Kumekuwa na matukio mbalimbali ambayo Polisi wametumiwa vibaya na Serikali, taasisi na watu wengine.
Hali hii imetufikisha mahali ambako ile kauli ya siku nyingi kwamba polisi ni usalama wa raia inaonekana haina maana tena.
Tumeshuhudia wakati wote polisi wakizuia maandamano ya wapinzani kwa madai wamepata taarifa za kiintelijensia.
Kumbe maandamano ni njia halali ya wanananchi kutaka jambo fulani lisilo na maslahi kwao na kwa taifa lisifanyike.
Lakini pia ni njia ya kupinga jambo fulani lililofanyika.
Kwa hiyo maandamano ni haki ya ya raia kote duniani kote, lakini leo haki hiyo ya raia ya kuandamana inapigwa vita na serikali kwa kutumia polisi.
Polisi wa Tanzania wanakubali kutumiwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushiriki ushindani wa kisiasa. Basi kutokana na kitendo hiki cha Polisi kushikilia maandamano yasifanyike watu wanachukua sheria mkononi.
Wanaamua kuandamana bila kujali matokeo yake. Hapo polisi hutumia nguvu kubwa kupambana na wananchi wasio na hatia.
Wanapiga virungu wananchi, wanapiga mateke, wanawakokota juu ya ardhi mfano wa mnyama aliyekufa na wanawamwagia maji ya upupu.
Hivi kama watu wanaandamana kwa amani katika nchi inayodai ni ya kidemokrasia nguvu ya polisi inakujaje?
Ukafika uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Tulishuhudia tena polisi wakitumiwa vibaya.
Rais aliyekuwa madarakani hakumpenda Edward Lowassa (na inawezekana bado hampendi). Huo ni ukweli.
Na alihisi kwamba angeshinda uchaguzi ule. Akahofu kwamba angeingia matatani kama Lowassa angekuwa Rais kwahiyo aliamua kutumia nguvu kubwa ya polisi kuhakikisha kwamba Lowassa hapati urais.
Rais huyo alitumia fedha nyingi kununua magari na vifaa vingine kutoka nchi za nje huku hospitali zetu zikiwa hazina dawa na baadhi ya wagonjwa wakilala sakafuni.
Wakati wa kampeni Rais huyo akapiga kelele kila siku kuwataka wananchi wasikaribie vituo vya kupigia kura. Watanzania ni wapenda amani. Basi watu wakabaki wanajiuliza kwa nini itumike nguvu kubwa ya polisi kuhakikisha kwamba wananchi hawakaribii vituo vya kupigia kura?
Kumbe yalikuwa maandalizi ya wizi wa kura! Polisi walikubali kutumiwa kuvuruga demokrasia nchini. Katika nchi ya demokrasia majeshi hawajihusishi na ushindani wa kisiasa.
Likaja zoezi la bomoa bomoa jijini Dar es Salaam. Huku wakijua kuwa hawajawahi kuwafuata wananchi wa maeneo mbalimbali kuwaambia kuwa hawatakiwi kuishi maeneo hayo basi watu wa mazingira waliamua kutumia polisi katika kutekeleza zoezi lao la kuweka X kwenye kuta za nyumba za wananchi.
Tunadhani wakuu wa polisi wamepitiliza katika kulinda nafasi zao za kazi kiasi katika Tanzania ya leo Polisi hawana jina zuri. Huo pia ni ukweli.
Tunatambua wajibu wa polisi wa kutekeleza amri na maagizo ya Rais hata kama hayana maslai kwa wananchi. Lakini wanapotakiwa na watu wengine wakatekeleze jambo fulani ni vyema wakajiuliza maswali kuhusu uhalali wa wao kushiriki zoezi au jambo hilo.
Kwa mfano, zoezi la bomoa bomoa kulikuwa na maswali mawili ambayo polisi walipaswa kujiuliza kabla ya kwenda kuwatia misukosuko wananchi wasio na hatia.
La kwanza, kama wananchi wameendelea kuishi maeneo waliyotakiwa kuhama siku nyingi ulikuwa ubinadamu kuwataka watumie dakika kumi tu kuondoka kwenye nyumba zao?
Tumeshuhudia baada ya kutekelezwa zoezi hilo lililokosa ubinadamu serikali ilitoa majuma mawili kwa wananchi kuondoka kwenye maeneo hayo.
Je, polisi wasingeweza kuishauri serikali kwamba dakika kumi ulikuwa muda mfupi mno kuwataka wananchi waondoke kwenye maeneo waliyoishi miaka na miaka?
La pili, polisi walipotakiwa kwenda kusimamia zoezi la kuweka X kwenye nyumba za wananchi walipaswa waulize kama hao wa mazingira waliwahi kwenda kuwaelimisha wananchi kwamba ingawa walijenga nyumba zao maeneo hayo kabla sheria ya kulinda mazingira haijatungwa sasa walitakiwa wahame.
Kwa kuwa watu wa mazingira waliona kwamba wanakwenda kutekeleza zoezi lisilo halali waliamua kutumia polisi.
Na Polisi wakakubali kwenda kushiriki zoezi la kunyanyasa wananchi. Hii ni kasoro tena kubwa.
Majuzi likaja tukio la Bungeni. Uongozi wa Bunge ulisindwa kufanya mambo ya kuridhisha kambi ya upinzani. Ukaamia kutumia polisi.
Uongozi wa Bunge ulitumia polisi zaidi ya 50 na mbwa kuwatoa Bungeni wabunge wa upinzani.
Sisi sote tunajua kwamba Bunge lina hadhi yake, lina kinga, lina haki zake na lina wajibu wake. Sasa kama halipati haki zake ni wazi viongozi wa Bunge watashindwa kuliendesha.
Na wakishindwa kulinedesha ni vyema wakajiuzulu badala ya kutumia polisi kuwadhalilisha hata wabunge wanawake.
Wakuu wa polisi wamepitiliza katika kulinda nafasi zao za kazi. Kwa hiyo wanashindwa kujiuliza maswali kabla ya kushiriki mazoezi yasiyo halali.