D)
ii) Mita za kujaza na kupakua
Maelezo yako kwamba mita za KOJ ni za kupakia na si za kupakua mafuta, ni uzushi. Mita hazifahamu kama zinajaza au kushusha. Lengo kwa mambo yote mawili ni kupima ujazo. Zimetengenezwa kwa ujumla kupima ujazo wa vimiminika kwa ajili ya kazi zote kama kupakia au kushusha kwenye malori, kupakia au kushusha kwenye mabehewa ya treni, kupakia au kushusha melini, mabomba ya mafuta, matangi, nakadhalika.
Matumizi mbalimbali yana mifumo tofauti na tabia tofauti, bidhaa na mazingira ya kazi.
Mita za KOJ zilitengenezwa kwa kuzingatia mazingira yote ya upakuaji, ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mshauri wa mradi, COWI na mtengenezaji FMC Energy System yameambatanishwa kama kielelezo D.
Upuuzi kwamba msongamano katika bandari, hauchangiwi na mita za mafuta bali mambo mengine kama ucheleweshaji wa vielelezo, meli kubeba zaidi ya bidhaa moja, uwezo wa usumaji mdogo, udogo wa mabomba yanayopokea mafuta, umbali wa matangi yanayopokea mafuta, kuongezeka kwa meli za mafuta dhidi ya uwezo nakadhalika.
Napenda kukukumbusha kwamba mita za KOJ zilifungwa kwa nia ya kupima kiwango kinachoelezwa na mawakala. Ni serikali iliyohitaji kwamba mita hizo zifungwe kwa usomaji sahihi wa kiwango cha kodi sahihi.
Wakala wa vipimo, akiwa wakala wa Serikali angelitambua hili, angefanya mashauriano kwa nia ya kufanya kazi kwa pamoja kupata ufumbuzi ikiwa lilikuwepo tatizo la kutanzuliwa. Kuishauri TPA/TRA kurejea katika utaratibu wa kusoma kilichotolewa na mawakala wa meli inaturudisha nyuma tulikotoka kwa sababu zisizo za msingi.
Kwa mtazamo huo, nakuomba ufute uamuzi wa kuzifungia mita mara moja.
Wako Mwaminifu.
Kwa niaba ya Mamlaka ya Bandari Tanzania
E. N. Mgawe.
Mgawe alitoa nakala kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Magdalena Chuwa, aliyesimamishwa kazi kupisha uchunguzi kutokana na kusitisha matumizi ya mita za kupimia mafuta (flow meters) yanayoingia nchini kwa miaka zaidi ya mitano, amejitetea.
Pamoja na Chuwa, mwingine aliyesimamishwa kazi ni Meneja Vipimo Kitengo cha Mafuta Bandari, Bernadina Mwijarubi, ikiwa ni siku moja baada ya Gazeti la JAMHURI kuchapisha taarifa za upotevu wa fedha Bandari kutokana na kuzuia matumizi ya mita hizo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alizuru Bandari ya Dar es Salaam na akatoa maagizo mita hizo zianze kufanya kazi baada ya kuzimwa mwa miaka mitano.
Habari hii ndiyo iliyomfanya Rais John Magufuli kulipongeza Gazeti la JAMHURI wakati akihutubia Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Jumamosi iliyopita.
Nipende pia kuchukua nafasi hii kuwashukuru sana waandishi wa habari. Vyombo vya habari mmetusaidia sana. Mumeisaidia sana Serikali hii, naomba msichoke. Naomba msichoke. Mnatoa elimu ya kutosha, mnatoa maelekezo ya kutosha, na sisi ndani ya Serikali huwa tunafatilia.
Juzi juzi kuna gazeti moja liliandika. Ni gazeti gani… la JAMHURI, likawa linatoa michoro ya huko, tukawa tunaulizana Waziri Mkuu, hawa wamejuaje sisi tunapanga mipango katikati na wao wameshajua. Tunawapongeza. Vyombo vya namna hiyo ndivyo vinatakiwa kufanya, siyo vyombo ambavyo vinakaa pale kwa ajili ya kuitafu…kuitukana Serikali na Tanzania.
Sisi Watanzania hatuna mahali pengine pa kwenda kukaa. Yapo magazeti mengine kwakweli yanaandika mpaka mtu unashangaa. Unajiuliza huyu ni Mtanzania au sio Mtanzania? Yeye kila kitu ni kuichafua tu Tanzania kana kwamba yeye pakitokea machafuko hapa ana mahali pengine pa kwenda kukaa.
Lakini kwa ujumla vyombo vingi vya habari vimekuwa very supportive kwenye Government hii. Nawapongeza sana keep it up. Na ndiyo maana nimeweza kutoa mfano, nimetoa mfano wa gazeti la JAMHURI lilivyotoa uozo kule kwenye flow meter. Tunataka magazeti mfanye hivyo.
Pakitokea kuna uozo mahali uandike. Sisi tunasoma. Sisi wote ni Watanzania, sisi wote tuna wajibu wa kuipeleka Tanzania mbele. Na tuiweke Tanzania yetu kwanza. Hakuna mtu atakayeisemea uzuri wa Tanzania. Ni vema sisi Watanzania, tuisemee Tanzania mazuri ili hata wa nje watatusemea mazuri.
Waziri Mkuu Majaliwa alipokwenda Bandari, alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru, kuwasimamisha kazi wawili hao kupisha uchunguzi.
Kabla ya kusimamishwa, Chuwa alikuwa amefanya mahojiano maalumu na JAMHURI ambapo alisema walikubaliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzifunga baada ya kampuni zinazoagiza mafuta kulalamika kuwa zinatoa vipimo vinavyotofautiana.
Anasema WMA haikushirikishwa kwenye ununuzi wa mita hizo mwaka 2004, badala yake waliitwa dakika za mwisho kwenda kuona ufungaji wake na baada ya kuaminishwa kuwa zilikuwa nzuri walitoa kibali zianze kutumika.
Alipohojiwa sababu za kuzifunga bila kuwasiliana na mamlaka nyingine na kushindwa kujibu barua ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Chuwa akasema: “Flow meters zilifungwa na TPA kwa kushirikiana na TRA. Kulikuwa na mawasiliano baina yao tu. Sisi hatukushirikishwa kabisa.
“Hatua hii ilianza kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa TPA, Ephraim Mgawe, kama unavyoona barua, ikaendelezwa na [Kaimu Mkurugenzi Madeni] Kipande na pia Awadhi Masawe. Hata kule Tanga, Massawe alifanya hivyo hivyo maana alikuwa Port Manager (Meneja wa Bandari) wa Tanga”.
Massawe alipohojiwa na JAMHURI kuhusu kufungwa kwa mita hizo, alionesha barua aliyoandikiwa na Chuwa ikimwamuru kuzifunga mita hizo, hata baada ya awali kuwa ametoa masharti zifanyiwe marekebisho. Barua aliyoandika kufunga mita hizo ni ya Februari 2, 2011 yenye kumbukumbu Na BA/84/221/01/26.
Chuwa anasema kwa nyakati tofauti waliwashauri wadau wenzao wa Bandari na TRA, lakini hawakupata ushirikiano hasa Madeni Kipande ambaye wakati wote alikuwa akitoa majibu ya dharau. Mvutano uliibuka baada ya Chuwa na wataalamu wake kudai mita hizo hazina ubora unaotakiwa.
“[Kipande] hataki hata kutusikiliza na kuna siku alitaka kumpiga mmoja wa wasaidizi wangu. Na walikwepa mita hizo [akina Kipande] kwa sababu wafanyabiashara au watu wanaoingiza mafuta wanapata hasara,” anasema na kuongeza kuwa baada ya wafanyabiashara kulalamika kwa Kipande, alimpelekea nakala ya malalamiko ndipo akalazimika kufunga hizo mita.
Anasema anahisi hakupata ushirikiano kwa sababu ya jinsia kwani Mgawe na hasa Kipande kwa wakati wote walikuwa wanamdharau yeye na timu yake.
Chuwa anasema sheria inamruhusu kusimamisha mfumo wowote unaoonekana si sahihi na alichukua uamuzi huo mwaka 2011 kwa sababu wao ndiyo wataalamu wa masuala ya vipimo na kwa wakati wote wamekuwa na mvutano kati yao na TPA na TRA.
Majaliwa amesema ikithibitishwa kuwa walihusika katika sakata hilo, hatua za kisheria zitachukuliwa na endapo hawakuhusika watarudishwa kazini ila akaagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow meters urejee mara moja kukadiria kusitumike tena.
Wakati akijitetea mbele ya Waziri Mkuu, Chuwa alisema kuwa alifikia uamuzi wa kuzifunga mita hizo baada ya kupokea malalamiko kwamba zinawapunja wateja. Hata hivyo, hakufafanua ni wateja wepi au wa aina gani, lakini Chuwa alithibitisha mita hizo zilianza kufanyiwa ukarabati Jumatano iliyopita na kupokea mafuta ya petroli.
Flow meter ya dizeli ilifunguliwa na mafundi na kukutwa imejaa kutu sababu ya kutotumika kwa muda mrefu. Waziri Mkuu alimwagiza Chuwa aandike barua ya kujieleza ni kwa nini aliamua kufunga mita hizo zisitumike kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita, na amletee barua hiyo ofisini kwake ifikapo saa 11 jioni.
“Nataka unieleze ni kwa nini ulitoa maelekezo ya kufunga mita hizo, na kwa nini jana uliamua kubadili uamuzi huo? Ni kwa nini umeamua kuchukua maamuzi haya baada ya kupokea ujumbe wa simu ya mkononi (sms) wakati mita zimekaa bila kufanya kazi kwa miaka mitano? Ni kwa nini umeamua kufanyia kazi ujumbe wa sms wakati unajua Serikali inafanya kazi kwa maandishi rasmi?” alihoji Waziri Mkuu na kuongeza:
“Umesema mlikuwa mnatumia utaratibu wa kupima kwa kijiti. Huu hauna uhakika na huwezi kutegemea taarifa ya mtu mwingine au kuingia kwenye meli ya mtu na kuanza kuchukua vipimo hadi ujiridhishe. Nataka kujua ni kwa nini mlikuwa na utaratibu wa ku-bypass mafuta ili yasipite kwenye mita za kupimia mafuta? Ni kwa nini umetoa amri zianze kutengenezwa jana na siyo mwaka 2012 au 2013?”
Mita hizo za Kurasini zilinunuliwa na Serikali kwa gharama za dola za Marekani milioni 1.2 mwaka 2004 na Majaliwa alisema haiwezekani kuacha kuzitumia wakati watu wanachezea mifumo na kuongeza mianya ya kupoteza mapato kwa Serikali. Ameagiza mita hizo zianze kufanya kazi mara moja.
Waziri Mkuu alisema matumizi ya mita hizo yaliafikiwa na Serikali baada ya kubaini upotevu mkubwa wa kodi kwenye mafuta yanayoingizwa nchini na baada ya kuona hakuna tija ya kuendelea na ukadiriaji au kupokea taarifa za waagizaji peke yao.
Majaliwa pia alitembelea na kukagua mita mpya ya kupimia mafuta inayojengwa Kigamboni eneo la Mji Mwema. Mita hiyo imegharimu dola za Marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96 za sasa).
Pia, alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Many-fold) iliyoko Kigamboni na kukagua mabomba ya kusambazia mafuta kwenye matangi ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na kampuni ya Oryx Energies.
Katika ziara hiyo, ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini, hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.
“Natoa mwezi mmoja hili bomba liondolewe kwenye mfumo huu na kama yapo mabomba mengine pia yaondolewe,” anasema huku akitazama kipande cha karatasi alichokuwa nacho mfukoni kinachosadikiwa kuwa alikikata kutoka katika ukurasa wa mbele wa Gazeti la JAMHURI.
“Msajili wa Hazina hili ni eneo lako na wewe unamiliki TIPER kwa asilimia 50, hebu simamia hili. Ninyi TPA leteni mapendekezo yenu serikalini ili tuone tunaweza kudhibiti vipi vitendo kama hivi,” alisema Waziri Mkuu.
Alimtaka Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru, awasiliane na Mwanasheria Mkuu waangalie upya mkataba na umiliki wa matangi ya TIPER uwe chini ya Serikali kwa asilimia 100 mafuta yanayoagizwa na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency) yahifadhiwe huko.
Serikali imeagiza katika kipindi hiki Chuwa na Mwijarubi wasisafiri kwenda popote hadi uchunguzi utakapokamilishwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Polisi wameagizwa kufuatilia suala hilo mara moja.
Katika hatua nyingine, JAMHURI imefanikiwa kumpata mhandisi bingwa wa flow meters hizo hapa nchini, Emmanuel Mataro.
Mataro anatajwa kuwa ndiye aliyeshiriki kuziweka mashine hizo kuanzia mwaka 2004 hadi kazi hiyo ilipokamilika mwaka 2005.
Kwa kutambua uwezo wake, WMA ilimpa cheti maalumu cha kumwidhinisha kuzifanyia matengenezo, lakini baadaye aliachishwa kazi katika kile kinachoelezwa kwamba ni mkakati wa wahujumu uchumi kutaka kuona mita hizo hazifanyi kazi na kwa hiyo mafuta yaingie nchini bila kupimwa.
Alipoulizwa na JAMHURI, Mataro akathibitisha: “Ni kweli natambuliwa kama mhandisi mtaalamu wa hizo mita, ni jambo la faraja kusikia sasa zinatakiwa zifanye kazi.”
Alipoulizwa kama yuko tayari kusaidia, akaongeza: “Mimi kulitumikia Taifa langu ni wajibu wangu, kama nitatakiwa kulitumikia Taifa langu hilo ni suala la wakubwa kuamua.”