Na Tatu Saad, Jamhuri
Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania ambao ni washiriki pekee wa kombe la shirikisho barani Afrika Yanga Sc, wamewaburuza Real Bamako ya Mali mabao 2-0, katika Dimba la Benjamin Mkapa.
Yanga wameendeleza ubabe katika dimba la nyumbani baada ya kumfunga TP Mazembe kutoka Congo mabao 3-1,Februari 19 mwaka huu,na kumfunga tena Real Bamako ya Mali 2-0 leo katika dimba la mkapa.
Huu ni mchezo wa marudiano baada ya kucheza mchezo wa awali katika ardhi ya Mali uwanja wa Stade Du 26 Mars na kutoka sare ya 1-1.
Katika mchezo huo wa awali Yanga Sc ilikua ikiongoza hadi dakika za mwisho mshambuliaji wa Real Bamako, Emile Kone aliposawazisha na kusababisha mechi kuisha kwa sare ya 1-1.
Yanga kwa sasa inashika nafasi ya pili katika Kundi D wanaloshiriki ikiwa na alama 7, wakiongozwa na US Monastiri ya Tunisia yenye alama 10, huku Tp Mazembe akishika nafasi ya Tatu na Bamako nafasi ya mwisho.
Hata hivyo wachezaji wa Yanga wametimiza Ahadi yao waliyoiweka jana katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuwa watafanya vizuri katika mchezo wa leo kama njia ya kumfariji mchezaji mwenzao Salum Aboubakar (Sure Boy) baada ya kufiwa na mtoto wake asubuhi ya jana.