Majuzi Rais Dk. John Pombe Magufuli alitimiza siku 100 tangu alipoingia madarakani Novemba 5, mwaka jana.
Watu wengi wamejitahidi kuchambua utendaji wa Rais Magufuli katika siku hizo 100. Ingawa hawakukosekana watu waliomkosoa, wengi wamesifu utendaji wake katika kipindi hiki.
Karibu watu wote wamechambua utendaji wa jumla wa serikali chini ya uongozi wa Dk. Magufuli. Lakini tusije tukasahau kwamba utendaji mzuri wa kila wizara ndio unaofanya utendaji wa serikali nzima uonekane kuwa bora.
Binafsi nimefuatilia utendaji wa wizara mbili katika siku hizo 100. Nimeona kama hazikuwapo. Kwa maneno mengine sikuona utendaji wa wizara hizo. Wizara hizo ni ile inayosimamia masuala ya watoto na ile inayosimamia masuala ya walemavu.
Inawezekana wizara hizo zimefanya kazi huko mikoani. Lakini Dar es Salaam hazikufanya kazi yoyote. Mimi sikuona. Ndiyo maana nimelazimika kuuliza katika siku 100 za utawala wa Dk. Magufuli wizara hizi zilikuwa wapi?
Tuanzie na wizara inayosimamia masuala ya watoto. Na hapa sizungumzii Wizara ya Elimu ambayo inasimamia watoto au wanafunzi wa shule. Nazungumzia wizara inayosimamia masuala ya watoto wote walioko shuleni na nje ya shule.
Watu wamesema kuona ni kuamini. Kama wizara inayosimamia masuala ya watoto ingekuwa inafanya kazi tusingeendelea kuona mambo tunayoyaona barabara za Dar es Salaam.
Katika baadhi ya barabara za Dar es Salaam ombaomba watoto wanasumbua sana wanaoendesha magari. Maeneo sugu ya ombaomba watoto ni mtaa wa Bibi Titi Mohamed mbele ya Maktaba Kuu ya Taifa mpaka Mnazi Mmoja mbele ya uwanja wa mashujaa, na barabara ya Morogoro eneo la Magomeni jirani na Msikiti Mkuu.
Katika maeneo haya watoto wanavamia magari na kugonga vioo. Kwa kweli wanaleta usumbufu mkubwa. Tena wanajihatarisha kukanyagwa na magari.
Si hivyo tu. watoto hawa wakubwa na wadogo inaonekana hawatakwenda tena shule. Juu ya yote wanakulia katika kujifunza kwamba mtu anaweza kuendesha maisha yake kwa kuomba tu! lakini pia hapana shaka watoto hawa wanaweza kufikia umri ambao wataona kwamba kazi ya kuomba haiwafai tena. Kwa hiyo vijana wa kiume watakuwa majambazi na wale wa kike watakuwa machangudoa. Taifa litakuwa limeshindwa kulea watoto wake.
Nimewasikia watu wakisema kwamba serikali inafuga tatizo ambalo inaweza kulimaliza. Watoto hawa wanasumbua watu barabarani huku mama zao wakiwa wameketi kando ya barabara wakisubiri kuletewa mapato na watoto hao.
Kama serikali ikitaka kumaliza tatizo hili ikamate watoto. Watoto wataonesha wazazi wao. Wazazi wao ambao wote ni akina mama wakitishwa na kuambiwa kwamba wakikutwa tena wameketi maeneo hayo watashitakiwa hapana shaka usumbufu wanaoleta watoto hawa kwa wenye magari utakwisha.
Tukumbushane kwamba watoto hawa wanalitia aibu taifa letu kwa mambo mawili.
La kwanza. Wanaleta usumbufu hata kwa wageni wenye magari wanaotumia barabara zetu. Lazima wanajiuliza kama taifa letu halioni kwamba watoto wetu wanaharibika?
La pili. Ingawa tumeamua kutoa elimu bure kutokana na umuhimu wake hapa tunaruhusu watoto wasiende shule na badala yake washinde barabarani wakiomba.
Tunaendeleza tatizo hili kwa uzembe wetu. Ni tatizo ambalo halihitaji msaada wa fedha kutoka nchi za nje.
Halafu kuna hili tatizo la ombaomba walemavu. Eneo sugu kwa tatizo hili ni barabara ya Ali Hassan Mwinyi kuanzia kituo kidogo cha Polisi cha Selander mpaka Maktaba Kuu ya Taifa.
Ulemavu walionao ninaowazungumzia hapa kwa wengi sio wa kushindwa kufanya kazi. Wengi wamelemaa miguu. Hawakulemaa mikono. Kwa hiyo kama wizara inayohusika na suala la walemavu ikiandaa mipango mizuri inaweza kuwakusanya walemavu hawa na kuwawezesha ili wafanye kazi badala ya kushinda kando au katikati ya barabara wakiomba.
Tunajua kwamba serikali inatambua aibu ambayo taifa linapata mbele ya wageni kutokana na ombaomba hawa walemavu wanaozagaa barabarani.
Tuchukue, kwa mfano. Wakati wa ziara ya Rais Obama wa Marekani serikali iliwakusanya ombaomba wote ikaenda kuwaweka uwanja wa taifa na kutumia gharama kubwa kuwalisha wakati wote wa ziara ya Rais huyo ili msafara wake usijue kuwa Tanzania tunaruhusu ombaomba wazagae katika barabara zetu.
Basi siku 100 zimekwisha na tumeshindwa kuona kazi za wizara hizo mbili. Tunataka tuone kazi za wizara hizo katika siku 100 tulizozianza.