Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Dkt.Stergomena Tax kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan amekabidhi rasmi msaada wa kibinadamu kwa Serikali ya Malawi kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa kimbunga Freddy kilichosababisha mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo tarehe 13 Machi,2023 na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo vya zaidi ya watu 400.
Msaada huo umekabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Dkt.Lazarus Chakwera leo Machi 20,2023 katika hafla fupi iliyofanyika katika Ikulu ya Rais jijini Lilongwe na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Malawi na Tanzania akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Nancy Tembo na Balozi wa Tanzania nchini humo,Humphrey Polepole.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Dkt. Tax amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia ametoa msaada wa kibinadamu na salamu za pole kwa Rais wa Malawi,Dkt. Lazarus Chakwera pamoja na wananchi wa nchi hiyo kwa madhara makubwa waliyoyapata kutokana na mafuriko hayo ikiwemo vifo, majeruhi, ukosefu wa makazi pamoja na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu ikiwemo barabara.
Amesema Tanzania kama ndugu, rafiki na jirani wa Malawi imeguswa na janga hilo na kuchukua hatua za haraka za kuratibu msaada huo kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo ili kuwathibitishia kwamba Tanzania ipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.
“Mhe.Rais Samia amenituma Malawi kuwasilisha ujumbe maalum wa salamu zake za pole na msaada wa kibinadamu kwa Mhe. Rais Dkt. Chakwera na Wananchi wa Malawi kufuatia madhara yaliyotokana na Kimbunga Freddy ambacho kimeleta maafa makubwa. Kama ndugu zetu na jirani zetu Tanzania inasimama na Malawi katika kipindi hiki kigumu cha mpito na leo nimewasilisha msaada huo na pia kutoa pole kwa niaba ya Mhe. Rais Samia na Watanzania” amesema Dkt. Tax.
Msaada wa kibinadamu uliotolewa ni fedha taslim na vifaa mbalimbali wenye ya thamani ya Dola za Marekani Milioni Moja. Msaada huo pia unajumuisha chakula, vifaa vya kuokolea, vifaa vya kujihifadhi, Helikopta 2 za kijeshi zitakazotumika kupeleka misaada katika uokoaji pamoja na wanajeshi 100 watakaoshiriki kusambaza msaada huo; Mahema 50; Blanketi 6,000; Tani 1,000 za unga wa mahindi na fedha taslim kiasi cha Dola za Marekani 300,000.
Kwa upande wake, Rais wa Malawi,Dkt. Lazarus Chakwera amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wananchi wa Tanzania kwa msaada uliotolewa kwao na kueleza furaha yake kwamba msaada huo umewafikia kwa haraka na kwa wakati.
Amesema msaada huo ni ishara ya undugu na mshikamano uliopo kati ya Tanzania na Malawi na kukumbusha kwamba hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuisiadia Malawi kwani iliwahi kufanya hivyo mwaka 2015, mwaka 2019 na mwaka huu 2023.
Waziri na ujumbe wake wamerejea nchini baada ya kukabidhi msaada huo.