Na Mwandishi Wetu, JAMHURI MEDIA

Mchungaji mmoja kutoka nchini Uganda amefunga kanisa lake baada ya kushinda sh. Milioni 100 kwenye mchezo wa bahati nasibu (betting).

Machi 16, mwaka huu, mtandao mmoja Uganda ulichapisha taarifa za mchungaji huyo akieleza kuwa ameamua kufunga kanisa lake ili afanye shughuli nyingine kwa kuwa amepata fedha nyingi.

Mtandao huo ulimnukuu mchungaji akieleza namna alivyocheza bahati nasibu ya Sh. milioni moja lakini akashinda Sh. milioni 100 ambazo hakutarajia kama angepata.

Kwa mujibu wa taarifa ya vyombo mbalimbali vya habari nchini humo, mchungaji huyo aliamua kufunga kanisa lake ili afanye shughuli nyingine kwa sababu sasa ni tajiri.

Mchungaji huyo alikiri kuwa alifungua kanisa hilo kwa sababu ya tamaa na wala sio upako.

“I must admit that I opened this church due to greed but not anointing (lazima nikiri kwamba nilifungua kanisa hili kwa sababu ya ‘tamaa’ na sio upako) inasema sehemu ya habari hiyo ikimnukuu mchungaji huyo.

Mchungaji huyo aliongeza kuwa alilazimika kufunga kanisa kwa sababu alikuwa na njia zake za kupata pesa na kufikia sasa amefanya mambo mengi ambayo hakuwahi kufikiria kama angeweza kuyafanya maishani mwake.