Kelele za hapa na pale zimeanza kusikika miongoni mwa Watanzania zikielekezwa kwenye uongozi wa Rais John Magufuli.
Wapo walioanza kulia wakisema amekuwa dikteta. Hii inatokana na kasi yake ya ‘kutumbua majipu’, kukaidi vishawishi vya safari za nje, kuwabana wakwepa kodi, kuwafurusha wahamiaji na wanaoishi nchini kinyume cha sheria na kuwashughulikia watendaji wazembe, mafisadi na wabadhirifu wa mali za umma.
Akili ya kawaida inanifanya niamini mtu kama Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, hawezi kufurahia yote yanayofanywa na Rais Magufuli. Hawezi kufurahi, na ndiyo maana badala ya kumsema Magufuli moja kwa moja, ameona atumie kisingizio cha magazeti kadhaa kudai eti yanatumiwa na anaowaita ‘wapinzani walioshindwa’ kumwandama.
Mheshimiwa Kikwete, hawezi kufurahi kuona viongozi wengi wabovu aliowalea, akiwamo ndugu yake Madeni Kipande aliyemlinda kwa kila hali, Magufuli akiwaondoa bila kupepesa macho.
Kikwete hawezi kufurahi kuona mfumo alioubariki wa kuwatukuza wakwepa kodi, sasa ukifumuliwa katika Bandari na kwa wakwepa kodi wengine aina ya Lake Oil.
Lakini ni nani kati ya wale walioishi nusu ya miaka 10 wakiwa angani na ughaibuni, wakilala hoteli za nyota tano wakiambatana na vimwana; wanaoweza kumfurahia Rais Magufuli, kwa kufuta uhondo huo?
Mawaziri wale waliokwenda Marekani mara tatu hadi nne kwa mwezi mmoja, watamshangilia Rais Magufuli? Wale ambao hawakujua mshahara ni nini, au hata waliofikia hatua ya kuuliza: “Hivi mshahara tunaolipwa siku hizi ni kiasi gani?”, wakaishi kwa marupurupu manono mno ambayo leo yamekoma, hao watampenda Magufuli kweli?
Wengine wamekosoa busara ya Rais Magufuli, ya kuuwezesha mhimili wa Mahakama kifedha ili mahakimu, majaji na watumishi wengine wapate vitendea kazi, na hivyo kuharakisha uamuzi wa kesi na mashauri mengi mno yaliyokwama kwa ukata.
Pamoja na ukweli wa kinadharia wa kuwapo mihimili mitatu ‘isiyopaswa kuingiliana’ -Serikali, Bunge na Mahakama, bado ukweli unabaki kuwa rais ndiye kiongozi mkuu wa nchi. Kamusi inamtaja Rais kama: “Kiongozi mkuu KABISA wan chi ambayo ni jamhuri.”
Hatuwezi kuwa na Rais aliyefanikiwa kwenye serikali, na kufeli katika Mahakama na Bunge, halafu rais wa hiyo nchi akapata tuzo ya kuongoza vizuri! Tunaweza kwenda mbele, tukarudi nyuma, bado rais atakuwa ndiye kiongozi mkuu KABISA anayewajibika kwa kila linaloihusu nchi na ustawi wa mambo yake yote.
Wanaokosoa kitendo cha Rais Magufuli, kwa uamuzi wake wa kuiahidi Mahakama Sh bilioni 250 ili ‘iharakishe kesi’, sidhani kama wameutazama upande wa pili wa kujua namna maelfu ya wananchi wanavyotaabika kupata haki. Kuna kesi ‘nyepesi’ ambazo zimedumu kwa miaka 10 au zaidi bila kutolewa hukumu, ama kwa uzembe wa mahakimu na majaji kadhaa, au kwa sababu ya ukosefu wa vitendea kazi. Tunapompata kiongozi mkuu wa nchi anayekitambua na kukitafutilia jawabu kilio cha wananchi kwa upande mmoja, na kilio cha mahakimu na majaji kwa upande mwingine, tunakuwa hatuna jingine, isipokuwa kumuunga mkono.
Siku 100 za Rais Magufuli, Tanzania imeanza kuonyesha uhai katika nyanja nyingi. Kuna mwelekeo mzuri wa nchi.
Kama Rais Magufuli, ameamua kuwa dikteta ili Tanzania ifikie hatua ya kimaendeleo kama Malaysia, Singapore, au Korea Kusini, atakuwa amefanya jambo la maana mno. Kama udikteta wake ni wa kuhakikisha Watanzania wanaondoka kwenye lindi hili la ufukara na kuingia kwenye maisha ya kuzifaidi rasilimali zao, wengi tungeomba awe dikteta zaidi ya hivi alivyo sasa.
Kama binadamu, anaweza kufanya makosa. Kwa mfano, katika utumbuaji majipu anaweza kutumbua ambayo pengine si majipu. Kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere, kwamba unapofagia nyumba, pamoja na dhamira yako nzuri ya kufagia, unaweza kujikuta kwenye uchafu ukifagia na noti au sarafu. Pesa si kitu cha kutupwa pamoja na uchafu, kwa hiyo unapobaini kwenye uchafu ulioutupa kuna fedha, unachofanya ni kurejea jaani kuziokota hizo fedha na kuzitumia.
Hii ina maana kuwa Rais Magufuli, atakuwa msikivu na mtenda haki kwa kuwarejesha wale ambao kwa bahati mbaya wamekumbwa kwenye tumbua tumbua hii. Hao watakuwa sawa na fedha zilizojumuishwa kwenye uchafu, lakini baadaye zikachukuliwa.
Ndugu zangu, nchi yetu ilishaoza. Ilishaoza kuanzia serikalini, bungeni na mahakamani. Ilishaonza kwa kwa sababu hatukuwa na uongozi unaowajibika. Ripoti nyingi zilishathibitisha hilo.
Kuirejesha Tanzania kwenye mstari sharti kuwe na kiongozi ‘kichaa’ kama Rais Magufuli na ‘nunda’ aina ya Waziri Mkuu Majaliwa Kassim.
Nchi ambayo imeshindwa kuwa hata na shirika lake la ndege ilhali kila mara kuna fedha zimetengwa kwa shughuli hiyo, hiyo si nchi, ni balaa! Nchi ambayo ina rasilimali za kila aina, lakini ikawa na watoto wanaoketi chini kwa kukosa madawati katika karne hii ya 21, siyo nchi hiyo!
Nchi yenye walalamikaji kuanzia mtendaji wa kitongoji hadi rais wa nchi, si nchi hiyo. Hata nyumbu wanapoliwa na mamba mtoni huwa hawalalamiki au kukatisha safari, bali husonga mbele kwenda kule walikokusudia. Hatuwezi kuzidiwa maarifa au ujasiri na kiumbe kama nyumbu!
Malalamiko yanayosikika sasa ni dalili nzuri. Ni dalili kwamba tumempata kiongozi aliyejua jipu limekaa wapi na kwa mkao gani. Vijana wa mitaani wanasema ukirusha jiwe gizani, ukasikia kilio ujue limempata mlengwa!
Tanzania ina wasomi wengi. Ajitokeze msomi awaye yeyote atueleze nchi iliyopiga hatua bila kuwa na uongozi imara wa aina ya Magufuli. Tunasifu Marekani (taifa dogo kiumri kati ya mataifa ya dunia hii) kwa maendeleo yake. Tunatamani tuwe kama wao. Wajitokeze wasomi watueleze namna Marekani ilivyofika hapo. Je, imefika kwa kumbembelezana? Tunaposema Marekani kuna demokrasia, tuelezwe ni demokrasia gani waliyoibariki ya kukwamisha au kufifisha maendeleo yao? Demokrasia ya kulinda na kuwanyenyekea wezi iko nchi gani duniani?
Wapi walikoendelea ambako watu wakiambiwa wawahi kazini wanalalamika kuwa wanaonewa? Wapi duniani ambako wezi wa mali za umma wanaposhughulikiwa wanajitokeza wa kuwatetea? Wapi ambako kuna nchi yenye wananchi wanaomwambia rais wake “punguza spidi” ya kushughulikia mafisadi? Tunaitaka Tanzania ile ile ya Kikwete? Kama ndivyo, kwanini tulikuwa na uchaguzi mkuu? Kwanini Rais Magufuli alazimishwe kutumia staili ya Kikwete kuongoza?
Wakati tunapata Uhuru mwaka 1961, uchumi wa Tanganyika ya wakati huo, ama ulikuwa sawa, au uliuzidi wa mataifa mengi ya Asia, ikiwamo Korea Kusini. Kwanini Korea imetuacha mbali? Kunaweza kutolewa sababu nyingi, zikiwamo za nchi hiyo kukaribisha wawekezaji na kufungua milango ya biashara kutoka mataifa ya Magharibi.
Sawa, ebu tujiulize, Korea, au Singapore, au Malaysia zimetumia miaka mingapi kuimarika kiuchumi? Tanzania tumeingia kwenye mageuzi ya kiuchumi kwa miaka mingapi sasa? Kwanini hatukui? Kwanini tumeendelea kuwa kama mtoto aliyebemendwa?
Jibu ni rahisi tu. Wenzetu katika mataifa hayo walianza kupambana na ufisadi. Pili, wakafungua njia au milango ya uchumi na uwekezaji kwa jumla. Tatu, msamiati wa kulalalamika kwao ukawa mwiko; na nne walizingatia vipaumbele vya kuanza navyo, ili kwa kuvitumia, hiyo iwe injini ya kuyajenga mataifa yao.
Tanzania imekuwa kama pakacha. Kwa hali aliyotuacha nayo Kikwete, nchi hii angepewa mtu wa aina yeke, bila shaka ingekuwa vigumu mno kuendelea. Ni kama kujaza maji kwenye pakacha, sijui kama kuna siku yatafika pomoni! Nchi hii iligeuzwa kuwa dimbwi la utajiri ambalo wenye ruhusa ya kuteka kilichokuwamo ni viongozi, ndugu, jamaa, wafuasi wao na wazungu waliowaghilibu kwa vijizawadi. Magufuli si wa kushonewa suti au kulazwa hotelini Serengeti halafu akabariki kuuawa kwa wanyamapori 700 bila malipo.
Rais Magufuli, tunayemfahamu, hapa alipo wala hajaanza kazi! Mengi na makubwa yanakuja. Anapotuasa tumwombee kwa Mungu, hatanii. Ni aina ya kiongozi anayeamini kitu na kutenda kile anachoamini. Aliamini kwa kuomba uongozi wa nchi atawatumikia Watanzania. Hilo ndilo kaliweka mbele sasa. Ndiyo maana hadi wiki iliyopita, akiwa na wastani wa siku 100 madarakani, hajaenda kwao, Chato kusalimu! Anajua yeye si Rais wa Chato, isipokuwa wa Watanzania. Hajapanda ndege kwenda ughaibuni. Hili si jambo la kustaajabisha kwa sababu kwa miaka 20 akiwa Waziri, alisafiri nje ya nchi mara nne; na mara mbili hivi alienda Ulaya. Safari zake kwa miaka 20 nje ya nchi hazikuvuka sita! Kwenye uwaziri ambako ndiko kwenye ‘michongo’, na kwa kuzingatia Mheshimiwa Kikwete, alivyokuwa shabiki wa safari, angeamua kusafiri tusingepata barabara za lami. Kama wakati huo hakusafiri, leo lipi la kutushangaza hata tuone anafanya makosa kutosafiri?
Wahenga walisema “laana isiyo maana haimpigi mtu”. Rais Magufuli achape kazi. Watanzania wengi makabwela wako bega kwa bega na yeye kwa kuwa wanauona mwanga wa ukombozi. Dua za hawa makabwela ni za maana sana, na kwa hakika zitashinda hadaa, ghiliba na ghururi za wabaya wote. Tanzania mpya imewadia. Kama udikteta faida zake ni njema kwa Watanzania, Rais Magufuli, ebu ongeza dozi tupone.