Pokea salamu za upendo na heri ya mwaka mpya 2016, wewe msomaji wa gazeti JAMHURI na safu ya FASIHI FASAHA. Pili, naomba radhi kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu uliikosa safu hii kutokana na mimi mwandishi kufanyiwa operesheni ya jicho. Namshukuru Mwenyezi Mungu kuniponyesha na tiba za madaktari. Amin! Wiki iliyopita vyombo vya habari vyote nchini, vilirembeshwa na habari za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dokta John Pombe Magufuli kutimiza siku mia moja za utawala na uongozi.
Muda huo umezungumzwa katika mitazamo miwili iliyotofauti ya hasi na chanya.
Mitazamo hiyo iliyotolewa na wananchi wa taifa hili huru la Tanzania chini ya ushawishi na mayowe kutoka vyama vya siasa, baadhi ya wanaharakati bila ya kuwasahau wanasheria na wanadiplomasia kupitia vyombo vya mawasiliano na umma.
Sina haja kuorodhesha mifano ya mitazamo hiyo kwa sababu ya ukweli wote tunafahamu. Kwani kurudia kutaja ni kupoteza muda. Lakini ukweli uliyopo wananchi wote tulikuwa katika mchakato wa kupima na kutathimini umahiri wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa maana ya uwezo, ujasiri, umakini na uungwana katka kutimiza ahadi ndani ya kipindi kifupi hicho.
Wamo wananchi waliolala ndani ya mtazamo wa kongole na sifa; ambao wamekunwa na “kutumbuliwa majipu” kwa maana ya watuhumiwa kutiwa mahabusu na kufikishwa mahakamani. Wengine vibarua vyao kuota nyasi n.k. kutokana na utamu wa kula rushwa na udora wa kubembea ndani ya kiti cha ufisadi.
Kadhalika, wapo waliokesha kwenye mtazamo wa shutuma na kubeza waliochukizwa na “Hapa Kazi Tu” kuona kana kwamba ni kufanya udikiteta.
Matukio ya kubomolewa nyumba zilizojengwa kinyume na sheria na maeneo hatari, watumishi wa umma kupuuza kufuata maadili ya utumishi kuadhibiwa na wale wahujumu uchumi pamoja na majangili kutiwa ngomeni. Watetezi wanaona eti hatua hizo ni udikteta!
Baada ya kukumbusha machungu hayo, napenda kusema PENYE TITI PANA TITI KATIKATI YA TITI. Wote hao wenye mitazamo tofauti juu ya utawala wa Awamu ya Tano, wana yao ndani ya nafsi zao. Wote wanapenda kunyonya maziwa isipokuwa wanatofautiana njia za kunyonya hilo titi.
Mathalani, wapo baadhi ya Watanzania wenzetu wanapenda sana kutawala na kuongoza lau kama wanajitambua hawawezi na hawatakiwi kwa sababu hawana sifa na uadilifu.
Hadi leo bado wanaamini wanaweza kuongoza ili hali wapo weupe. Wanaloweza ni ung’ang’anizi, ulaghai na kilio ili waonewe huruma wawekwe katikati ya titi bila kutambua penye titi pana titi na wananchi wameshajizatiti kuwakataa. Cha ajabu hata wale wapambe wao wapiga chapuo, ngezi, nzumari na kayamba wanatambua hao wanaowashabikia hawana sifa na uwezo.
Kwa vile walishalipwa fedha za kupiga ala hizo, hawana budi kufanya kazi. Hata kama wanajua fika si kila mtu anaweza kuwapo katikati ya titi. Siku 100 za utawala wa Rais Magufuli unalaumiwa pia kwa vipi hauingilii na kutanzua mgogoro wa kisiasa ulioko Zanzibar. Wapo wanaomtaka Rais aseme neno la kutorudia uchaguzi na badala yake atangazwe aliyepata kura nyingi za urais wa Zanzibar.
Rais Magufuli naye haoni sababu ya kutamka hivyo au kuingilia kati mgogoro huo kwa sababu tu ni Rais wa muungano. Anachoeleza kuwa penye titi pana titi hawezi kuwa katikati ya titi. Anavitaka vyombo na watu husika kutambua lilipo titi na watanzue namna ya kunyonya hilo titi. Ushauri wangu tulio nje ya Zanzibar tulitazame suala hilo kwa makini na uzalendo wala si kwa ushabiki wa kisiasa, mihemko ya kiharakati au kisheria za mpururu mparara.
Tuzame ndani ya siasa za Pemba na Unguja na sheria timilifu. Tukiri baadhi ya Watanzania ni wapya katika masuala ya visiwa vya Pemba na Unguja. Hadhari ichukuliwe.
Nimalizie kwa kusema ndani ya siku hizo 100 Serikali imetuonyesha dhamira ya kurudisha heshima ya Mtanzania na kuondoa unyonge wa kuwa ombaomba ili hali uwezo tunao wa kupanga mipango kwa kwa kutegemea chetu kichopo kibindoni kwa sababu mkwiji wetu sasa alhamdulillahi !!
Tuupe nguvu utawala wa Awamu ya Tano uweze kufanikisha mipango yake penye titi pana titi katikati ya titi. Tafakari!.