Na Mwandishi Wetu-Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linaendelea na operesheni maalumu ya kuwasaka watu wanaojihusisha na uhalifu ambapo kupitia operesheni hiyo pamoja na taarifa toka kwa wananchi tumefanikiwa kukamata bastola moja aina ya CZ 75 LUGER yenye namba za usajili A487385 pamoja na risasi 71 za bastola iliyokuwa inatumiwa na wahalifu.
Silaha hiyo pamoja na risasi zilipatikana nyumba iliyopo huko maeneo ya Ilkyurei, Kata ya Kiranyi, wilaya ya Arumeru na Mkoa wa Arusha baada uwepo wa taarifa toka kwa wananchi kuhusiana na wahalifu hao.
Aidha wahalifu hao walikimbia baada Polisi kukaribia kufika katika nyumba hiyo na tunaendelea kufanya upelelezi ili kuwakamata.
Sambamba na hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linatoa onyo kwa watu wachache wanaojihusisha na matukio ya uhalifu kuacha mara moja kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Pia tunawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kudumisha hali ya usalama katika mkoa wetu.
Wakati huo huo,katika operesheni hiyo kwa nyakati tofauti wamefanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 11 wakiwa na mirungi bunda 528 yenye uzito wa kilogramu 162.97 ambayo walikuwa wakiisafirisha kwa kutumia vyombo vya moto ikiwemo gari pamoja na pikipiki.
Upelelezi wa matukio hayo bado unaendelea, na pindi utakapokamilika majalada yatapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi.
Pia,Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka limefanikiwa kumfikisha mahakamani mtu mmoja aitwaye Julius Raphael Mollel (27) mkazi wa kijiji cha Lashaine wilaya ya Monduli kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi (jina limehifadhiwa) (08) wa darasa la pili ambapo tarehe 06.03.2023 alikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Aidha Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha linaendelea kukutana na wananchi pamoja na viongozi wa kata, mitaa pamoja na vijiji kwa lengo la kutoa elimu kuhusiana na ukatili wa kijinsia pamoja na masuala ya usalama ikiwemo umuhimu wa kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi katika maeneo yao ili kukomesha matukio ya uhalifu.
Pia tunaendelea kutoa wito kwa wananchi kutojihusisha na vitendo vya ukatili kwani hatutamuonea muhali mtu yoyote atakayebainika kujihusisha na makosa ya unyanyasaji.