Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limekamata mtandao wa majambazi sita ambao wamedaiwa kujihusisha na utekaji na kupora eneo la msitu wa Nyimbili Kata ya Mtungwa wilayani Momba almaarufu BoT (Benki Kuu) kutokana na mfululizo wa matukio ya ujambazi eneo hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe,Theopista Mallya, akizungumza jana amesema majambazi hao wamekamatwa Februari 17, mwaka huu, baada ya kufanya uporaji saa 7:00 usiku katika msitu huo.

Kamanda Mallya amewataja waliokamatwa kuwa ni Shughuli Siame (47) mkazi wa kijiji cha Nambinzo, Furaha Sembuli (49) mkazi wa Mlowo wilayani Mbozi, Andalwisye Gwalamba (41) mkazi wa kijiji cha Ntungwa Wilaya ya Momba.

Wengine ni Oden Simtenda (45) mkazi wa Ntungwa, Lowa Simbeye (51) mkazi wa Ntungwa na Andrew Simlembe mkazi wa kijiji cha Chilulumo wilayani Momba

zaidi tukio hilo alisema watuhumiwa hao wakiwa na silaha za moto na za jadi walivamia na kuteka magari 10 likiwamo lililobeba maiti ya mwanafunzi na kisha kuwapora fedha,simu vitu vingine mbalimbali abiria waliokuwa wakisafiria magari hayo.

Amesema majambazi hao walikuwa na bunduki, mapanga na mashoka ambapo waliwaamuru abiria kwenye magari kushuka na kisha kuanza kuwapora mali zao.

Amesema katika magari 10 yaliyotekwa katika msitu huo ambao maarufu unaitwa msitu wa BoT,moja ya magari hayo lilikuwa limebeba maiti ya mwanafunzi lenye namba za usajili SM 14056 ilikuwa ikisafirishwa kutoka wilayani Momba kwenda wilayani Mbozi.

Kamanda Mallya alisema majambazi hao baada ya kuteka magari hayo walianza kuwapora abiria simu na fedha ambapo katika gari lililobeba maiti walipora fedha taslimu Sh.216,000 pamoja na simu za watu waliokuwa wakisindikiza maiti hiyo zenye thamani ya Sh.1,200,000.

Amesema baada ya tukio hilo kutokea polisi walianza msako haraka na kufanikiwa kuwakamata watu sita wanaosadikiwa kuhusika katika tukio hilo na mmoja wa watuhumiwa alikutwa na simu mbili ambazo zinasadikiwa kuporwa eneo la tukio

Katika kipindi cha ndani ya mwezi mmoja na nusu majambazi wamefanya uporaji katika msitu huo mara mbili tukio la juzi likiwa ni la tatu.

Katika tukio la kwanza waliteka magari manne saa 4:00 usiku yaliyokuwa yakitokea mnadani katika kijiji cha Kamsamba na tukio la pili waliteka basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster na Noah.

Please follow and like us:
Pin Share