Na. Edward Kondela,JamhuriMedia,Arusha
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Shilingi Bilioni 5.9 kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya ujenzi wa minada mipya na ukarabati wa minada ya zamani ili kuboresha usalama wa mifugo.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (Mb.) amebainisha hayo mwanzoni mwa wiki, wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Mnada wa Meserani uliopo Mkoani Arusha, ambapo amesema lengo la serikali ni kuhakikisha inajenga na kuboresha minada mbalimbali nchini ili kuwa na hali ya usalama zaidi.
Ulega amesema Mnada wa Meserani ambao unafanyiwa ukarabati kwa kuwekewa uzio mpya unagharimu Shilingi Milioni 167 na kwamba ujenzi wa uzio huo unaendelea vizuri.
“Nimeona shughuli za ujenzi wa ukuta wa Mnada wa Meserani unaendelea vizuri kwa ajili ya usalama wa mifugo kunapokuwa na ukuta imara mnakuwa na uhakika wa usalama wa mifugo yenu.” amesema Ulega
Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa niaba ya wafugaji, inamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Shilingi Milioni 167 kwa ajili ya kuboresha Mnada wa Meserani, huku akiwa ametoa jumla ya Shilingi Bilioni 5.9 katika minada yote nchini kwa ajili ya ujenzi wa minada mipya na kuiboresha minada ya zamani.
Nao baadhi ya wafugaji katika Mnada wa Meserani wameshukuru jitihada za serikali katika kuwaboreshea mazingira ya minada kuwa na usalama zaidi, huku wakiiomba serikali kuzidi kuwaondolea changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wakati wa kusafirisha mifugo pamoja na upatikanaji wa mahitaji muhimu ya mifugo katika minada yakiwemo maeneo maalum ya kupumzishia mifugo yao.
Katika hatua nyingine akiwa kwenye ziara hiyo ya kikazi ya siku moja Mkoani Arusha Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb.), kwenye Kijiji cha Naalarami kilichopo Wilaya ya Monduli, kushuhudia ujenzi wa bwawa la kunyweshea maji mifugo maji litakalogharimu Shilingi Milioni 466 amemtaka mkandarasi kuanza ujenzi mara moja ili wananchi wa eneo hilo kuanza kupata maji mara mvua zitakapoanza kunyesha.
Pia, amewaasa wananchi wa jamii ya ufugaji kuwa na utaratibu wa kuvuna mifugo yao na kuondokana na tabia ya kuwa na mifugo mingi isiyo na tija kwao ambapo mingine hufa kutokana na ukosefu wa malisho na maji wakati wa ukame na hasa nyakati hizi za mabadiliko ya tabia ya nchi.