Tangu shule zimefunguliwe Januari, mwaka huu na Serikali kuanza kutekeleza sera ya elimu bure darasa la kwanza hadi kidato cha nne, kumetokea mambo mengi.
Tumesikia wakuu wa shule katika maeneo kama Mwanza, Kagera na Kilimanjaro wakifukuzwa kazi kwa kuchangisha wazazi baadhi ya michango. Mbaya zaidi Watanzania wengi wamelipokea visivyo suala hili.
Tunapata taarifa nyingi kutoka sehemu mbalimbali za nchi wazazi walio wengi hawaelewi kama chekechea nao wamo katika mpango wa elimu bure au la. Si hilo tu, tunapata taarifa nyingi kuwa baadhi ya wakuu wa shule wamepokea Sh 29,000 kama fedha za kuendesha shughuli zote za shule.
Wazazi walikuwa wanachangia ulinzi, uji kwa watoto, chakula cha mchana na mambo mengine yanayogusa watoto wao, nao wamesusa.
Tumesikia jijini Dar es Salaam kuwa baadhi ya shule wezi wameingia na kupora madawati, viti na meza katika baadhi ya shule kwani hazina ulinzi na wakuu wa shule hawana fedha za kulipa walinzi.
Tumepokea taarifa kutoka katika baadhi ya mikoa kuwa wazazi wanakwenda shuleni kudai watoto wapewe sare, kalamu na madaftari.
Yapo mengi yanayoelezwa katika mkanganyiko huu. Kwa jinsi hali ilivyo tunapata wasiwasi kuwa mpango huu usipopitiwa na kuangaliwa kwa karibu, unaweza kuwa na madhara makubwa kwa elimu ya taifa letu kuliko faida za kisiasa. Idadi ya watoro itaongezeka, kwani hata watoto waliokuwa wanapata chakula shuleni kwa sasa hawapati.
Sisi tunasema kutokana na sintofahamu kubwa inayoendelea, Waziri wa Elimu Prof. Joyce Ndalichako anapaswa kutoa mwongozo wenye kufafanua kwa kina katika mpango wa elimu bure serikali inalipia nini, na kipi wazazi wanawajibika kulipa.
Tunasema, bila kufanya hivyo tutawatwisha mzigo mkubwa wakuu wa shule na kuwajengea uhasama na jamii kwa gharama ya kuharibu elimu nchini.