Na Daniel Limbe, Jamhuri Geita
Wakati kukiwa na uvumi kwamba Uwanja wa Ndege wa Chato mkoani Geita umetelekezwa na sasa unatumika kwa kuanikia nafaka, hali sivyo ilivyo.
Uwanja huu bora na wa kisasa uliojengwa wakati wa utawala wa Awamu ya Tano wa Rais Dk. John Magufuli, ulilalamikiwa katika mitandao ya kijamii, ukitajwa kutokuwa na faida yoyote.
Baada ya Magufuli kufariki dunia Machi 2021, watu wengi waliamini au kuaminishwa kuwa matumizi ya uwanja huo yamekwisha na kubaki kile kinachoitwa kwa Kiingereza ‘White Elephant’.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba Uwanja wa Ndege wa Chato kwa sasa ni miongoni mwa viwanja muhimu Kanda ya Ziwa, kikitumiwa na wakazi wa mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma, pamoja na wafanyabiashara wa Rwanda na Burundi.
Mfano ni wafanyakazi na watafiti wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), ambao kwa sasa hawatumii Uwanja wa Ndege wa Mwanza kutokana na umbali pamoja na foleni za magari katikati ya Jiji la Mwanza.
Kwa kutambua umuhimu wa uwanja huo, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) imeamua kuupanua na tayari mchakato wa kuchukua mashamba na maeneo jirani umeanza.
Februari 13, mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedit Katwale, amekutana na wadau wa maendeleo na wananchi wanaomiliki maeneo yanayotarajiwa kuchukuliwa na TAA kuzungumzia suala hilo kwa manufaa ya umma.
Baadhi ya wananchi wanataka kufahamu watapata nini kwa kuachia maeneo yao, wengine wakionyesha shaka ya malipo ya fidia, wakidai kuwa baadhi yao walipunjwa wakati wa shughuli kama hiyo walipopisha ujenzi wa kambi teule ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) 663 KJ.
Wamesema walitapeliwa fedha za kuhamisha makaburi baada ya uthamini wa awali kuonyesha kuwa thamani ya kaburi moja ni Sh 700,000; kwamba miongoni mwa fedha hizo, Sh 500,000 zingetumiwa na serikali kufukua makaburi na kuyahamishia eneo jingine na Sh 200,000 zingetolewa kwa familia ya marehemu mhusika.
Hata hivyo, hilo halikufanyika, wakidai kuwa serikali iliingia mitini na Sh 500,000 hivyo wananchi kulazimika kutumia Sh 200,000 walizopewa kufanya shughuli ya kufukua na kuhamisha makaburi ya wapendwa wao pasipo msaada wa serikali.
“Sasa mmekuja tena na maneno yenu. Mnategemea tutawaamini vipi wakati zile Sh 500,000 kwa kila kaburi mlitudhulumu?” anahoji Shema Bunzali mbele ya mkuu wa wilaya.
Mkazi mwingine wa Kijiji cha Nyabilezi, Samweli Fimbo, anapaza sauti kuonyesha dhuluma kubwa aliyofanyiwa katika tathmini ya mwaka 2021 iliyoonyesha kuwa alikuwa na shamba lenye ukubwa wa ekari 27, lakini wakati wa kupokea fidia akaambiwa ukubwa wa shamba hilo ni ekari tisa tu.
“Mheshimiwa DC, mimi nipo tayari kuachia eneo langu kwa sharti moja; mthamini wa serikali akalipime upya lililokuwa shamba langu, tuondoe ekari tisa na zinazobaki nilipwe fidia.
“Ule ulikuwa utapeli mkubwa. Watu wamenunua magari kwa fedha zetu za fidia,” anasema Fimbo.
Wakazi wengine, Abednego Jumbula na James Kafuru, wanasema hawana imani na uthaminishaji unaofanywa na serikali iwapo una nia njema kwa wananchi kutokana na kiwango kidogo cha fidia inayokusudiwa kutolewa ikilinganishwa na hali halisi na jinsi maisha yalivyopanda.
Wanasema Sh 600,000 kwa ekari moja ni fedha chache ambazo hazitawasaidia kupata ardhi eneo jingine katika vijiji jirani, kwa kuwa ekari moja kwa sasa ni Sh 1,000,000.
Eneo linalotarajiwa kuchukuliwa na TAA lipo katika vijiji vya Nyabilezi, Kata ya Bukome na Ngw’abaluhi, Kata ya Katende; eneo linalopakana na kambi ya JWTZ.
Ofisa Mthamini Mkoa wa Geita
Awali, akizungumza na wananchi, Ofisa Mthamini Mkoa wa Geita, Nelson Gilbert, anasema ofisi yake hufanya uthamini kulingana na miongozo iliyopo na kwamba suala la malipo hufanywa na Hazina ambaye ndiye mlipaji mkuu wa serikali.
“Sisi ni kama marefarii tu. Tunafanya uthamini kwa maana ya kuzitendea haki pande zote mbili; serikali na wananchi. Hatuhusiki na malipo.
“Udogo wa malipo hutokea baada ya Mthamini Mkuu wa Serikali anapojiridhisha na kuandaa ripoti yake,” anasema Gilbert.
Anawatoa hofu wananchi akisema uthamini utakaofanyika utazingatia sheria, taratibu na kanuni kwa kuwashirikisha wananchi ipasavyo wakati wa kuhakiki mali zilizopo kwenye ardhi yao.
Anawasihi kushiriki wao wenyewe badala ya kutuma wawakilishi ambao wakati mwingine huwa hawajui mipaka, jambo linaloweza kusababisha manung’uniko yasiyo ya lazima.
“Tuhesabu kwa pamoja miti, nyumba, makaburi, mazao na mengineyo. Hii itasaidia kupunguza malalamiko japo haitakuzuia kupinga iwapo unaona kuna vitu havikuorodheshwa kwenye jedwali la uhakiki,” anasema Gilbert.
Kwa upande mwingine, DC Katwale ameonyesha kukerwa na utapeli wa fedha za kuhamisha makaburi, akiahidi kufuatilia jambo hilo kujua waliohusika.
“Kwa hili, hata mimi sikubaliani nalo. Huwezi kumkata mtu Sh 500,000 kati ya Sh 700,000 halafu usitekeleze ulichoahidi. Lazima nilifuatilie,” anasisitiza.
Anasema uwepo wa uwanja wa ndege Chato umeongeza fursa ya maendeleo kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa, huku watalii wakiutumia kwenda hifadhi za taifa za Burigi-Chato na Rubondo.
Anawataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali kwa kutoa maeneo yao kwa hiari ili upanuzi wa uwanja uendelee kama ilivyokusudiwa na kuupandisha hadhi.
Kaimu Meneja wa Uwanja wa Ndege Chato, Mary Mihayo, anasema wastani wa abiria 40 kutoka Dar es Salaam hushukia Chato na kwenda maeneo mbalimbali.
Mary Anatupilia mbali uvumi kuwa uwanja huo haufanyi kazi baada ya kifo cha Dk. Magufuli.
“Ndege za ATCL hufanya miruko mara mbili kwa wiki kutoka Dar es Salaam. Abiria ni wa kutosha na kuna wakati wengine hukosa nafasi. Abiria waendelee kutumia uwanja huu kwa kuwa ni mzuri na huduma zetu ni bora sana,” anasema.
Anaitaka jamii kufahamu kwamba uwanja unaendelea na kazi na kupuuza uvumi unaolenga kupotosha umma.
“Abiria wetu wengi ni wafanyakazi na wamekuwa wakitoa maoni ya kuongezwa safari kutoka mbili hadi tatu kwa wiki, kwamba kutawasaidia wale wanaopenda kusafiri mwishoni mwa wiki,” anasema Mary.
Anatumia fursa hiyo kuyakaribisha mashirika mengine ya ndege kufanya safari za Chato kutokana na ongezeko la abiria.
Uwanja wa Ndege wa Chato unasifika kwa ubora wake na ukubwa wa eneo, huku barabara ya kurukia ndege ikiwa na urefu wa kilomita tatu.
Mbali na ndege za abiria, uwanja huo hutumiwa pia na ndege za jeshi.
Nini kifanyike?
Serikali iwatendee haki wananchi wanaotarajiwa kuondolewa kwenye maeneo yao kupisha upanuzi wa uwanja kwa kuwashirikisha katika kila hatua ya uthamini na kuwalipa kulingana na thamani ya ardhi na hali ya maisha kwa sasa.
Serikali isifanye makosa tena kwa kushindwa kuwasaidia wananchi kuhamisha makaburi ya wapendwa wao kutokana na tamaa ya wachache wenye lengo la kuwaibia wananchi.
TAA iweke wazi muda wa kuanza kutumia eneo hilo ili kutoa nafasi kwa wananchi kulima na kuvuna mazao ya muda mfupi kutokana na uhaba wa chakula uliopo sasa.
Serikali ichukue hatua kwa watumishi waliohusika kufisadi fedha za makaburi za mwaka 2021.
Wananchi watambue umuhimu wa kuwa mbali na maeneo ya viwanja vya ndege kwa masilahi yao na serikali.
Jamii ielimishwe namna inavyoweza kujikwamua kiuchumi kwa kutumia fursa za uwepo wa viwanja vya ndege katika maeneo yao.