Na Eleuteri Mangi, JamhuriMedia,Dodoma
Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo inawasisitiza wazazi, walezi na walimu kuzingatia maadili katika malezi ya watoto nyumbani,shuleni na vituo vya malezi ili kutoa huduma ya malezi kwa watoto kwa kuzingatia maadili ya Mtanzania.
Hayo yamesemwa na Afisa Utamaduni Tito Lulandala wakati akitoa mada kwa niaba ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye mafunzo ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa walimu, walezi na wamiliki wa vituo vya malezi (day care centres) na shule za awali hivi karibuni jijini Dodoma.
Lulandala amesema kuwa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo inatarajia washiriki wa semina hiyo watakuwa mabalozi wa maadili kwa watoto kwa sababu wanafahamu kuwa watoto hujifunza vyema katika umri wa awali pia hujifunza zaidi katika mazingira yanayowazunguka na kutoka kwa watu walio karibu yao.
“Kwa hiyo, zungumza ya watoto, tembea yao, mitazamo yao juu ya mambo mbalimbali katika jamii itategemea jinsi wanavyoiona mienendo yenu ninyi wazazi na walezi, kwa mfano wewe mlezi ukivaa kinguo kifupi kisicho na staha, mtoto wa kike naye anaiga” amesema Lulandala.
Ameongeza kuwa Serikali inatarajia malezi yanayotolewa na wazazi na walezi yatawafanya watoto kuyatafsiri maisha katika muktadha wa utamaduni wetu na watajua kupitia walezi hayo kuwa mwanamke ni nani na mwanaume ni nani katika jamii.
Malezi hayo kwa muktadha wa utamaduni wetu yatawaelekeza kinagaubaga kuwa mwanaume hapaswi kutenda na kutendewa nini na mwanamke hapaswi kutenda na kutendewa nini na kusisitiza kuwa hakuna baba mwenye jinsia ya kike na hakuna mama mwenye jinsia ya kiume. Hiyo ndiyo dhana halisi ya familia katika muktadha wa utamaduni wa Mtanzania.
Akifunga mafunzo hayo, Baraka Makona kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na mambo mengine alisisitiza kuwa wizara na taasisi zenye dhamana na usimamizi wa maadili kushirikiana vyema ili kukabiliana na tatizo la mmomonyoko wa maadili ambalo linachangia vitendo vya ukatili kwa watoto ikiwemo ulawiti na ubakaji na kuwaagiza waandaji wa mafunzo hayo kila mara wanapotoa mafunzo au semina wahakikishe mada ya maadili iwe miongoni mwa agenda katika programu zote za mafunzo.
“Ni matarajio ya Serikali, baada ya Semina hii, mtakuwa mabalozi wazuri wa kuwahamashisha wazazi kuwajibika katika malezi ya watoto wao. Vituo vya kulelea watoto na shule wanawajibu wa kujumuisha mada zinazohamasisha uwahjibikaji wa wazazi na walezi kwenye malezi ya watoto. Kila mara mnapokuwa na mikutano au vikao vya wazazi hakikisheni mnakuwa na mada zinazohamasisha uwajibikaji wa wazazi katika malezi bora ya watoto yanayozingatia maadili yetu” amesema Bw. Makona.