Ally-Edha-Awadh-Tanzania536098d68ea44dec173aFebruari, 2013 tuliandika habari ambayo hatimaye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, imeuthibitishia umma ilikuwa kweli.

Kampuni ya Mafuta ya Lake Oil imebainika kukwepa kodi ya Sh bilioni 8.5 kwa kufanya udanganyifu kwenye biashara ya mafuta kwa kutumia kivuli cha usafirishaji nishati hiyo nje ya nchi. Imepewa miezi miwili ilipe, na kama haikufanya hivyo, basi ishitakiwe.  

Hili si jambo jipya hata kidogo. Uchunguzi wetu kwa wakati huo ulibaini kuwa Lake Oil ilikuwa imekwepa kodi iliyofikia Sh bilioni 26. Bado tunaamini kiwango kilichotajwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, cha Sh bilioni 8.5 ni kidogo. Uchunguzi zaidi unapaswa ufanywe.

Kama ilivyo kwa matukio mengine makubwa kama haya, bado tunaahidi kuisaidia Takukuru kwa kuipa nyaraka zinazohusiana na ukwepaji kodi huu. Tunafanya hivyo tukijua hatari iliyo mbele yetu, lakini hatuna namna nyingine, ispokuwa kuifia nchi hii iliyobarikiwa.

Tunasikia wengine sasa wakisema wafanyabiashara wakibanwa namna hii, wataikimbia nchi! Naamini wakikimbia wataenda kwenye nchi zilizofanana na Tanzania ya wakati huo, na kamwe hawataenda Marekani, Uingereza, Ujerumani, Japan au katika taifa lolote linalojua maana na umuhimu wa kodi. Vitisho hivi ni vya kupuuzwa kwa sababu ulipaji kodi umehalalishwa hata kwenye maandiko matakatifu.

Mwaka 2013 tulipoandika Lake Oil ilikuwa ikiuza mafuta yasiyolipiwa kodi kwa kisingizio cha kuyasafirisha nje ya nchi (on transit), tulikuwa hatubahatishi.

 Tukasema mafuta hayo, badala ya kupelekwa nchi jirani kama wahusika walivyodai, yalikuwa yakiuzwa katika soko la ndani; vituo vingi vikiwa jijini Dar es Salaam na eneo lote kuanzia Kibaha hadi Morogoro.

Kampuni ya Lake Oil inamilikiwa na mmoja wa wafanyabiashara wanaotajwa kuupata utajiri mkubwa wakingali na umri mdogo.

Ukwepaji kodi wa Lake Oil ulishamiri mwaka 2011 na kuendelea hadi mwaka juzi.  JAMHURI ina nyaraka nyingi zinazothibitisha haya.

Mchezo uliofanywa na kampuni hiyo kwa kiwango kikubwa uliwahusisha maafisa kadhaa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Wakaguzi wa Mafuta. Baadhi ya majina ya wahusika wakuu tunayo, lakini lililo jema ni kuwa miongoni mwao wameshakumbana na mkono wa ‘mtumbua majipu’.

 Mafuta hayo yasiyolipiwa kodi yamekuwa yakifurika katika soko la mafuta nchini, na hiyo kuwa miongoni mwa sababu zilizofanya bei ya nishati itofautiane kutoka kampuni moja hadi nyingine licha ya ukweli kuwa mafuta mengi yanaagizwa kutoka nje kwa pamoja.

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), wakati huo ikidhani kuwa ilifanikiwa kusimamia vema soko la mafuta nchini kwa kuweka bei elekezi na bei kikomo, ukweli tulioubaini ulikuwa kwamba bei hiyo kwa kiwango kikubwa ilidhibitiwa na udanganyifu kwenye ukwepaji kodi.

Kampuni ya Lake Oil ilikuwa ikiuza mafuta kwenye vituo vyake na vya kampuni nyingine kwa kiwango cha chini kuliko hata kile cha uagizaji kikijumuishwa na kodi za hapa nchini.

Kwa mfano, kodi zote kwa lita moja ya dizeli – gharama za uagizaji na kodi kabla ya kuuzwa kwenye soko la rejareja wakati huo ilikuwa Sh 1,918.24; lakini kampuni hiyo ilikuwa ikiuza lita hiyo hiyo moja kwa wastani wa Sh 1,840 hadi Sh 1,890.

Sababu hiyo ikatajwa kuwa miongoni mwa sababu nyingi zilizozifanya kampuni nyingine, ikiwamo BP zifunge biashara zake nchini kwa sababu ni ukweli ulio wazi kwamba kwa uadilifu wao wa kulipa kodi zisingeweza kushindana na zile zilizokwepa kodi au kufanya ujanjaujanja kwa kuuza nchini mafuta ambayo yalipaswa kusafirishwa nje ya nchi.

BP walijitahidi kulalamikia suala la ukwepaji kodi kwenye mafuta, walikwenda hadi ngazi za juu serikalini na katika TRA, lakini hawakusikilizwa. Walikuwa hawawezi kushindana kuuza mafuta yao dhidi ya mafuta ya wakwepa kodi. Wakwepa kodi waliuza bei ya chini mno ambayo hata haikufikia kiwango halali baada ya kukokotoa kodi zote.

Kilio kama hicho kilichowasibu BP ndicho walichokabiliana nacho wafanyabiashara wadogo wadogo wa mafuta.

Mmoja wa wafanyabiashara hao alipata kuniambia maneno haya: “Sote tunaagiza mafuta kwenye soko la dunia. Tunanunua sehemu moja, tunasafirisha kwa kutumia meli moja, lakini tunapouza sokoni wenzetu wanauza mafuta kwa bei ya chini sana. Bei hiyo wakati mwingine inakuwa chini kabisa ya kiwango kinachopaswa kulipwa kihalali baada ya kodi zote halali za Serikali.

“Mafuta yanauzwa bei ya chini kwa sababu yale yanayopaswa kupelekwa DRC, Burundi, Rwanda au Zambia yanaishia hapa hapa nchini. Huwezi kushindana na wakwepa kodi. Wao wanauza bei ndogo. Wapo waliokwishafunga biashara hii, na sisi tuko njiani endapo Serikali haitadhibiti hali hii. Wahusika wanajulikana…”

 Mwaka 2013 tukaeleza kuwa kwa makusudi, kampuni zilizojihusisha na ukwepaji kodi zilisaidiwa na uongozi wa TRA na Wakala wa Vipimo kuhakikisha meta za kupimia kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini, hazitumiki! Tuna barua nyingi zilizoandikwa na uongozi wa juu wa TRA na Wizara ya Fedha kubariki wizi huo wa kuacha matumizi ya meta za mafuta.

Kwa kuacha meta, kilichofanywa na TRA eti ni kutumia nyaraka za waagizaji wenyewe!

 Tukasema kwamba udanganyifu wa mafuta yanayosafirishwa nje ya nchi, si pekee unaotumika kama mbinu ya ukwepaji kodi, bali mafuta huanza ‘kuibwa; bandarini kwa sababu flow meters hazitumiki.

Uchunguzi wetu ulibaini kuwa wastani wa malori 200 hadi 250 yenye dizeli na petroli hupata nyaraka za kughushi zinazoonesha kuwa nishati hiyo inapelekwa nje ya nchi, lakini matokeo yake huingizwa kwenye soko la ndani.

Ni kipindi hicho ambacho Lake Oil na kampuni nyingine nyingi ziliweza kupanuka kwa kufungua vituo vya mafuta vingi jijini Dar es Salaam, eneo la Barabara Kuu ya Dar es Salaam-Morogoro, na maeneo karibu yote nchini.

Wakati tukifanya uchunguzi huo tukabaini meli zaidi ya 20 zilizoingiza mafuta ya dizeli na petroli, lakini sehemu ya mafuta hayo hayakulipiwa kodi. Baadhi ya meli hizo ni za Torm Almena, Ocean Princes, CPO Singapour, Navig 8, UACC Shams na nyingine.

Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ikatufanya kama mahayawani tunaoandika uongo na uzushi. Hata kama ilijaribu kufuatilia yale tuliyoyaandika, matokeo yake yakawa sifuri.

Kwa mfano, mafuta ya Lake Oil yaliyodaiwa kupelekwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kati ya Oktoba 8, 2011 hadi Septemba 20, 2012 sehemu yake ilisambazwa katika soko la ndani.

Desemba 12, 2011 meli ya UACC Shams ilipakua dizeli ambayo sehemu yake ilipakiwa katika malori 15 na kuonesha yanasafirishwa nje ya nchi, lakini yaliishia kuuzwa katika soko hili hili la ndani. Nyaraka za mambo haya zipo, lakini kama tulivyosema, tulipuuzwa kwa kila hali.

Leo inashangaza kuwasikia baadhi ya watu wakisema tuna ugomvi binafsi na Mheshimiwa Kikwete. Wengine wanaenda mbali zaidi kwa kusema hasira zangu, au zetu zilitokana na ‘kuukosa u-DC’. Nani kasema u-DC ni kazi ya maana zaidi kuliko hii tunayoifanya ya kuifia nchi yetu? DC ana wigo gani wa kufukua haya tunayofukua kwa manufaa mapana ya Taifa letu?

 

Mchezo ulivyo

Nyaraka bandia huandaliwa kuonesha kuwa mafuta ya petroli au dizeli yanasafirishwa kwenda nje ya nchi. Kwenye hati hizo huandikwa namba bandia za magari. Mfanyakazi wa kampuni inayokwepa kodi alitumika kuchukua nyaraka hadi Misugusugu, Kibaha mkoani Pwani, kwa ajili ya kupigwa mhuri. Hapo Misugusugu kuna kituo kwa shehena zinazosafirishwa nje ya nchi.

Katika kituo hicho, afisa wa TRA walilipwa wastani wa Sh milioni 2 kwa kila ‘gari’; na baadaye nyaraka hizo zikapelekwa mpakani Tunduma ambako maafisa wa TRA dau lao lilipanda hadi Sh milioni 4 kwa kila lori la dizeli na Sh milioni 6 kwa nyaraka za lori lenye petroli. Nyaraka zile za kughushi zilibarikiwa na kule ambako inaonesha mafuta yangepelekwa (nchi husika).

Baada ya kukamilisha mchezo huo, mafuta huingizwa katika soko la ndani bila kulipiwa ushuru wowote.

Tulizungumza na TRA, wakakiri kuwa wameshaubaini wizi huo, ingawa hawakuonesha namna yoyote ya kuibana Lake Oil na kampuni nyingine zilizokwepa kodi.

TRA wakawa wakweli kwa kusema licha ya baadhi ya kampuni nyingi za mafuta kushirikiana na watumishi wa Mamlaka hiyo, lakini vitisho kutoka kwa vigogo na familia zao ilikuwa sababu tosha ya kuwavunja nguvu kiutendaji.

Naibu Kamishna wa Forodha kwa wakati huo, Bellium, nilimwuliza swali wakati wa semina kati ya TRA na wahariri katika Hoteli ya Courtyard, Dar es Salaam, na majibu yake yakawa haya: “Tuko mbioni kuanzisha Mfumo Mpya wa Forodha. Utasaidia utoaji mizigo bandarini na kuhakiki mizigo inayostahili kusafirishwa nje ya nchi. Mfumo huu unaitwa TANCIS. Nawahakikishia kuwa mfumo huu utasaidia sana kudhibiti udanganyifu kwenye bidhaa nyingi yakiwamo mafuta.

“Natoa wito kwa wananchi wenye taarifa za wakwepa kodi kuziwasilisha TRA, na majina yao yatakuwa siri. Kwa yeyote anayefanikisha kukamatwa kwa magendo na ukwepaji kodi, atalipwa asilimia tatu ya kiwango cha kodi ambayo TRA wanastahili kukipata kwenye bidhaa husika.”

Haya si maneno yangu, bali ya afisa huyo wa TRA. Wasomaji wanaweza kuamua kama kweli JAMHURI tunastahili, au hatustahili kuipata asilimia hiyo tatu!

Ndugu zangu, nareja kusema tena na tena kuwa hatuna ugomvi na mtu, lakini tuna maslahi kwa rasilimali za nchi yetu. Huu umekuwa msimamo wetu tangu tulipoamua kwa dhati kuanzisha JAMHURI.

Historia ni somo zuri sana. Taifa la watu wasiofundishwa au wasiotaka kurejea historia, ni Taifa mfu. Historia inatusaidia kujua tumetoka wapi, tuko wapi na tunataka kuelekea wapi. Tunapoisema Serikali ya Awamu ya Nne hatufanyi hivyo k,wa husda, bali ni kwa kuzingatia rejea ya mambo ya aina hii. Kama wapo wanaoudhiwa na hiki tunachokifanya, watuwie radhi. Tunafanya hivi ili Rais Magufuli, na wasaidizi wake watambue kuwa wana kazi kubwa na wajibu halali wa kusikiliza na kuchukua hatua pale wanapopewa taarifa zenye ukweli kama hizi za ukwepaji kodi wa Lake Oil kwenye biashara ya mafuta.

Woga ndiyo silaha dhaifu kuliko zote kwenye mapambano yoyote.

Mithali 3: 27 tunasoma haya: “Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, Ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda.”

Kwa maandiko haya, tunawapa watu mema ya kusaidia kupata kodi ili zilifikie Taifa zima. Tunafanya hivyo kwa sababu tumejaaliwa mkono wa kuyatenda. Tukiwanyima haki hiyo Watanzania, Mungu atatuadhibu. Tunaijua hatari iliyo mbele yetu lakini neno la Mungu katika Mithali 3:25-26 linasema: “25 Usiogope hofu ya ghafla, Wala uharibifu wa waovu utakapofika.

“26  Kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako, Naye atakulinda mguu wako usinaswe.”