Na Tatu Saad, JAMHURI MEDIA

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania limetoa tamko kwa wanaohitaji kuanzisha mashindano yoyote ya mpira wa miguu.

Kupitia ukurasa wake wa Mitandao ya kijamii TFF wametoa taarifa inayosema wao ndio wenye mamlaka ya kutoa kibali kwa mashindano yoyote yafanyikayo hapa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo TFF wamesema kwa yoyote anayehitaji kuandaa mashindano yoyote iwe ni taasisi au mtu binafsi anatakiwa kuomba kibali ili kucheza mashindano hayo.

“Mtu binafsi au taasisi inayotaka kuandaa mashindano inatakiwa kuomba kibali ili kucheza mashindano yake” imesema taarifa hiyo

Hata hivyo taarifa hiyo imethibitisha kuwa TFF imepokea taarifa ya mashindano ya Ramadhan yanayojulikana kama ‘Ramadhani Cup’ ambayo yamepewa kibali cha kuchezwa.

Taarifa inasema mashindano ya Ndondo Cup na mengine ambayo yanatangazwa kufanyika hayajapewa kibali na shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania ‘TFF’.

Aidha TFF imewaomba wadau wa soka na waandazi wa mashindano kama hayo kufuata taratibu zilizowekwa na shirikisho la soka Tanzania kwani wao pekee ndio wenye mamlaka ya kutoa kibali Kwa mashindano yoyote yanayofanyika nchini.

“Ni vyema yeyote anayetaka kuendesha mashindano yake akafuata utaratibu” imesema taarifa hiyo