Waziri wa Nishati,January Makamba ameeleza kuwa, Juni mwaka huu utafanyika uzinduzi wa kitaifa wa Dira ya Taifa ya kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia na Mpango Mkakati wa utekelezaji wa Dira hiyo ambayo itaainisha masuala mbalimbali ikiwemo hatua ambazo Serikali itachukua ili kuwezesha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.
Waziri Makamba aliyasema hayo jijini Dodoma wakati akitoa elimu ya nishati safi ya kupikia kwa Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) pamoja na Wenyeviti na Makatibu wa UWT wa Mikoa na Wilaya ambao watasadia kulipa msukumo suala hilo na kusambaza elimu husika katika ngazi ya Kata na Matawi nchi nzima.
“Takwimu zinaonesha kuwa,asilimia Nane tu ya Watanzania ndio wanatumia nishati safi ya kupikia hivyo,Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo kuwa ndani ya miaka 10 asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, ameshatuelekeza tutengeneze Dira.
“Mkakati na Mwelekeo na pia kuanzisha mfuko wa nishati safi ya kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi, hii ni kazi kubwa lakini inawezekana na kazi inaendelea.” amesema Makamba.
Ameeleza kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kulivalia njuga suala la nishati safi ya kupikia ikiwa ni moja ya jitihada zake za kuboresha maisha ya Watanzania hasa kinamama.
Makamba amesema kuwa,ustawi wa mwanamke wa Tanzania unahatarishwa na namna anavyotafuta nishati na aina ya nishati anayopikia, “Wataalam wanasema lisaa limoja jikoni ni sawa na sigara 300 sasa hapa unategemea ustawi utatoka wapi?, bahati nzuri Rais ameliona hili na kwa Wizara ya Nishati,suala Nishati ya kupikia ni jambo namba moja la kutekeleza ili kuleta ustawi ulio bora nchini.”
Amewaeleza wajumbe hao pia athari mbalimbali zinazotokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia kama vile kuni ambapo alitaja athari hizo kuwa ni pamoja na magonjwa katika mfumo wa upumuaji, mazingira hatarishi wakati wa kutafuta kuni, wanyama hatarishi na athari katika masomo kwa watoto wa kike kwani badala ya kutumia muda mrefu kusoma, muda mwingi wanautumia kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia.
Katika kuhakikisha kuwa, kazi hiyo ya uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia inafanyika kwa ufanisi, Waziri Makamba ametoa mitungi 400 ya gesi ya kupikia kwa UWT kila mkoa nchini pamoja mitungi 1500 kwa UWT Makao Makuu ili waweze kuitumia katika uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT, Mary Chatanda amemshukuru Waziri wa Nishati kwa kutoa elimu hiyo ambayo Wajumbe hao wataitumia kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika ngazi za chini.
Mgeni rasmi katika Mkutano huo alikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM),Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana.