Tatizo la kweli la dunia ya leo si umasikini; maana tunao ujuzi na amali zinazotuwezesha kuufuta umasikini. Tatizo lenyewe hasa ni mgawanyiko wa binadamu katika tabaka mbili – tabaka ya matajiri, na tabaka ya masikini.  Jambo hilo ndilo linaloleta matatizo, vita, na chuki kati ya watu.

Tunaweza kuziona tabaka hizi katika mafungu mawili. Kwanza, katika nchi moja watakuwako watu wachache wenye mali  nyingi,  na mali yao huwapa sauti kubwa; hali wananchi walio wengi sana wanateseka na umasikini na dhiki za aina mbalimbali. Tabaka hizo zinaonekana hata katika nchi tajiri kama Amerika. Na katika nchi nyingine kama India, Ureno au Brasil, tofauti iliyoko baina ya tajiri na watu wachache wenye nafasi na ufukara wa wananchi walio wengi ni fedheha tupu!

Na pili, tukitazama dunia kama mkusanyiko wa nchi nyingi, tunaona tabaka za aina hiyo hiyo. Upande mmoja kuna nchi chache, tajiri, zinazotawala dunia katika mambo ya uchumi; na kwa sababu ya utajiri wao zinatawala mambo ya siasa pia. Upande mwingine kuna nchi ndogo ndogo zilizo masikini ambazo inaonekana mwisho wao utakuwa kukandamizwa daima.

Jambo muhimu katika mgawanyiko huu baina ya matajiri na masikini siyo tu kwamba mtu mmoja ana chakula kingi kuliko anachoweza kukila,  hali wengine wengi hawana chakula; au ana nguo nyingi kuliko anazoweza kuzivaa, hali wengine wanakwenda uchi;  au ana nyumba nyingi kuliko anazozihitaji kwa kuishi, hali wengine wengi hawana hata kibanda cha kujisitiri. Wala jambo muhimu katika mgawanyiko huu baina ya nchi tajiri na masikini siyo tu kwamba nchi moja ina utajiri wa kuweza kuwapatia raia wake wote hali njema ya maisha, hali nyingine haiwezi kuwapatia raia wake hata huduma za lazima. 

Tatizo la kweli, na lililo zito, hutokea kwa sababu yule aliye tajiri anayamiliki maisha ya wale walio masikini, na nchi iliyo tajiri ina uwezo wa kutawala siasa za nchi zilizo masikini. Na lililo zito ni kwamba utaratibu wetu wa maisha na uchumi, katika nchi moja na baina ya nchi moja na nyingine,  unasaidia na kudumisha migawanyiko hii, hata kuwafanya wale walio tajiri wazidishe utajiri na nguvu zao daima, hali walio masikini wazidi kuwa masikini na kupungukiwa uwezo wa kuyatawala maisha yao wenyewe.

Pamoja na maneno yote yanayosemwa kuhusu usawa wa binadamu, na juhudi za kutafuta maendeleo na kuuondosha umasikini, bado hali hiyo inaendelea. Bado matajiri katika nchi, na nchi tajiri katika dunia, zinaendelea kuwa tajiri kwa haraka zaidi kuliko zile masikini zinavyoweza kupunguza umasikini wao. Wakati mwingine hali hii hutokea kwa kupangwa makusudi na matajiri, ambao hutumia utajiri na nguvu zao kwa shabaha hiyo. 

Lakini mara nyingi, pangine mara nyingi zaidi, hali hiyo huwa ni matokeo ya taratibu zinazoonekana kuwa za kawaida, za maisha na za uchumi, ambazo watu wamejiundia wenyewe. Kama vile ambavyo maji hutoka sehemu kame kabisa za nchi hutiririka kuelekeza baharini kwenye maji tele, vivyo hivyo utajiri nao hutiririka kutoka nchi masikini kabisa na kwa watu masikini kabisa, ukaingia mikononi mwa zile nchi, na wale watu, ambao ni matajiri tayari.

Mtu anayemudu kununua mkate mmoja tu kwa siku huwa anaiongeza faida ya mwoka-mikate, ingawa tajiri yule tayari anazo fedha nyingi kuliko anavyojua kuzitumia. Na nchi masikini, inayouza bidhaa zake kwenye soko la dunia ili inunue mashine za kuleta maendeleo, hugundua kwamba bei inazopata, na bei ambazo hubidi kuzilipa, zote zinakadiriwa katika masoko ya mabepari, ambako nchi masikini huwa kama mbilikimo anayefurukuta mikononi mwa pandikizi la jambazi!

Kwani aliye nacho atapewa na kuongezewa tele; lakini asiye nacho, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.

Kwa haki kabisa, watu wengi wanazidi kuuchukia mgawanyiko huu wa binadamu baina ya matajiri wachache sana na masikini walio wengi sana, katika nchi moja na baina ya nchi moja na nyingine. Nchi masikini na watu masikini wa dunia nzima sasa wameanza kuushambulia mgawanyiko huu. Na kama hawatafaulu kupata mabadiliko yatakayoleta usawa zaidi, basi mapambano hayo yatalipuka kuwa vita. Hatimaye dhuluma na amani ni viwili ambavyo haviwezi kukaa nyumba moja. Amani katika dunia hii inayobadilika maana yake lazima iwe mabadiliko yanayoelekea kwenye haki, siyo kudumisha tabaka zilizopo sasa.

Hii ndiyo sababu wakati mwingine maendeleo yakaitwa amani. Kwani maendeleo ya kweli ndiyo msingi wa amani. Na hii ndiyo sababu mazungumzo yenu juu ya mataifa kushiriki katika maendeleo ya watu ni muhimu na ya lazima.

 

Binadamu ndiyo Shabaha

Shabaha ya maendeleo ni binadamu. Ni kuleta hali inayomwezesha mwanadamu kukamilika, katika roho, akiwa peke yake au katika jamii. Jambo hili ni rahisi kwa Wakristo kulielewa, kwa sababu Ukristo unataka kila mtu ajitahidi kuungana na Mungu kupitia kwa Kristo. Lakini ingawa Kanisa, kwa sababu ya kumthamini sana binadamu, hujaribu kuepuka lile kosa la kudhani kuwa maendeleo ni viwanda vipya, au kuongezeka kwa mazao, au hesabu nzuri za pato la taifa, lakini inavyotokea mara nyingi ni kwamba Kanisa nalo hufanya kosa jingine kinyume cha hilo.

Maana wale wanaoliwakilisha Kanisa, na mashirika ya Kanisa, mara nyingi huendesha shughuli zao kama kwamba maendeleo ya binadamu ni jambo la mtu binafsi, lisilokuwa na uhusiano wowote na jamii ya watu na utaratibu wa uchumi wa mahali mtu yule anapoishi na kujipatia riziki yake. Makanisa yanahubiri utii; na mara nyingi inaonekana yanakubali kwamba utaratibu wa leo wa maisha ya watu katika uchumi wa siasa ni kudura ya Mungu – haubadiliki. Hujaribu kujituliza na hali mbaya zisizovumilika, kwa vitendo vya zaka na upendo, ambapo binadamu mpokeaji wa upendo huo na zaka hizo, hubaki ni kitu tu. Lakini wale wanaoteseka kwa maonevu na umasikini wanapoanza kuchachamaa, kama binadamu kujaribu kuzibadilisha hali hizo, wale wanaoliwakilisha Kanisa hujitenga kando.

Nia yangu leo ni kupendekeza kwenu kwamba Kanisa likubali kuwa maendeleo ya watu maana yake ni maasi. Katika historia, watu hufikia hatua ya kuyakataa mambo yanayowabana katika uhuru wao kama binadamu. Maoni yangu ni kwamba ikiwa hatutashiriki kwa vitendo katika mapambano ya kuondoa utaratibu wa maisha na wa uchumi unaowadidimiza watu kwenye umasikini, uonevu na unyonge, basi Kanisa litakuwa halina uhusiano na maisha ya binadamu, na dini ya Kikristo itakuwa kama ni mkusanyiko wa imani za ushirikina zinazokubaliwa na wenye hofu. 

Ikiwa Kanisa, wafuasi wake na mashirika yake hayatawaangazia binadamu upendo wa Mungu kwa kujiunga nao na kuongoza mapambano ya kuzipinga hali zao za sasa, basi Kanisa litaambatanishwa na dhuluma na ujahili. Na ikiwa hivyo, Kanisa litakufa, na kwa maoni ya kibinadamu, litastahili kufa, maana litakuwa halina maana inayoeleweka kwa mtu wa kisasa.

Maana binadamu huishi na mwenziwe. Maisha yake huwa na maana kwake binafsi na kwa wenziwe anapoishi katika jamii. Kwa hiyo, tunapozungumza juu ya maendeleo ya binadamu, lazima tuwe tunakusudia vile vile kutafuta maendeleo ya jamii inayomtumikia, inayoendeleza hali yake, na kuilinda heshima yake. Kwa hiyo maendeleo ya watu ni pamoja na maendeleo ya uchumi, maendeleo ya siasa, na maendeleo ya maisha kwa jumla. Na katika wakati huu wa historia ya binadamu, lazima maendeleo yawe na maana ya maasi matakatifu, kwa shabaha ya kuleta mabadiliko. 

Mana hii hali ya watu lazima ikataliwe na wote wanaokubali kwamba binadamu ni kiumbe cha pekee cha Mungu aliye hai. Tunasema kwamba binadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu. Mimi nakataa kumfikiria Mungu aliye fukara, mjinga, mshirikina, mwoga, dhalili, ambao ndiyo hali ya walio wengi kati ya wale walioumbwa kwa mfano wake mwenyewe. Binadamu wenyewe ni waumbaji, hujitengenezea hali zao za maisha, lakini tulivyo hivi sasa tu viumbe, tena si viumbe wa Mungu, bali wa binadamu wenzetu.

Bila shaka Wakristo hawawezi kubishana juu ya jambo hili. Maana binadamu hawajapata kuwa kitu kimoja kama walivyo sasa, wala hawajapata kugawanyika kama walivyogawanyika sasa. Hawajapata kuwa na uwezo mkubwa wa kutenda mema kama walio nao sasa, na wakaumia kwa dhuluma ya wazi wazi kama dhuluma ya sasa. Uwezo wa binadamu haujapata kuwa wazi kama ulivyo hivi sasa, na wala haujapata kupuuzwa wazi wazi na makusudi kama unavyopuuzwa hivi sasa.

Kwa lugha ya utaalamu, dunia sasa ni kitu kimoja. Binadamu ameitizama dunia kutoka mwezini akaona jinsi ilivyo kitu kimoja. Ninaweza kusafiri  kutoka Tanzania hadi New York kwa muda wa saa chache tu kwa ndege za jeti. Mawimbi ya redio yanatuwezesha kuzungumza na wenzetu, ama kwa wema au kwa ubaya, mnamo kipindi cha sekunde baina ya mtu kusema na kusikiwa. Bidhaa hutengenezwa kwa vifaa vya ustadi kutoka sehemu zote za dunia, na halafu huuzwa maelfu ya maili kutoka mahali zinakotengenezwa.

 

>>ITAENDELEA