Hatimaye Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wametiliana saini katika Hati ya Makubaliano ya kuuziana nafaka, hususan mahindi.

Makubaliano hayo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza juhudi za kunufaisha wakulima na ufanisi katika NFRA kwa manufaa ya Taifa kwa jumla.

 

Ikumbukwe kwamba NFRA ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kisheria kwa ajili ya kununua na kuhifadhi chakula ambacho baadaye hutumika kukabiliana na majanga ya kitaifa yakiwamo mafuriko na njaa.

 

Akizindua utilianaji saini wa makubaliano hayo mjini Dodoma hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Mohammed Muya, alisema hatua hiyo imekuja wakati mwafaka ambapo Tanzania inatekeleza Azimio la Kilimo Kwanza.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, alizindua Azimio hilo miaka minne iliyopita kutokana na kutambua mchango wa kilimo katika uchumi wa Taifa kama si kuboresha maisha ya Watanzania.


“Makubaliano haya yanatukumbusha na kutambua fursa zilizopo Tanzania kama ghala la chakula na soko kwa nchi zinazotuzunguka,” alisema Muya.


WFP ni mdau muhimu katika kutekeleza Azimio la Kilimo Kwanza ili kuhakikisha upatikanaji wa soko la uhakika wa nafaka zinazozalishwa katika mazingira yatakayochangia kukuza pato la wakulima nchini.


Licha ya sekta ya kilimo kuendelea kutajwa kuwa ndio uti wa mgogo wa uchumi wa Tanzania, wakulima wengi nchini wameendelea kukabiliwa na umaskini wa kipato na kimaisha kwa jumla. Huenda mkakati huo wa Serikali ukawa mkombozi wa wakulima nchini.


Mkurugenzi Mwakilishi Mkazi wa WFP, Richard Regan, anasema walianza kununua nafaka kutoka Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 2011, wakiwa wanunuzi wakubwa wa chakula Duniani.


WFP wanafanya kazi katika nchi 80 Duniani ambapo katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania ndiyo yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha nafaka. Mwaka jana shirika hilo lilinunua tani 80,000 hadi 100,000 zenye thamani ya kati ya Dola za Kimarekani 17 na milioni 18.


Kwa mujibu wa Regan, makubaliano hayo kati ya NFRA na WFP yanalenga kununua tani 200,000 za nafaka kwa mwaka, zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 35 hadi milioni 40.


Aidha, gharama za usafiri, maghala na bandari zinakadiriwa kuwa zaidi ya Dola za Kimarekani 100,000 sawa na Sh milioni 50 kwa mwaka, ambazo ni uwekezaji mkubwa katika uchumi wa Tanzania.


NFRA imekubali kununua asilimia 10 ya P4P kutoka kwa wakulima wadogo wadogo ili kuwapatia soko la uhakika kwa vile wengi wao wana uwezo wa kuzalisha ziada ya nafaka. Kwa sasa Mpango wa P4P unafanya kazi na vikundi 30 vya wakulima nchini.

 

Regan anasema wakifanikiwa watatoa mchango mkubwa katika kununua chakula kwenda nchi za Sudan, Somalia, Kenya, Uganda na Afrika Magharibi ambapo Mpango wa P4P utasaidia kufungua soko la nafaka na hivyo kuinua pato la wakulima wadogo wadogo.

 

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Charles Walwa, anasema taasisi hiyo ya Serikali imegawanyika katika kanda saba nchini; ambazo ni Kipawa mkoani Dar es Salaam, Arusha, Shinyanga, Dodoma, Makambako mkoani Iringa, Sumbawanga mkoani Rukwa na Songea mkoani Ruvuma.

 

Ni dhahiri kuwa hatua iliyochukuliwa na Serikali kupitia NFRA ya kusaini Hati ya Makubaliano ya kuuziana nafaka na WFP inalenga kuwanufaisha wakulima, kuimarisha ushirika na kujenga uwezo wa taasisi hiyo ya Serikali katika kushughulikia masuala ya usalama wa chakula.