Katika sehemu ya mwisho ya makala hii tunaangalia jinsi utakavyompa mwathirika huduma ya kwanza kwa matatizo yafuatayo kabla hajatokea daktari au atakapopelekwa zahanati ama hospitali kwa tiba inayostahili …

 

Kula Sumu

Mtu akila sumu (poisoning by mouth) anahitaji kufanyiwa huduma ya kwanza haraka sana. Sumu iliyoingia tumboni inaweza ikapunguzwa nguvu kwa kunywa maziwa au maji mengi. Halafu mgonjwa ashawishiwe kutapika. Kuna njia za kuweza kumfanya atapike. Unaweza kumtia kichefuchefu kwa kumpa bilauri ya maji ya moto yaliyotiwa hamira (backing powder), ama yaliyotiwa povu la sabuni (soapsuds). Kama anakataa anyweshwe kwa nguvu.

Baada ya kumpa maji hayo na akawa hatapiki, kumtekenyatekenya kwa vidole nyuma ya shingo yake au mbele kooni kunaweza kumtapisha. Baada ya kutapika apewe bilauri ya maziwa yaliyotiwa kijiko kimoja kidogo cha chumvi ya haluli (epsom salt). Mchanganyiko huo hupambana na sumu (antidote) na kumletea nafuu aliyekula sumu za aina nyingi. Kama inaonekana mgonjwa anapoteza fahamu, ama kupatwa na shock, yafaa atiwe joto mwilini kwa kumpa kahawa, chai au kinywaji kingine cha moto.  

 

Kuchomwa na Vitu

Kuchomwa na vitu vyenye makali kama msumari, kisu, jembe, uma ama mkuki, bati na mbuzi ya kukunia nazi, lazima kuchukuliwe kama ni jambo la hatari. Michomo hii inayoingia ndani mwilini husababisha maambukizo ya ugonjwa mbaya wa pepopunda (tetanus au lockjaw), ingawa majeraha ya aina hii huwa hayatoi damu nyingi. Bana kwa upapi wa kitambaa kwa juu si karibu sana na sehemu yenye jeraha kuzuia damu isitoke kwa wingi. Mgonjwa apelekwe hospitali, baada ya kusafisha sehemu hiyo kwa maji mengi na sabuni. 

Kizunguzungu

Hutokea mtu akasikia kizunguzungu, kisulisuli, gumbizi au kisunzi (vertigo) ambapo mwili wake hukosa uwezo wa kusimama wima, huku akiona kila kitu kinazunguka au kutembea, kuelekea upande fulani. Na katika kufikiria kuwa ndiye anayeyumba ama kuzunguka, hujaribu kuvifuatilia na kujiweka anavyofikiria kuwa ndiko sawa. Hivyo, humfanya ayumbe na hatimaye huanguka. Mtu awapo na kizunguzungu husikia pia kichefuchefu (nausea).

Hii zaidi husababishwa na kuwapo kwa kitu kama nta (wax) ndani ya sikio. Kuna dawa, kama vilivyo vileo, ambavyo hutokea vikasababisha kizunguzungu. Vertigo inaweza pia ikawa ni alama (sign) ya magonjwa mengine. 

 

Kutokwa na Damu Puani

Mtu anayevuja damu puani (nose bleeding) yafaa awekwe kitako. Nguo alizovaa zilegezwe shingoni, vifungo na tai vifunguliwe. Kwanza asafishwe damu iliyoganda nje na ndani ya pua na iminywe kwa nguvu. Mdomo wake wa juu ubinuliwe kwa juu. Kama kwa kufanya hivyo damu haitakoma haraka kuvuja, chukua shashi (gauze) au kitambaa kilichofuliwa ukisokomeze ndani ya pua, katika hali ambayo haitaleta tabu kuja kukichomoa baadaye. Kamwe usitumie pamba kumtia puani mtu anayevuja damu.

 

Kwikwi

Kwikwi (hiccups) ni namna ya mishtuko inayokuja ikaachia na kuja tena katika kiwambo cha mnofu, kinachotenganisha uwazi wa tumboni na wa ndani ya kifua (diaphragm). Mara nyingi mtu akishikwa na kwikwi anaweza akaizuia kwa kunywa maji ya baridi sana au maji ya limau au ya ndimu. Kuuvuta ulimi, kupenga kamasi au kupiga chafya husaidia kuondoa kwikwi.

Lakini kama mtu anaendelea kuwa na kwikwi kwa muda wa saa nyingi, itabidi apelekwe kupimwa ili ijulikane kwikwi yake inatokana na kitu gani hasa, kwani huletwa kutokana na mambo mengi.