Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara inayodhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, hatimaye imeanza Jumamosi iliyopita huku timu tatu za Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club mabingwa watetezi, Azam (Wanalambalamba) iliyoshika nafasi ya pili na Dar es Salaam Young Africans (Yanga) ya mitaa ya Jangwani na Twiga, zote za jijini zikipewa nafasi kubwa ya kuitawala. Simba iliyoonesha kiwango kikubwa kabisa cha soka msimu uliopita, safari hii imepata straika mahiri kutoka Ghana, Daniel Akuffo na Mrisho Ngassa, winga aliyepelekwa huko kwa mkopo na timu yake ya Azam baada ya kuibusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, wakati wa michuano ya Kombe la Kagame miezi miwili iliyopita.
Hata hivyo, kuhamia kwake Simba kumemfurahisha mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo raia wa Uganda, Emmanuel Okwi aliyetamba kwamba miguu yake msimu huu itakuwa ya moto kuliko uliopita.
“Thamani” ya Okwi ilithibitika wakati wa michuano ya Kombe la Kagame wakati Simba ilipofanya vibaya, hatua iliyosababisha baadhi ya wachezaji wakiwamo wa kulipwa kutoka nje ya nchi waliosajiliwa kuamua kuachana nao mara moja.
Hata kocha Milovan Cirkovic alikiri waziwazi kwamba kutokuwapo kwa mshambuliaji huyo aliyekuwa akifanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Uturuki, kulisababisha safu nzima ya timu hiyo kutokuwa lolote.
Kauli kwamba akiwa pamoja na Mrisho Ngassa uwanjani wakicheza kikosi kimoja itakuwa ni baala, ilianza kuonekana Jumanne iliyopita wakati Simba ilipokwaana na Azam katika mechi ya Ngao ya Hisani ya kuashiria kuanza kwa Ligi Kuu wakati Wekundu hao wa Msimbazi walipotoka kifua mbele. Wote pamoja na Mwinyi Kazimoto ndiyo walioipa ushindi wa mabao 3-2 timu yao licha ya kutoka nyuma huku ikilazimika kusawazisha kwanza.
Mbali na hao, Akuffo naye ameonesha umahiri mkubwa wa kufanya mambo makubwa uwanjani, hivyo inawezekana Simba ikawa bora zaidi msimu huu na kuweza kutetea vizuri ubingwa wake, lakini iwapo tu safu ya ulinzi itakuwa imara ili kuwadhibiti washambuliaji wa timu inazopambana nazo.
Licha ya hao, wachezaji wengine wanaotarajiwa kung’ara katika ushambuliaji ni pamoja na John Bocco wa Azam, straika ambaye msimu uliopita ndiye aliyeondoka na kiatu cha dhahabu. Alitumbukiza wavuni mipira 19 na huenda akawa mzuri zaidi safari hii, lakini atakosa krosi maridadi alizokuwa akizipata kutoka kwa Mrisho Ngassa na Ramadhani Chombo Redondo aliyehamia pia Simba.
Mapengo hayo mawili kwa timu hiyo ni makubwa na huenda ikajilaumu kwa uamuzi wake wa jazba wa kumpeleka Mrisho Ngassa kucheza kwa mkopo Simba, kule alikoanza kuonesha makali aliyokuwa nayo miaka miwili iliyopita.
Nayo kwa upande wake, Yanga inayonolewa na kocha Mbelgiji Tom Saintfiet inajivunia safu yake mpya ya mbele yenye washambuliaji mahiri kama Saidi Bahanuzi aliyetokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, Didier Kavumbagu aliyesajiliwa kutoka Atletico de Burundi ya Bujumbura, Burundi na mabeki walioitosa Simba na kuipa kiwewe – Kelvin Yondani na Mbuyu Twite.
Washambuliaji hao wawili wanatarajiwa kuongeza makali ya mbele kwa timu hiyo ambayo msimu uliopita iliwategemea zaidi Kenneth Asamoah, raia wa Ghana aliyetemwa, pamoja na Mganda Khamis Kiiza ambaye bado yupo.
Ukiziacha timu hizo tatu, nyingine zinazoshiriki ligi hiyo ni Coastal Union na JKT Mgambo za Tanga, JKT Ruvu na Ruvu Shooting Stars za Kibaha mkoani Pwani, Mtibwa Sugar na Polisi Tanzania zote za Morogoro, African Lyon ya Dar es Salaam, JKT Oljoro ya Arusha, Tanzania Prisons ya Mbeya, Kagera Sugar ya Kagera na Toto African ya Mwanza.