Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Njombe
Malori kadhaa yaliyokuwa yakitoka vijijini kubeba mizigo mbalimbali katika maeneo ya Luponde Halmashauri ya Mji wa Njombe yametekwa na watu wasiofahamika na kuwachapa viboko madereva ili kuwashinikiza kutoa fedha.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Hamis Issah amesema kuwa tukio hilo limetokea Machi 18, mwaka huu, majira ya saa 4 usiku maeneo ya Luponde mkoani Njombe.
Amesema kuwa kutokana na tukio hilo Jeshi la Polisi linaendelea kufanya doria ili kuwabaini wahalifu, kwani mbali ya kuwachapa viboko madereva hao pia waliwataka kutoa fedha kwa nguvu na mara baada ya kutekeleza uhalifu huo walitoweka.
“Jana usiku gari zilikuta magogo yamewekwa barabarani ambayo ni miti iliyokatwa kwa ajili ya kutengeneza barabara jambo lililowalazimu kutelemka kwa nia ya kuyatoa.
“Kitendo cha madereva hao kutelemka ndipo wahalifu walipopata mwanya wa kuwakamata na kuwachapa viboko kisha kuwapekua na kuchukua fedha kwa madereva hao huku wakiwatishia kwa silaha.
“Wakati zoezi hilo linafanyika magari yalikuwa mengi, baadaye lilikuja gari la maji ambalo nalo walikuwa wakilisubiri kwa kuwa ilitoka kwenye mauzo ya maji na kuwapora sh.laki nane hivyo ukijumla na fedha za madereva wengine wa malalori zinakuwa zaidi ya milioni 1,500,000″alisema Kamanda Issah.
Aidha kamanda Issah amesema hakuna madhara yeyote yaliyotokea kwa binadamu wala magari na tayari yameendelea na safari huku akiahidi kupanga mikakati zaidi na madereva pamoja na madalali ili kuhakikisha wanakuwa salama wanaposafirisha mizigo yao.
Tukio hili linajiri ikiwa ni takribani wiki tatu zimepita tangu ulipotokea utekaji wa malori ya mizigo yaliyokuwa yakitoka mnadani pamoja na basi la abiria katika eneo la kati ya Nyombo na Kidegembye huko Lupembe wilayani Njombe.