Wakati zamani dhamira ya wanasiasa wengi ilijikita katika kutafuta uongozi wa kutumikia umma, siku hizi mambo ni tofauti. Wengi wao wanasaka uongozi kwa lengo la kujipatia ulaji! Nani anapinga? Fuatilia kwa makini viongozi wa kisiasa nchini hususan kuanzia ngazi ya kata, jimbo hadi Taifa utaona wengi wao wanatumia nyadhifa zao kujitafutia maslahi binafsi ya kujineemesha na familia zao.

Mifano ni mingi lakini nitatoa michache itakayotosha kuthibitisha ninachokisema. Chukulia kwa mfano madiwani. Wengi wao hawajizatiti kushughulikia matatizo yanayowanyima wananchi maendeleo. Badala ya kuelekeza nguvu katika kubuni na kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya wananchi, baadhi ya madiwani wamejikita katika kupigania nyongeza za posho za vikao na malipo yao ya kila mwezi.

 

Madiwani wengine wanakazania kuanzisha kampuni za kibiashara kwa kutumia majina ya ndugu, jamaa na rafiki na kuziombea zabuni mbalimbali katika halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji. Tatizo ni kubwa zaidi kwa upande wa wabunge. Wengi wa wanasiasa hawa wamegeuza nyadhifa zao hizo kuwa silaha ya kujifutia umaskini na kujichumia utajiri.


Kitu cha kwanza kufanya mara baada ya kuchaguliwa, wabunge wengi huhamia jijini Dar es Salaam. Wanaishi huko na familia zao wakisingizia kutafuta misaada ya maendeleo ya wananchi. Leo ukipewa mtihani wa kutafuta mbunge mwenye mtoto anayesoma katika shule za kawaida lazima utashindwa kwa sababu hakuna mbunge wa aina hiyo hapa Tanzania.


Wakati wa kampeni za kuomba uongozi, wanasiasa wengi wamekuwa wakijivisha ngozi za unyenyekevu na ukarimu huku wakiwa wamejaa maneno matamu mithili ya asali. Lakini baada ya kuchaguliwa wamerejea katika asili yao ya ukaidi na ubadhirifu wa mali za umma. Viongozi wengine wa kisiasa, hasa wabunge wanajidhihirisha waziwazi kuwa hawako kwa ajili ya kuwatumikia wananchi; wengi wamejenga kasumba ya kutopokea simu wanazopigiwa na wananchi wa kawaida kutoka majimboni mwao.

 

Wabunge hawa hawakumbuki kuwa hao wananchi wa kawaida, ndiyo madaraja (wapigakura) yaliyowavusha kutoka kwenye umaskini kwenda kwenye neema ya kusomesha watoto wao katika shule za kimataifa. Neema nyingine ya wabunge ni ile ya kugharimiwa na Serikali matibabu nje ya nchi, huku baadhi ya wananchi wa kawaida wakiteswa na maradhi mbalimbali na wengine wakipoteza maisha baada ya kukosa uwezo wa kujigharimia matibabu!


Kikubwa zaidi, hali ya mshahara, posho za vikao na marupurupu ya wabunge ni nzuri mno ikilinganishwa na wataalamu mbalimbali kama vile madaktari, walimu na maofisa wa jeshi nchini. Pengine neema hizo lukuki ndizo chanzo cha watu wengi (hata wasio na sifa za uongozi), kukimbilia siasa kama njia ya kuwafikisha kwenye uongozi ili kufanikisha lengo lao kujiweka katika mtandao wa ulaji.


Ndiyo maana suala la kuboresha maisha ya kila Mtanzania limeendelea kuwa wimbo endelevu kwa vile dhamira halisi ya viongozi wengi wa kisiasa, hasa madiwani, wabunge na mawaziri ni zaidi ya uongozi wa kuwatumikia wananchi. Ahadi nyingi za kimaendeleo zinazotolewa na viongozi wa kisiasa hazitekelezwi kwa sababu wengi wapo kwa ajili ya ‘kula’. Hawajihangaishi kushughulikia kero za wananchi waliowaweka madarakani.

 

Kwa bahati mbaya sana, wananchi wengi wameendelea kuwa wepesi mno wa kurubunika na maneno matamu ya wanasiasa wenye uchu wa madaraka na utajiri. Lakini pia wameendelea kuwa wagumu wa kuhoji utekelezaji wa maendeleo waliyoahidiwa. Ndiyo maana kwa kutambua udhaifu huo wa wananchi wengi, wanasiasa wamekuwa na uthubutu wa kuomba uongozi na kuahidi mambo makubwa huku wakijua wazi kuwa hawatayatekeleza.


Kwa mfano, madiwani na wabunge wengi wameshindwa kutekeleza ahadi za kushughulikia ukosefu wa ajira kwa vijana na huduma duni za afya na elimu, miongoni mwa matatizo mengine chungu nzima yanayowakabili wananchi katika maeneo yao ya uongozi. Matokeo yake wananchi maskini wameendelea kuwa maskini wa kutupwa, huku madiwani na wabunge waliowachagua kwa matarajio ya kuwaletea maendeleo wakidhihirika kujiboresha na familia zao katika uchumi na maisha kwa jumla.


Kutokana na hali hiyo, Fikra ya Hekima inawahimiza Watanzania kuhakikisha wanakuwa makini kwa kuepuka kuwapa uongozi wanasiasa wanaotafuta ulaji. Tuwapatie uongozi watu wanaotufaa katika kipindi hiki cha mageuzi ya uchumi na mapambano dhidi ya umaskini.