Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan amewataka Wakandarasi wazawa walioshinda zabuni kuhakikisha kufanya kazi zenye ubora kwa ufanisi, uaminifu na kufuata makubaliano yaliyofikiwa katika mikataba.

Rais Samia ametoa wito huo leo wakati akishuhudia utiaji saini mikataba ya kuimarisha gridi ya taifa na kusambaza umeme vijijini katika hafla iliyofanyika Ikulu.

Aidha, Rais Samia amewataka wakandarasi waliokosa kandarasi kuridhika na maamuzi ya zabuni yaliyoamuliwa kwa kuwa kupinga maamuzi hayo kunachelewesha kuanza kwa miradi iliyopitishwa

Vilevile, Rais Samia amezitaka wizara zinazohusika na malipo ya wakandarasi wa miradi kuhakikisha wanawalipa kwa wakati pindi wanapokamilisha kazi zao.

Aidha, Rais Samia amesema miradi hii yenye thamani ya shilingi trilioni 1.9 ni ya muhimu kwa wananchi kwa kuwa itaimarisha huduma za maji, kilimo, afya na hivyo kuleta maendeleo.

Shirika la Umeme (TANESCO) limeweka saini mikataba 6 kwa ajili ya miradi 26 ya gridi imara na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) imeweka saini mikataba 14 kwa ajili ya miradi ya kupeleka umeme kwenye migodi midogomidogo na maeneo ya kilimo.

Miradi hiyo itapeleka umeme katika maeneo 336 ya uzalishaji mali, vitongoji 1522, vituo vya afya 65 na maeneo 336 yenye vyanzo vya maji ili kujenga uchumi, kuongeza uwekezaji na utoaji huduma za jamii katika ngazi za chini.