Tanzania imeahidi kushirikiana na Jumuiya ya Madola kukabiliAna na changamoto za kidunia zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, Uviko 19, migogoro, ugaidi na umasikini.
Ahadi hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo aliposhiriki maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Balozi Shelukindo amesema licha ya uhusiano wetu na historia ya pamoja kama wanachama wa Jumuiya ya Madola tunaamini kuwa kwa umoja wetu tunaweza kuzikabili changamoto za kidunia kwa urahisi zaidi.
“Kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake kwa wakati, itakuwa rahisi kuzikabili changamoto za kidunia hususan mabadiliko ya tabianchi, Uviko 19, migogoro, ugaidi na umasikini,” alisema Balozi Shelukindo
Kwa Upande wake, Balozi wa Uingereza hapa Nchini, Mhe. David Concar amesema Jumuiya ya Madola imekuwa na mchango mkubwa kwa Tanzania hususan vijana ambao ndiyo taifa la kesho wamekuwa wakinufaika na ufadhili wa masomo kwa ngazi mbalimbali, biashara na uwekezaji pamoja na ajira.
Balozi Concar amesema Jumuiya ya Madola imefurahishwa na hatua ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikizichukua katika masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, ulinzi na usalama na utawala wa sheria.
“Tanzania imeboresha sana masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, ulinzi na usalama na utawala wa sheria….. mtakumbuka hivi karibuni mikutano ya kisiasa imeruhusiwa pamoja na uhuru wa vyombo vya Habari umeongezwa jambo ambalo linaashiria kukua na kukomaa kwa demokrasia,” alisema Balozi Concar.
Balozi Concar ameongeza kuwa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya biashara na uwekezaji nchini na hivyo kuchangia uchumi wa Tanzania kukua.
Maadhimisho ya siku ya Jumuiya ya Madola yamehudhuriwa pia na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba pamoja na baadhi ya wanamichezo wa Tanzania walioshiriki kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola.
Maadhimisho yameongozwa na Kauli Mbiu isemayo ‘Kujenga mustakabali endelevu na wenye amani wa pamoja’.