Na Cresensia Kapinga,JamhuriMedia,Mbinga

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma ACP Marco Chilya amewataka madereva wa malori yatokayo ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kubeba makaa ya mawe mkoani Ruvuma kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao wakizingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili waweze kuepukana na ajali zisizo za lazima.

Ameyasema hayo leo huko kijiji cha Amani Makolo Barabara ya Kitai – Ruanda katika machimbo ya makaa ya mawe baada ya kutokea kwa ajali mbili zikihusisha malori ya makaa ya mawe na pikipiki katika Vijiji vya Muhiwesi na Songambele- Nakambale Wilaya ya Tunduru na kusababisha vifo vya watu sita ambao walikuwa wamebebwa mtungo kwenye pikipiki.

Kupitia hilo pia kamanda Chilya amewataka madereva hao kuwa makini kutokana na operesheni na doria maalum za usiku na mchana zinazoendelea kufanyika maeneo yote ya mkoa ambapo mpaka sasa makosa hatarishi 41 na madereva tisa wa malori wamekamatwa kwa makosa hatarishi ikiwemo mwendokasi na kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari ambapo watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Kamanda Chilya amesema kuwa Jeshi la Polisi limepanga mikakati mbalimbali ya kuweza kupunguza wimbi na ongezeko la ajali za barabarani ikiwemo ukaguzi wa kina wa magari ili kudhibiti ajali zitokanazo na ubovu wa vyombo vya moto na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wanaoendesha vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara.

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya akitoa elimu kwa baadhi ya madereva wa maroli yanayobeba makaa ya mawe katika Kijiji cha Amani Makolo kilichopo wilayani Mbinga.

Kwa upande wake kaimu kamanda wa kikosi cha usalama barabarani (RTO) Mkoa wa Ruvuma ACP Muya Zuberi Maunganya amewataka wamiliki wote wa vyombo vya moto kutumia fursa hii ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kuweka stika kwenye vyombo vyao na kwa wale ambao watakuwa hawajaweka stika hatua za kisheria zitachikuliwa dhidi yao.

Kwa upande wao madereva hao wa maroli wamelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma kwa kuwapatia elimu ya usalama barabarani na wameliomba jeshi hilo kutoa elimu kwa madereva bodaboda na waenda kwa miguu kwani kwa asilimia kubwa wao ndio wamekuwa chanzo cha ajali za barabarani na si vinginevyo.