Wiki hii linaanza Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bunge hili linaanza na changamoto nyingi. Linaanza na changamoto ambayo vyama vya upinzani ukiacha ACT-Wazalendo havijichanganui iwapo havitambui ushindi wa Rais John Magufuli au vinautambua.
Wakati anahutubia Bunge walitoka nje ya Ukumbi Novemba 20, 2015, lakini linapokuja suala la mgogoro wa Zanzibar mara kadhaa nawasikia wakitamka kumwomba Rais Magufuli aingilie mgogoro huo.
Wapo waliosema bungeni wametoka kupinga uwepo wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ila wengine wanasema walitoka ukumbini kupinga vitendo vya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na mazigira yaliyompatia ushindi Rais Magufuli.
Hata hivyo, ipo Ibara ya 41 (7) inayosema: “Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.” Kwa wenye kuheshimu utawala wa sheria wanajua kifungu hiki kimefunga harakati nyingi.
Sitanii, inawezekana kwa Zanzibar tumesahau haraka. Mwaka 2001 wakati Chama cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) vinaingia mwafaka, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema: “Haya yametokea, tusameheane ila tusisahau.” Inawezekana baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), wakubwa wametekeleza yote. “Wamesameheana na wakasahau.”
Nimeligusia hili la Zanzibar kwani naona unyanyapaa na hatari inayotengenezwa. Baada ya kulifuta gazeti la Mawio ni wazi Serikali ilikuwa inatuma salaam. Salaam nzito na nene kuwa yeyote atakayefungua mdomo atashughulikiwa vilivyo.
Watakuwa huko walikokaa wanafurahi nakusema anayetaka kujua unyeti wa suala la Zanzibar, basi achungulie Mawio. Nasema utawala wa aina hii haukubaliki kufungia magazeti bila kupitia mahakamani.
Napata tabu, kuwa suala hili linaweza kuandikwa kishabiki. Niseme tu, jambo ambalo pengine si wengi wanaolifahamu. Miaka 16 iliyopita, mimi ndiye niliandika habari ya “CUF yatoa siku 90.” Habari hii niliiandika baada ya kumhoji aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Wilfred Lwakatare (sasa mbunge kupitia Chadema). Mahojiano haya niliyafanya Novemba, mwaka 2000.
Huwezi kuamini, Mwaka 2000 CUF walikuwa wanataka uchaguzi urudiwe ndani ya siku 90 alizozitamka Lwakatare katika habari hiyo niliyoiandika kwenye gazeti la Mwananchi. CCM walikuwa wakijenga hoja kuwa kwa hali yoyote uchaguzi hauwezi kurudiwa wote. CCM walikuwa wakisema uchaguzi hata kama ulikuwa na dosari haiwezekani kusema uchaguzi wote ulikuwa na dosari hivyo ufutwe na kurudiwa wote.
Ikumbuke CUF walikuwa wanatoa madai hayo baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutangaza matokeo yaliyoipa CCM ushindi. Zamu hii ni kinyume. CCM wamekataa matokeo kabla hayajatangazwa, na Tume imefuta uchaguzi wote, ikiwamo ya baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliokuwa tayari wamepewa hati za ushindi safi!
Sitanii, baada ya CCM kukataa matokeo hata kabla hayajatangazwa rasmi na ZEC, wakataka uchaguzi urudiwe, mengi yametokea. Jecha Salim Jecha, nadhani naye ‘ametii amri’, sasa uchaguzi umetangazwa kurudiwa Machi 20, 2016. Najua bungeni ndiko siasa zinakopaswa kuhamia baada ya uchaguzi. Huko bungeni sasa natarajia mjadala wenye masilahi kwa taifa katika tukio hili.
Narudia, ikiwa tumesamehe na kusahau, Lipumba aliona miaka mingi mbele. Kwa jeuri ya dola tunaweza kuanza kusikia kauli za kumwita Amani Abeid Karume msaliti hadharani. Hii Sadifa Khamis Juma hakunifurahisha. Inawezekana alikuwa na umri mdogo mwaka 2000 na 2001 wakati yanatokea mauaji Zanzibar na ndiyo maana anaweza kutoa kauli ya utayari wa kutawala minazi.
Sadifa hafahamu kuwa Zanzibar walifika mahala kwa sababu ya siasa tu, wananchi wakawa hawazikani. Wakawa CCM na CUF hawashirikiani katika harusi. Ikawa mabomu yanalipuka kila kukicha. Zanzibar ikafika mahala kila kukicha visima vya maji tunakuta vimetapakaa kinyesi. Ile ilikuwa fadhaha ya aina yake. Msuguano uliokuwapo Zanzibar uliendelea kukua mwaka hadi mwaka.
Hata kama hatufahamu Karume na Maalim Seif walikubaliana nini Novemba 2009, lakini hatua ya wawili hawa kufikia mwafaka uliowashinda akina Chifu Emeka Anyauko na wengine, tufahamu kuwa ilikuwa hatua kubwa. Kufanikiwa kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ingekuwa nguzo ya kujenga demokrasia ya kweli.
Kwa bahati mbaya, ninachokishuhudia sasa kuna watu wapo kazini. Wameshika nyundo wanabomoa amani, utulivu, mshikamano na demokrasia Zanzibar. Yakumbukeni maneno yangu, ninao uzoefu wa kinachoendelea Zanzibar. Hofu yangu ni kuwa suala la Zanzibar likiingizwa katika Bunge linaloanza leo kwa njia ya vijembe, eti Serikali haitolewi kwa makaratasi, tujiandae kuwa sehemu ya historia chafu.
Sitanii, jingine katika uzoefu wangu wa masuala ya kibunge napata shida. Zitto bado ni kijana na inawezekana naye hana kumbukumbu za uendeshaji wa masuala ya Bunge. Kwa kuwa ni msomaji mzuri, pengine nimkumbushe na kumtabiria hatima yake kisiasa. Mtu aitwaye Augustino Mrema, aliingia bungeni kwa kishindo. Mwaka 1994 alilitikisa Bunge kwa kashfa ya mashamba ya mkonge Tanga, yaliyokuwa yanabinafsishwa kwa P.V. Chavda.
Zitto akumbuke wakati huo Mrema alikuwa CCM na Naibu Waziri Mkuu. Baadaye alikwenda upinzani kwa nguvu kubwa, nusura awe Rais wa Tanzania kupitia NCCR Mageuzi mwaka 1995. Kadri siku zilivyopita, biashara ya jumla alisema kwake ilizidi kuwa ngumu akahamia rejareja, kwa maana ya kuacha kugombea urais na kuhamia kwenye ubunge.
Kidogo kidogo, Mrema aliendelea kupoteza mwelekeo kwa kiwango ambacho akaanza kuungana na CCM ambao awali aliwapinga. Si Mrema pekee, John Cheyo mzee wa ‘out a.k.a mapesa’ alikuwa na wabunge wanne, akiwamo Danny Makanga. Alikuwa moto wa kuotea mbali. Ghafla chama chake kilianza kufifia kama moto wa kifuu akabaki na mbunge mmoja, ambaye ni yeye. Yaliyowapata wawili hawa mwaka 2015, unayafahamu na yaliyobaki ni historia.
Nafahamu uhusiano wa karibu alionao Zitto na Mwenyekiti wa CCM, Prof. Dk. Mhe. Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete. Najua uhusiano huo ulivyofifisha uwezo wa Zitto kufikiri akawaona wapinzani wenzake ni magarasa tu. Najua alivyofanikiwa kulipata Jimbo la Kigoma Mjini. Zitto sasa ameanza kuwachokoza wenzake wa kambi ya upinzani bungeni kwa kuwambia Kamati za Bunge ziko sawa tu!
Zitto akiendeleza mkondo wake wa kuwaona wapinzani wenzake si lolote si chochote, atathibitisha maudhui ya mchezo wa kuigiza wa “Mkataa Pemba…” Ni imani yangu kuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai hataruhusu mijadala ya ushabiki isiyo na tija bungeni. Suala la Zanzibar, miundo ya Kamati za Bunge, anapaswa kuliangalia kwa jicho la ukomavu.
Sina uhakika sana kama Kamati ya Maendeleo ya Jamii inayosimamia bajeti ya Sh bilioni 15 ni sawa na Kamati ya Nishati na Madini inayosimamia trilioni 1 au Miundombinu inayosimamia trilioni 3.5 au ya bajeti inayosimamia trilioni 22. Yapo malalamiko ya wazi, kwamba baadhi ya wenyeviti waliokabidhiwa kamati ni majanga.
Sitanii, leo siko hapa kukosesha watu furaha, lakini nakuhakikishieni baadhi ya Kamati huenda zitafanya kazi kwa ufanisi mdogo kuliko maelezo. Zipo kamati ambazo ni moyo wa nchi. Sikutarajia wabunge tunaowafahamu kwa uzembe wao leo ndiyo wenye kuongoza Kamati hizi nyeti. Nyaraka za miradi na mashirika yaliyoko chini ya kamati hizi ni nyingi na sina uhakika iwapo wakubwa hawa watazisoma.
Ninachokishuhudia sasa ni uhalisia kuwa huenda tukarejesha Bunge la kanyaga twende. Hawa wenyeviti wa kamati wasio na uwezo sahihi watataka kujitutumua na matokeo yake, wataishia kurusha vijembe. Angalau mpaka dakika hii nafurahi sijasikia wabunge wakipepetana kama mabunge yaliyotangulia. Naamini kuwa watajadili hoja kwa staha, badala ya kauli za funga milango tupigane kidogo.
Sitanii, Rais John Pombe Magufuli ameanza vyema. Haikuwa kazi rahisi kuwambia matajiri akina Said Salim Bakharesa, Bin Sulum na wengine walipe kodi. Kuna watu wamevuliwa viatu na mikanda polisi jambo ambalo hawakupata kuliwaza maishani mwao. Ni katika msingi huo nashawishika kusema Rais Magufuli aungwe mkono kwa kila hali.
Nchi ilipo sasa inahitaji kujengwa upya. Tufute mawazo ya misaada na uchuuzi, kwa maana ya kuuza bidhaa za kutoka nje ya nchi tuwekeze katika ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati. Hivi leo kweli kuna sababu gani ya Tanzania kuagiza mitumba wakati tunalima pamba? Kuna sababu gani kwa taifa letu kuagiza hadi njiti za meno wakati tuna misitu tele?
Haya ndiyo masuala ninayotarajia Bunge letu lijadili. Bunge lijadili masuala ya kuwezesha Watanzania kumiliki uchumi. Majirani zetu Kenya wemechukua mfano wa China. Benki ya Biashara ya Kenya kwa sasa Mkenya akipata zabuni yoyote ya kutoa huduma hapa nchini anapeleka LPO anapewa fedha kwa sharti la kufungua akaunti kwenye benki yao.
Kwa bahati mbaya sisi tunawaza siasa zaidi ya biashara. Hatuwezi kupata kodi kutokana na maneno ya majukwaani. Kodi inapatikana katika kuwawezesha Watanzania wakajenga viwanda vya viatu, zikatumika ngozi za wanyama wetu na kuuza nje ya nchi viatu.
Ni kwa kuwawezesha Watanzania wakajenga viwanda vya mabati, nondo, misumari na vifaa vya plastic (PVC) vitakavyowawezesha kuzalisha wakauza ndani na nje ya nchi kisha wakalipa kodi, tutaendelea.
Sitanii, na naomba kuhitimisha hii makala ya leo kwa kuwaomba wabunge watumie Bunge la 11 kuanza safari ya kujenga matajiri nchini Tanzania. Bila kujali itikadi, wabunge ishauri na kuisimamia Serikali iwezeshe wazawa kumiliki uchumi wa nchi hii wazalishe, wauze ndani na nje ya nchi. Kama ni siasa tumefanya miaka 50 iliyopita, hatujaona matunda yake zaidi ya kujifurahisha kisaikolojia.
Kama alivyosema Rais Magufuli kuwa atawawezesha wafanyabiashara Watanzania naamini ni wakati wa kuumuunga mkono, tukiwa na ndoto ya siku moja kuwapa msaada Marekani. Wapo wanaoweza kudhani hizi ni ndoto, lakini Angola mwaka 2011 imeipa Ureno msaada wa dola milioni 80 kwa njia ya uwekezaji. Kama Angola imeweza kwa nini sisi tushindwe? Tunaweza, tuchukue hatua.