Serikali imezitaka kamati za ulinzi na usalama katika Mikoa na Wilaya zote nchini pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuanzisha operesheni ya kuwaibaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria waagizaji na wasambazaji wa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku na Serikali.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis (kulia) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima wakati wa mazungumzo baina yao yaliyofanyika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kabla ya kuanza kwa ziara ya Naibu Waziri kukagua miradi ya sekta ya mazingira mkoani Mwanza iliyoanza Februari 22, 2023.

Agizo hilo limetolewa jana Jijini Mwanza na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi wa dampo la kisasa lililojengwa Kata ya Buhongwa Jijini Mwanza.

Naibu Waziri Khamis amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kutokana na athari za mazingira na pia mifuko hiyo kuwa hatarishi kwa afya za wananchi, hata hivyo wapo baadhi ya watu wamekuwa wakikiuka katazo la matumizi ya mifuko hilo lililotolewa na Serikali mwaka 2019.

“Tumeona katika dampo hili la Buhongwa limekuwa ni kituo cha mifuko ya plastiki, hii imeonesha kuwa huko mitaani kuna watu wanaojishughulisha na biashara ya uagizaji na usambazaji wa mifuko ya plastiki isiyo na ubora.

Naziagiza Kamati za Ulinzi, NEMC na Mabaraza ya Halmashauri ya Wilaya kusimamia mianya yote inayopenyeza mifuko hii” alisema.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Khamis Hamza Khamis akisalimiana na Viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa dampo la kisasa lililojengwa katika Kata ya Buhongwa Wilayani Nyamagana jijini Mwanza Februari 22, 2023.

Aidha Naibu Waziri Khamis alisema nadharia za kisayansi zimedhibitisha kuwa mifuko ya plastiki inaathari kubwa kimazingira kutokana na kuchukua kipindi kirefu kutekeleza na kuoza kuanzia miaka mitatu na kuendelea na hivyo kuleta tishio kwa kubwa kwa maisha na ustawi wa viumbe na binadamu.

Akifafanua zaidi alisema Serikali ya Awamu ya Sita kamwe haitorudi nyuma katika katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki na kuwataka watu wachache wanaojishughulisha na biashara ya uagizaji na usambazaji wa biashara hiyo kuacha mara moja kabla ya kukamatwa na kufikishwa katika na mkono wa sheria.

Katika hatua nyingine,Khamis ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kuanzisha mradi huo ambao utasaidia juhudi za Serikali za kutotumia fedha nyingi kwenye ununuzi wa vifaa tiba kwa kuwa taka zinazozalishwa katika Jiji la Mwanza zitapelekwa kwa wakati katika dampo hilo na kunusuru magonjwa ya mlipuko.

Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara wa mapambano ya uharibifu wa mazingira na katika kudhibitisha kauli kwa vitendo ametoa sh.bilioni 3 kwa kila Halmashauri nchini kwa ajili ya kuanzia miradi ya ujenzi madampo ya kisasa ynayochakata taka kisayansi na kulinda afya za wananchi.

Akizungumzia ujenzi wa mradi wa dampo hilo, Meneja mradi wa dampo hilo kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza Desderius Polle amesema ujenzi wa dampo lenye ukubwa wa hekta 34 uliokamilika mwaka 2020 una thamani ya sh.bilioni 8.9 na unafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Programu ya Uendelezaji wa Majiji ya Kimkakati Tanzania (TSCP).

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Khamis Hamza Khamis akikagua mradi wa dampo la kisasa mradi wa dampo la kisasa lililojengwa katika Kata ya Buhongwa Wilayani Nyamagana jijini Mwanza wakati wa ziara yake Februari 22, 2023

Polle amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa shimo la kuhifadhi taka ngumu lenye ukubwa wa mita za mraba 39,000, ujenzi wa barabara ya zege yenye urefu wa Kilomita 0.7, ujenzi wa barabara ya changalawe yenye urefu wa kilomita 1.8, ujenzi wa bwawa la kuhifadhi maji ya mvua, ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua, upandaji wa miti na uwekaji wa taa za barabarani na maegesho ya mitambo na uchimbaji visima.

Naye Diwani wa Kata ya Nyamagana, Joseph Kabadi ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kusimamia vyema utekelezaji wa mradi wa dampo hilo la kisasa ambalo litakuwa suluhisho wa utunzaji wa mazingira kwa kuwa taka ngumu zitakuwa zikiteketezwa kwa wakati na hivyo kulinda za afya za wananchi wanaozunguka kata hiyo.Naibu Waziri Khamis yupo katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazohusu sekta ya mazingira nchini.