LukuviHatimaye suala la ubomoaji wa makazi ya wananchi katika bonde la Msimbazi na Mkwajuni jijini Dar es Salaam limechukua sura mpya. Tunaambiwa katika semina elekezi kwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyofanyika mjini Dodoma, wengi wao wamemgeukia Rais John Magufuli na kumtaka suala hili aliangalie upya, vinginevyo ‘litakigharimu chama tawala’

Rais Magufuli alipiga marufuku semina elekezi kwa mawaziri na vigogo wa serikali zilizokuwa zikifanyika katika hoteli za kitalii kwa gharama kubwa. Aliwaambia wataelekezana wakiwa kazini. Lakini kwa wabunge wa CCM, wameona ni muhimu sana kuwa na semina hiyo.

Wabunge hao wamekuwa na semina elekezi ya siku mbili mjini Dodoma, kwa lengo la kupeana mikakati ya kupambana na Kambi ya Upinzani ambayo imefanikiwa kuongeza idadi ya wabunge katika Bunge la 11 lililoanza rasmi wiki iliyopita.  Tunaambiwa wabunge hao walilalamikia suala la bomoabomoa kwamba linakichafua chama chao mbele ya wananchi.

Kuna waliojenga katika mabonde ambako wanahatarisha maisha yao na wakati wa mvua kubwa kila mwaka Serikali inalazimika kuwaokoa. Lakini pia kuna waliojenga mita 60 kutoka barabara au mito. Wengine wamevamia maeneo hya wazi. Hawa wamekiuka sheria na kanuni za ujenzi kwa hiyo nao pia wanabomolewa.

Kazi hii ya bomoabomoa ilianza mwaka Novemba, mwaka jana tulipotangaziwa kuwa Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaanza ubomoaji wa nyumba zilizojengwa bila kufuata taratibu za ujenzi, yaani “bila kibali cha ujenzi, bila kufuata michoro ya mipango miji na bila kufuata matumizi ya ardhi ambayo ni maeneo ya wazi.”  Maeneo husika hasa yako Mbezi, Tegeta, Bunju, Mwenge, Biafra na kadhalika.

Kamishna wa Ardhi alituambia kuwa ubomoaji unafanywa baada ya kubaini kuwa maeneo yaliyotengwa mijini kwa matumizi ya umma ikiwa ni pamoja na maeneo ya wazi, njia za miundombinu na huduma nyinginezo za umma yamekuwa yakitumiwa vibaya au kuvamiwa na wawekezaji binafsi, hivyo kukosesha umma manufaa yaliyokusudiwa.

 Baada ya tangazo hilo tukawa tunaona ‘laivu’ karibu kila siku tingatinga likibomoa nyumba zilizojengwa katika maeneo ya wazi jijini Dar es Salaam. Kazi hii imekuwa ikiendeshwa chini ya usimamizi wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Tukaona nyumba zikibomolewa kwa waishio mabondeni, hifadhi za misitu ya mikoko na maeneo oevu, na ya wazi

 Tukaambiwa ubomoaji ulisitishwa ili wananchi washerehekee sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya. Baada ya hapo tingatinga likaendelea na kazi yake. Kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu” ikapewa tafsiri ya kipekee. Ubomoaji wa vibanda ukapewa tafsiri ya upasuaji majipu.

Baada ya muda mfupi tukaona sheria ikichukua mkondo wake. Tingatinga likaoneshwa kadi nyekudu pale Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, ilipoitaka Serikali kuacha ubomoaji wa nyumba 681 zilizopo katika Manispaa ya Kinondoni.

Nje ya Mahakama, wahusika walionekana wakishangilia na kushereheka, kiasi kwamba ikabidi askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) kuingilia kati. Baada ya tafakuri ikaeleweka kuwa Jaji alikuwa amezuia “kwa muda” tu hadi shauri lao litakapofunguliwa. Kumbe tingatinga linasubiri kuingia kazini wakati wowote. Wananchi ni vizuri wakaelewa kuwa sheria na haki ni vitu viwili tofauti.

Hata hivyo, hongera kwa Mbunge wa Kinondoni kwa kuwaongoza wapigakura wake wachukue mkondo wa sheria. Sasa na waathirika wengine nao wamejitokeza na kwenda mahakamani kuomba zuio.

Nimekuwa nikifuatilia mijadala katika mtandao wa kijamii, wengine wakiunga mkono bomoabomoa na wengine wakilaani. Kuna wanaosema hatuwezi kuhalalisha vitendo vya kujenga kiholela mabondeni, kwani wakazi wa mabondeni kwa uamuzi wao wenyewe wamejenga wakijua fika kuwa hawaruhusiwi.

Wanasema Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikiwasihi wakazi wa maeneo yaliyotajwa wahame mabondeni, na hata iliwapa viwanja Mabwepande ambako walitakiwa kwenda kujenga na kuishi. Badala yake waliuza sehemu walizopewa na kurudi kuendeleza mabondeni kinyume cha sheria za mazingira na mipangomiji.

Hoja hii inajibiwa na wale wanaosema si wote kati yao waliopewa maeneo mbadala na wakarudi. Hata hivyo, mamlaka husika iliwaona wakipokea fidia na ikawaona wakirudi mabondeni kwanini ikawaacha tu? Kwanini isichukue hatua mbadala ya kuwazuia na wala si njia hii inayotumika sasa?

 Wengine wakasema katika malumbano haya ni vizuri tukaangalia sheria inasemaje na kisha tukaitekeleza kama ilivyo. “Iliyobaki ni mitaji ya kisiasa ya wanasiasa”. 

Wanaopinga msimamo huu wanasema kama dawa ya nyumba zilizojengwa kinyume cha sheria ni kubomolewa tu, kwa nini basi na wale wahalifu wanaohukumiwa kunyongwa wasinyongwe tu kwa sababu Mahakama imekwishatoa hukumu?

Kwa upande wa pilim sheria pia imevunjwa na wale waliotoa kibali. Hivyo ni vizuri kuwaadhibu hao maofisa kwanza badala ya wenye nyumba. Kwa njia hii tutakuwa tumezuia siku zijazo kutolewa kwa vibali feki.

Alhasili, suala hili ni nyeti mno, zito na linagusa maisha ya wananchi wengi, wakiwamo watoto na vikongwe. Hivyo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha inawalinda watu wake. Kwa sababu ni jambo la hatari mno kuwavunjia watu maskani yao, hasa pale ambako hawajapatiwa makazi mbadala.

Serikali inadai kuwa ina nia njema ya kuhakikisha miji yetu inapangwa kwa kuzuia ujenzi holela. Lakini wakati huo huo imeachia makazi haya yawepo kwa muda mrefu. Si tu imeacha, bali kwa kupitia maofisa wake, imetoa vibali feki kwa njia ya rushwa. Sasa katika mazingira haya ya uvunjifu wa sheria kosa ni la nani?

Wakati tunazungumzia uvunjifu wa sheria, ni vizuri tukaliangalia suala hili kwa mapana, ili tusije tukaingia katika mtego wa kuwalaumu wale waliojenga mabondeni, na kuwaacha mapapa na nyangumi tulionao katika jamii yetu.

Kwani mara nyingi tunapozungumzia bomoaomoa katika mabonde ya Msimbazi au Mkwajuni huwa tunasahau kabisa kuwa katika Jiji la Dar es Salaam kuna uvunjifu mkubwa wa sheria unaofanywa na wajenzi/wawekezaji wakubwa. Nani asiyejua kuwa kwa miaka mingi sasa wawekezaji hawa wamekuwa wakijenga ghorofa kila mmoja kivyake, bila kuzingatia sheria, utaratibu na kanuni?

Haya yamesemwa na hata ripoti kuandikwa kisha kutupwa kapuni. Miaka kadha iliyopita nimeshuhudia wataalamu/wahandisi wakipita mitaa ya Kariakoo na kuchunguza haya maghorofa yanayochipuka kama uyoga. Wakagundua kuwa idadi kubwa ya ghorofa hizo zina uwezekano wa kuporomoka na kuua watu. Ndiyo maana tunashuhudia mara kwa mara ghorofa hizi zikiporomoka au zikipata nyufa.

Bw. Sudhir Chavda ni mmoja wa wahandisi ujenzi waliobobea katika nchi hii. Amekuwa katika fani hii tangu miaka ya 1970, hivyo anaelewa anachosema.

Yeye na wataalamu wenzake wameunda asasi ya kiraia (Front Against Corrupt Elements in Tanzania – Facit) ili kupambana na rushwa na ufisadi katika sekta ya ujenzi. Hivi karibuni aliwaambia waandishi kuwa maeneo ya Kariakoo yanaongoza katika uhalifu wa mpango wa jiji (city master plan) ambao umevurugwa. 

Anasema wawekezaji wamekuwa wakivamia maeneo yaliyo wazi huku wakijijengea bila ya kufuata sheria, kanuni na taratibu za mipango miji.

Mhandisi Chavda anakumbuka wajenzi wa miaka ya 1960 na 1970 ambao hawakuwa wanatawaliwa na uchu wa kujitajirisha haraka. Leo hii wawekezaji wanataka kurudisha mitaji yao katika muda mfupi, hata miaka miwili. Wawekezaji kama hao kwa kawaida huwa wanawahonga maofisa wa Serikali Kuu na Jiji, anasikitika Chavda

“Inasikitisha kuona wajenzi/wawekezaji wanaohalifu sheria na mipango miji kwa njia hii ndiyo wanaochangia siyo tu katika kuvuruga mpango wa jiji, bali pia mmomonyoko wa maadili na weledi miongoni mwa maofisa na wataalamu wetu,” anaongeza Chavda. Lakini wangapi wanajali? Badala yake tunachangamkia bomoabomoa ya mabondeni.

Hali hii sasa inaonekana kote nchini. Kwa mfano, kuna ghorofa tatu zilizojengwa Nyasaka, Manispaa ya Ilemela (Mwanza) ambazo tunaambiwa ujenzi wake umekiuka taratibu za ujenzi. Miongoni mwa mamlaka zilizofuatilia na kuthibitisha kwamba ujenzi huo ulikiuka taratibu zinazotakiwa, ni Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB).

Hata hivyo, tunaambiwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela anaonyesha dalili za kumkingia kifua mmiliki ambaye alitakiwa kuwasilisha vibali vya ujenzi huo kufikia Novemba 30, mwaka jana. Wakati wataalamu wamethibitisha kuwa ujenzi wa ghorofa hizo umekiuka taratibu zinazotakiwa, Mkurugenzi anasema ataendelea “kumsubiri” mmiliki amwonyeshe vibali vya ujenzi huo.

Na wakati Mkurugenzi “anasubiri”, msimamizi wa ujenzi wa ghorofa hizo tunaambiwa anatamba mitaani kuwa ametenga fungu nono la “kuwaweka sawa” viongozi husika ili wamwandalie vibali feki vitakavyomnasua katika kashfa hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela alishangazwa jinsi wataalamu walivyoifumbia macho kashfa hii. Ndipo akasema: “Haiwezekani ujenzi wa ghorofa hili ukafika hatua hii bila ninyi kujua… yaani hata idara yenu haina ukaguzi?  Mmeugeuza mradi wenu na kuidhalilisha Serikali?”

Kisha Mkuu huyo wa Wilaya akawaagiza wahandishi wa Manispaa kumpelekea ofisini kwake taarifa kamili kuhusu hatua walizochukua dhidi ya mmiliki wa ujenzi huo.

Mkaguzi wa Majengo wa Manispaa akajitetea mbele ya mkuu huyo wa wilaya kwamba wamekwishamwandikia mmiliki wa majengo hayo barua ya kumtaka apeleke vielelezo vya ujenzi huo kwa wiki kadhaa sasa bila mafanikio.

“Tumemtumia (mmiliki) barua alete vielelezo ila bado hajaleta majibu. Nilishapita kukagua majengo haya mara nyingi, lakini nikaambiwa mhandisi wa ujenzi ambaye ni bosi wangu ndiye amekuwa akipita kukagua majengo haya, hivyo nikaona haina haja mimi kumwingilia. Unajua ukishaambiwa anayefuatilia ni mkubwa wako utahoji nini? Mimi siwezi kumnyoshea kidole bosi wangu.”

Wakati sakata hili linaendelea, wakazi wa Nyasaka wamesema kwa masikitiko kuwa msimamizi wa ujenzi wa ghorofa hizo amekuwa akitamba mitaani kwamba hakuna mtu wala mamlaka inayoweza kumchukulia hatua za kisheria kwani “amekwishaiweka serikali mfukoni mwake”.

Msimamizi alipoulizwa na waandishi kwa simu kuhusu suala hilo alikata na kuzima simu. Haya yanaendelea nchini kote na si Ilemela pekee. Wale wananchi wa mabondeni hawana uwezo (wala nia) ya “kuiweka serikali mfukoni”, bali wao ndiyo wamewekwa mfukoni. Wenye nia na uwezo wa kufanya hayo wanafanya na wanatamba.

Uozo huu wa kuiweka Serikali mfukoni ulipigwa vita na Mwalimu Julius Nyerere. Leo tumeingia Awamu ya Tano ya upasuaji wa majipu, lakini wawekezaji wanaojenga ghorofa wanathubutu kutumia lugha ile ile.