Miaka ya nyuma ipatayo kama thelethini hivi nilikuwa mtu mzima, lakini ambaye ni mfugaji na mchungaji mzuri wa mifugo. Kwa wakati ule niliona kazi pekee duniani ni ufugaji hasa wa mbuzi na niliona mbuzi kama mali pekee mtu anayopaswa kuwa nayo, akiwa hana mbuzi niliona ni maskini ambaye hajui miradi ya maana hapa duniani.
Mbali na ufugaji wa mbuzi, pia nilikuwa mkulima mzuri wa mazao ya chakula kama mahindi, maharage, njegere na viazi – shamba lilikuwa kama sehemu ya kazi yangu kuu ya ufugaji wa mbuzi. Niliendelea na kazi hiyo hadi pale Serikali ilipotuletea mabwana mifugo na mabwana shamba kwa ajili ya kuboresha miradi yetu, bwana mifugo alinishauri nipunguze mbuzi ninaowafuga isivyo kisasa na nifanye ufugaji wa kisasa.
Kwa hakika alinichanganya na kunifanya nijione mnyonge katika mradi wa mbuzi niliofikia kumiliki zaidi ya mbuzi mia mbili na ushei hivi. Wakati huo nchi yetu iliingia katika Vita ya Uganda ukatolewa wito wa kila Mtanzania kupigana kwa hali na mali. Leo hii natembea kifua mbele kwa kuwa nilifanya uzalendo wa kutoa mbuzi wengi na kuku kadhaa kwa ajili ya vijana wetu waliokuwa ‘mstari wa mbele’.
Nimeamua nikumbuke hili kwa kuwa kuna jambo linalonikera sana, ni jambo ambalo mpaka leo kwa elimu yangu ya darasa la nne haliniingii kichwani kiasi kwamba nafikiria kuingia katika ulingo wa siasa ili nipinge ukoloni mamboleo unaoendelea hapa nchi, kwa kuletewa bidhaa pasi na matakwa yetu zaidi ya kupangiwa na wakoloni wetu.
Miaka ile tukilima mazao yetu ilikuwa nadra sana kusikia mtu anaumwa ugonjwa wa ajabu kama kuhara, kipindupindu, malaria na hata presha zilizozagaa sasa hivi kwa watoto wetu. Utafiti mdogo niliofanya bila kuzingatia vigezo vya utafiti nimepata majibu ya kweli ambayo hayana hata punje ya shaka kwamba ni utafiti wa uwongo.
Miaka yetu ya ujana sikuwahi kusikia ugonjwa unaoitwa malaria, sababu kubwa ilikuwa ni matumizi ya dawa maarufu iliyoitwa DDT. Hii ni dawa tuliyokuwa tukinunua kwa mgawo unaoambatana na masharti ya kununua bahasha na glasi za maji katika duka la ushirika, hivyo kutokana na umuhimu wake DDT ilihifadhiwa chumbani tunakolala ilimradi iwe salama na wizi unaoweza kufanyika na mtu asiye na uwezo wa kununua bidhaa hiyo.
DDT ilikuwa ni sehemu ya maisha yetu na sikuwahi kusikia mtu amekufa kwa sababu ya kulala na DDT isipokuwa nilikuwa najua kuna watu wanakufa kwa kuamua kunywa dawa hiyo kutokana na wivu wa mapenzi, ugomvi wa mashamba, imani za kishirikina na kadhalika.
Wataalamu wa afya pamoja na mabwana shamba hawakuwahi kusema au kutamka kuwa DDT ni sumu kwa maisha ya binadamu. Tuliitumia DDT kuweka katika mashamba yetu ili mazao yasidhuriwe na wadudu na magonjwa ya mimea, tulitumia dawa hiyo kuweka katika vihenge vya mazao baada ya kuvuna ili mazao yetu yasibunguliwe na wadudu.
Ubora wa utunzaji mazao ulitegemea na utumiaji wa DDT katika uhifadhi, tulitumia nafaka hizo baada ya kuziosha na kusaga, sikuwahi katika maisha yangu kusikia mtu kadhurika na DDT hadi hapo ilipopigwa marufuku na serikali nyingine na si yetu.
Miaka michache baadaye tulianza kuugua malaria kila siku, ongezeko la mbu likawa kubwa kuliko nzi, mbu wakashika dola ya maradhi hadi leo, idadi ya wanaopoteza maisha ikawa kubwa na sasa imegeuka kuwa janga la kitaifa tunalohitaji msaada kutoka kwa watawala wanaotumia ushauri wao kufanya biashara ya dawa na vyandarua vya mbu.
Katika nchi zao matumizi ya DDT bado yanaheshimika na unaweza usionane na mbu kwa sababu utumiaji wa dawa hiyo unatokomeza mazalia ya mbu ambao ni chanzo kikubwa cha ugonjwa wa malaria, mimi ni shahidi kwamba sikupata kuugua malaria na wala kumuona mbu hadi pale tulipoambiwa tusitumie DDT.
Jambo hili linanikera sana ninapoona wasomi wanaoitwa mabingwa wa fani mbali hasa za afya na kilimo wanaposhindwa kufanya utafiti wa kujiridhisha na matumizi ya DDT. Nchi za wenzetu ni jambo muhimu kuua mazalia kwa kutumia dawa hiyo, sisi pamoja na kujua kuwa wao wanatumia na sisi wametukatalia tunashindwa kujiuliza maswali machache na kutoa ufumbuzi.
Sisi tumebakia kuwa soko la dawa, soko la utafiti baada ya kuumwa na mbu, soko la vyandarua vya mbu na ukifika mbali unajiona kama soko la kifo kwa uamuzi tuliofanyiwa na siyo tulioufanya. Wimbo wa ‘malaria haikubaliki’ tunaimbishwa huku wao wakijua kuwa wanafanya biashara yao kikamilifu.
Sitaki niwalaumu waliopitisha ulaji huu, lakini nataka niwalaumu wanaoendeleza ulaji huu, kwa ufupi hili ni jipu kubwa lililoiva linapaswa kutumbuliwa, naamini Waziri wa Afya na Naibu Mawaziri wa Afya watatumbua jipu hili mapema iwezekanavyo, vinginevyo watakuwa mawaziri wa wagonjwa wa malaria, ‘malaria inakubalika sana’.
Wasaalamu,
Mzee Zuzu
Kipatimo.