maguMoja ya mambo yanayowashangaza kama siyo kuwatatanisha Watanzania wengi tangu utawala huu wa awamu ya tano uingie madarakani, ni hii kasi ya utendaji kazi inayooneshwa na viongozi mbalimbali ndani ya Serikali kuanzia ngazi ya Taifa mpaka ngazi ya kijiji.

Kinachowashangaza zaidi wananchi hao siyo utendaji kazi wa kasi wa sasa wa viongozi hao, bali ni kipi kilicho nyuma ya viongozi hao ambao baadhi yao walikuwapo katika awamu iliyopita na wala hawakuonekana kuwajibika  zaidi katika kuwahudumia wananchi kama wanavyoshuhudiwa sasa hivi.

Maana baadhi ya mambo ambayo viongozi hao wanayakemea kwa sasa, ikiwamo pamoja na kuyavalia njuga kama ubadhirifu wa fedha, rushwa, kutowajibika ipasavyo kwa baadhi ya watumishi si mambo mapya, bali yalikuwapo huko nyuma na wananchi waliyapigia kelele, lakini viongozi hao hata hawakushtuka na kuacha vilio vya wananachi viende na maji.

Watanzania wengi wakiwamo wanasiasa walilalamika huko nyuma kuwa Taifa hili lina mchwa wachache wanaolitafuna, wengine wakaja na orodha ya mafisadi, zikalalamikiwa huduma mbovu za kijamii kuanzia afya, elimu, barabara, lakini viongozi hao walipuuza na kubeza vilio vya Watanzania wenzao.

Jambo la kutia simanzi, wale wananchi na baadhi ya wanasiasa, wakiwamo waandishi wa habari waliojitokeza kupinga vikali vitendo vya kifisadi ndiyo walioonekana wabaya, wana wivu,  hawalipendi Taifa lao, mwisho wa siku baadhi yao wakafanyiwa unyama usiomithilika, aliyewafanyia tuliambiwa anachunguzwa ila hadi leo hatujaambiwa ni nani.

Baadhi ya waandishi nguli mfano wa Padri Privatus Karugendo katika makala yake aliyoipa kichwa cha habari ‘Tishio sio waandishi, tishio ni mafisadi’ katika gazeti la Raia Mwema la Julai 30-Agosti 5, 2008 (toleo namba 040) akaonya kuwa kuwaadhibu wanaofichua na kukemea vitendo vya kifisadi hakutaliokoa Taifa bali dawa mujarabu ilikuwa ni kuwashughulikia mafisadi.

Walioshauriwa wakatenda kinyume chake, tukashindwa vita, ambayo leo hii chini ya Rais Magufuli tumeianza tena, majipu yanayotumbuliwa leo hii ni balaa, hali hii yote inatokana na utawala uliopita kushindwa kuwalenga maadui sahihi badala yake ikawaadhibu majemedari wake muhimu katika mapambano.

Turejee kwenye maswali ya wananchi, kama nilivyobainisha hapo awali katika makala hii, kwa sasa wanajiuliza, je, kiliwasibu nini viongozi hao walioko kwenye awamu hii mpaka wakashindwa kutimiza majukumu yao, je, huko nyuma wakati wanakabidhiwa majukumu yao ya kazi hawakupewa maelekezo  (job description) ya nini wanatakiwa kufanya?

Wananchi katika kujijibu maswali yao juu ya viongozi hao wanaonekana sasa hivi kuwajibika ipasavyo, wanakuja na majibu ya aina mbili, mosi, ni kuwa viongozi hao wanafanya yote hayo kwa kumuogopa Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Magufuli, ambaye ameonesha kuwa hataki mchezo na viongozi wazembe ikizingatiwa kuwa kaulimbiu yake ni ‘Hapa kazi tu.’

Na hata kabla ya kuchaguliwa na baada ya kuchaguliwa kuwa Rais, Dk.  Magufuli amekuwa akiwaonya na kuahidi kutowavumilia wafanyakazi wazembe, walarushwa, wasiojali maslahi ya wananchi, akisema yeye kazi yake ni kuwatumbua tu, na tunaona jinsi baadhi ya wafanyakazi wanavyotumbuliwa kwa sasa.

Jibu la pili ni lile linalosema kuwa viongozi hao mfano wa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wanafanya hivyo ili kuzihami tu nafasi zao ikizingatiwa kuwa utawala mpya unapoingia madarakani huja na watendaji wapya kabisa ambao wataendana na Serikali hiyo mpya.

Yumkini katika majibu yote hayo mawili kuna ukweli, ila tunaitazama hali hiyo katika dhana nzima ya mfumo wa kiutawala, na nani anausimamia mfumo huo, kwani uzoefu unaonesha kuwa siku zote yule aliyeko juu kabisa katika ngazi ya utawala ndiye huwa anatoa taswira gani ya mambo yanavyotakiwa kwenda, mfano akiwa muadilifu, hata wengi walio chini yake watakuwa waadilifu ila akiwa mbadhirifu tambua na  wengi walioko  chini yake watakuwa  wabadhirifu tu.

Na zaidi ya hayo, kiongozi huyo asiyekuwa muadilifu siku zote huwa hapendi kusikia utawala wake ukiambiwa unanuka ufisadi, rushwa, haujali wananchi wake na wale wanaoonekana kuuanika hadharani utawala huo, basi huwa wanaonekana wanoko na kama upo kwenye mfumo huo wa utawala utanyang’anywa nafasi yako.

Haya mambo yameshuhudiwa sana katika utawala wa awamu iliyopita, utawala ambao kwa kiasi kikubwa uliweka kando malalamiko yaliyokuwa yakitolewa kuhusu kukithiri kwa vitendo vya kifisadi, nakisi ya uadilifu, uzembe kazini, na wale waliojaribu kuchukua hatua waliona athari zake.

Kwani baadhi ya watendaji waliojipambanua kutetea maslahi ya wananchi waliondoshwa kimizengwe madarakani, huku wale walioonekana kukaa kimya na kuacha mambo yajiendee tu ndiyo walioonekana ‘mashujaa’, wakapendwa, na wengine wakapandishwa vyeo.

Hivyo katika hali kama hiyo ni vigumu sana kwa wale viongozi walioko katika ngazi za chini kuchukua hatua kali dhidi ya wazembe, utachukuaje hatua hiyo wakati mkuu wako hapendi kusikia na wala hata yeye akiambiwa anapuuza tu?

Mfano, tumesoma  sana habari za ufisadi mkubwa katika Wizara ya Maliasili na Utalii, waandishi wamepiga kelele sana lakini mwisho wa siku hakuna hatua zilizochukuliwa na utawala ukaondoka zake.Tunasubiri kwa hamu jipu hili.

Wamepewa meno?

Tuiangalie Serikali ya sasa ya Rais Magufuli hususani yeye mwenyewe Rais, ni mtu ambaye  amejipambanua kuwa ana sifa ya uadilifu, uchapaji kazi na kujali maslahi ya wananchi wake, na kuthibitisha azma yake hiyo kivitendo, Rais Magufuli amekuwa akichukuwa hatua  mbali mbali ikiwamo kuwatumbua watendaji wazembe kazini na kuwataka wasaidizi wake wengine wafanye hivyo, na wanafanya kweli.

Katika hali kama hii ambapo mkuu wako mwenyewe ni mpiga kazi, hataki masihara kazini, hata wewe msaidizi wake lazima ufanye kazi yako kama inavyotakiwa kwani yeye ndiye anayekuwa mwongozo wako, na zaidi ya hapo unakuwa huna hofu ya kushughulikiwa.

Hivyo kwa upande wangu kutokana na utendaji kazi wa Rais mwenyewe Magufuli, sishangai kuwaona baadhi ya viongozi wetu wa sasa wakicharuka, kwenda huku na kule kutatua matatizo ya wananchi na wengine hata kufikia hatua ya kufungiana mageti ya milango katika maeneo ya kazi ili kuwadhibiti wachelewaji.

Je, viongozi hao walikuwa sahihi?

Miongoni mwa sifa bora za kiongozi yeyote yule  muadilifu ni pamoja na kujitenga na kundi (utawala) lolote lile lisilojali maslahi ya wananchi, linalowabeza  wale wanaopinga kwa haki vitendo vya kifisadi, kwani kutokufanya hivyo naye anakuwa ameshiriki katika kuchangia matatizo katika nyanja mbali mbali ikiwamo huduma mbovu za kijamii, kiuchumi na kadhalika.

Naomba nitoe mfano wa mtu kama  huyu muadilifu hapa hapa nchini kwetu, naye ni komredi, mjamaa (socialist), marehemu Henry Mapolu, ambaye yeye alisikia kwenye redio kwamba ameteuliwa na Rais kuwa mkuu wa wilaya, lakini hakukubali uteuzi huo kwa madai kuwa hakuwa ameshauriwa mapema juu ya kazi hiyo, kifupi hakutaka kuwa sehemu ya mfumo ambao binafsi yake aliuona hauko sawa katika kuendesha nchi.

Watu aina ya Mapolu kuwapata kwa sasa ni nadra, lakini hata hivyo  pamoja na kwamba baadhi ya viongozi hao waliokuwapo katika awamu iliyopita na awamu hii wapo walionesha udhaifu kiutendaji, kwa sasa itabidi tuwape muda ili watende vema na kutuletea maendeleo katika Taifa letu, hawana kisingizio cha kubanwa kwa sasa.

 

Kila la heri!

 

Simu 0658010594