Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri Mkoani Tabora wameagizwa kusimamia kikamilifu mfumo wa Ugavi wa bidhaa za afya ikiwemo ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya kupunguza changamoto zinazotokana na Usimamizi mbovu.
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 22,2023 na Mkuu wa Wilaya ya Tabora Louis Bura akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batrida Buriani kwenye Mafunzo ya wawezeshaji wa Mfumo ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba iliyofanyika katika ukumbi wa mtemi Isike Mwanakiyungi mkoani hapa.
Alisema kwamba Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya unakuwa asilimia 100 .
“Viongozi wana jukumu kubwa kuvisimamia vituo vya afya ili viweze kukusanya mapato ya kutosha kwa ajili ya ununuzi wa madawa na vifaa tiba ,sambamba na kusimamia mnyororo wa ugavi’’ .
Aidha Mkuu wa Wilaya alisema viongozi wakishatekeleza hayo watu wote watapata huduma za bidhaa za afya katika vituo vyetu vya kutolea huduma bila manung’uniko hasa tunapoelekeza katika utekelezaji wa Bima ya Afya .
Hata hivyo alibainisha kwamba mfumo huo unawezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba zinazokuwa zimekosekana Bohari ya Dawa (MSD) ,huvyo kuimalisha na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa za afya katika vituo vya kutolea huduma nchini na kupunguza hoja za kiukaguzi katika ununuzi wa bidhaa.
Louis Bura alisema anatumaini mara baada ya kumaliza mafunzo hayo watakuwa mabalozi wazuri na wataondoka na uelewa wa pamoja wa utekelezaji wa mwongozo wa mfumo huo ili kuweza kusimamia kikamilifu kwa ajili ya kuleta matokeo sahihi .