Na Jacquiline Mrisho- MAELEZO
Jumla ya wawekezaji wapatao 23 kutoka nchi za Uganda, Kenya, India, Uturuki, China, Sudan, Falme za Kiarabu, Pakistan, Zambia na Tanzania waliotembelea kujionea maendeleo ya ujenzi wa Kongani ya Kisasa ya Viwanda iliyopo katika eneo la Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani wameonesha nia ya kuwekeza katika eneo hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Afriq Engineering and Construction anayehusika na usanifu na ujenzi wa miundombinu wezeshi katika kongani hiyo, Mhandisi Charles Bilinga amesema kuwa mradi huo unakusudia kutumia jumla ya Dola za Marekani milioni 51 sawa na takriban Shilingi bilioni 122.4 katika kipindi cha miaka mitano.
Kongani hiyo inakadiriwa kuwa na jumla ya viwanda 203 vyenye uwekezaji wa Dola za Marekani bilioni 1.326 sawa na Shilingi trilioni 3.182 ambapo kwa sehemu kubwa fedha hiyo inatarajiwa kutoka nje ya nchi na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na viwanda.
“Kati ya wawekezaji 23 walioonesha nia ya kuwekeza, jumla ya wawekezaji watatu wako tayari kuanza ujenzi wa viwanda ambapo mmoja wa wawekezaji hao ni kutoka nchini Uturuki Tanturk Tanzania Power Company Limited ambae anatarajia kujenga kiwanda cha majenereta aina ya Perkins kwa ajili ya kuuza katika soko la Afrika Mashariki na Nchi za Kusini mwa Afrika.” amesema Bilinga.
Ameongeza kuwa, ujenzi huo unatarajiwa kuanza mwezi Juni, 2023 na utagharimu takriban Shilingi bilioni 24 na unatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja 200. Aidha, viwanda vingine vilivyothibitisha kuanza ujenzi ni kampuni kutoka nchini Uturuki ambayo itajenga kiwanda cha chuma kitakachogharimu Shilingi bilioni 36 na kutoa ajira za moja kwa moja 300 na kampuni nyingine ya Uturuki itajenga kiwanda cha mabati kitakachogharimu Shilingi bilioni 120 na kutoa ajira za moja kwa moja 300.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa Kongani hiyo kutoka kampuni ya Kamaka, Nelson Mollel amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha nchi kufunguka katika eneo la uwekezaji ambapo kasi hiyo ya ujenzi katika kongani hiyo umefanyika katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake na wanaendelea kuona matunda mema ya uwekezaji huo.
“Mradi huu unatekelezwa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza mradi umeshafikia asilimia 80, tayari tumeshazungusha uzio wa eneo lote la uwekezaji takriban KM 9, kuanza kwa ujenzi wa barabara za ndani KM 16.16, ujenzi wa kituo cha Polisi, jengo la Zimamoto na Uokoaji na hosteli za makazi ya Maafisa, jengo la utawala pamoja na Zahanati, uwekezaji huu utakapokamilika utaongeza Pato la Taifa na fedha za kigeni kwa takribani zaidi ya Shilingi trilioni 3.12.” Alisema Mollel
Kwa upande wake mnufaika wa ajira katika ujenzi wa Kongani hiyo, Elias Salmin ambaye ni fundi ujenzi amesema kuwa kutokana na ajira aliyoipata, ameweza kujitegemea na kuendesha maisha yake tofauti na mwanzo hali ilivyokuwa kwani mtaani ajira za kila siku zimekuwa ngumu kupatikana.
Mradi huu ni wa Mwekezaji wa Kitanzania ajulikanae kama Kamaka Company Limited ambaye amewekeza katika ujenzi wa miundombinu wezeshi katika kongani hiyo ili kurahisisha uwekezaji wa viwanda kwa watu wanaohitaji.