majaliwaUongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ambao umeshikwa na baadhi ya viongozi walioshiriki kwenye upotevu wa maelfu ya makontena, unafanya kila mbinu kujinasua kwenye kashfa hiyo.

Juhudi hizo za kujinasua zinatokana na Gazeti la JAMHURI kuwataja kwa majina na vyeo viongozi walioshiriki kwenye upotevu huo, lakini sasa wakiwa wamekabidhiwa dhima ya kuongoza vitengo mbalimbali nyeti katika TPA.

Nyaraka zilizolifikia JAMHURI zinaonyesha kuwa Januari 4, mwaka huu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, P. Gawile, alimwandikia barua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, akijaribu ‘kuwaondoa’ kwenye kashfa ya upotevu wa makontena 2,431.

Gawile ametoa maelezo yanayolenga kuwatetea Rajah Mdoe (Naibu Mkurugenzi Mkuu), Hebel Mhanga (Kaimu Meneja wa Bandari Dar es Salaam), Koku Kazaura (Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria) na Phares Magesa ambaye kwa sasa ni Ofisa Mwandamizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Gawile, katika maelezo yake anasema Menejimenti ya TPA imepokea maelezo ya kila mhusika na kuyachambua.

Lililo kubwa kwenye hitimisho la taarifa yake ni kwamba wote wanaotajwa kuhusika kwenye upotevu huo si wao kama wao binafsi, bali ni uteuzi wa Idara za Fedha, TEHAMA, Ulinzi, Utekelezaji na Idara ya Huduma za Sheria.

Lakini haelezi ni kwa namna gani wakuu wa Idara hizo wanavyoweza kuepuka ‘kitanzi’ ambacho wao kama wawakilishi wa Idara, walihusika moja kwa moja.

“Idara haipo kama hewa. Idara inaongozwa na watu. Asema nani waliohudhuria kwenye vikao maana idara yenyewe haiingii kwenye kikao,” kimehoji chanzo chetu cha habari.

Gawile anasema idara hizo ndizo zilizounda Kamati ya kusimamia TICTS, ICDS na CFS, na si uteuzi wa majina.

“Hivyo viongozi hawa Idara zao ndio zilipewa majukumu, na si wahusika wa moja kwa moja,” anahitimisha Gawile katika utetezi wake.

Gawile, amefanya uchambuzi wa kila mmoja na kuainisha kama ifuatavyo:

 

Rajah Mdoe (Naibu Mkurugenzi Mkuu)

Anasema mhusika hapo awali alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Fedha. Hata hivyo alipandishwa cheo kukaimu nafasi ya Naibu Mkurugenzi Mkuu (H).

“Maelezo ya Bw. Mdoe yanaonyesha kuwa hakuteuliwa yeye kama mjumbe wa Kamati iliyoundwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu (Madeni Kipande). Sambamba na Idara kuwa miongoni mwa Wajumbe wa Kamati, alitekeleza majukumu yake na kutoa ushauri mbalimbali kama inavyoonekana kwenye kumbukumbu za vikao,” anasema Gawile.

 

Hebel Mhanga (Meneja wa Bandari)

Gawile anakiri kuwa kipindi Kamati inaundwa, Mhanga alikuwa Bandari ya Dar es Salaam katika nafasi ya Meneja Makasha (makontena).

Anasema: “Kabla ya kupandishwa cheo hakuwa Mjumbe wa Kamati husika, hivyo alipandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Utekelezaji na kuchukua dhamana ya kuongoza na kuwa mwakilishi wa Kamati/Tume iliyoundwa.”

 

Kokutulage Kazaura (Mkurugenzi wa Huduma za Sheria)

Maelezo ya Gawile, yanasema kuwa baada ya kuchambua maelezo yake ameona hahusiki na tuhuma za upotevu wa makontena kwa kuwa taaluma na majukumu yake ya kazi havihusiani na sakata lililojitokeza.

 

Lazaro Twange (Mkuu wa Ulinzi)

Gawile anasema Idara ya Mkuu wa Ulinzi ni miongoni mwa Idara teule zilizokuwa zikiunda Kamati ya kushughulikia TICTS, ICDs na CFS.

Anasema barua ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA ya Desemba 5, mwaka jana kwenda kwa Waziri Mkuu zinaonyesha kuwa taarifa ya upotevu wa makontena 2,431 zilitolewa na Mkuu wa Ulinzi.

Kwa sababu hiyo, Gawile, anasema: “Menejimenti ilipendekeza asichukuliwe hatua za kinidhamu.”

 

Phares Magesa (TEHAMA)

Gawile anamtetea kwa kusema: “Kwa sasa Phares Magesa ni ‘Principal Web Management Officer’. Hapo awali alikuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi wa TEHAMA. Kwa mujibu wa maelezo ya Bw. Magesa ni kuwa hakuteuliwa kuwa mjumbe, bali uteuzi uliofanyika ni Idara yake kuwa Mjumbe wa Kamati.”

 

Baada ya utetezi kwa kila mmoja, Gawile, amefikia hitimisho kwa kusema: “Kwa kuzingatia maelezo niliyopokea na uchambuzi uliofanyika, ni maoni yangu kuwa watumishi waliotajwa hapo juu kuhusishwa na tuhuma za upotevu wa makontena 2,431 tuhuma zao haziwezi kuwatia hatiani kwa kuzingatia Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004 na Kanuni zake.”

Tofauti na ilivyoelezwa na Kipande wakati akiunda Kamati hiyo, Gawile anametoa ushauri kwa kusema: “Kamati iliyoundwa (kusimamia TICTC, ICDS na CFS) haikupewa hadidu za rejea za kushughulikia upotevu wa makontena 2,431.

“Kamati haikupewa kushughulikia/kuingilia majukumu ya kila siku katika Bandari ya Dar es Salaam.

“Uteuzi uliopo ni uteuzi wa Idara za Fedha, TEHAMA, Ulinzi, Utekelezaji na Idara ya Huduma za Sheria kuunda Kamati ya TICTS, ICDS na CFS na si uteuzi wa majina. Hivyo viongozi hawa Idara zao ndio zilipewa majukumu na si wahusika wa moja kwa moja.”

 

Wiki iliyopita JAMHURI liliripoti kuwa watendaji walioteuliwa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Badari, Kipande kusimamia upakiaji na upakuaji wa makontenda kisha yakaanza kupotea kwa kiwango cha kutisha na mengine kuibwa, ndiyo sasa wanaokaimu nafasi nyeti TPA.

Mwanzo, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim alibaini upotevu wa makontena 329 yaliyoitia Serikali hasara ya wastani wa Sh bilioni 12, baadaye wakagudua makontena 2,387.

Ilipofikia hatua hii, Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Awadhi Massawe akaagiza ufanyike uchunguzi wa kina, na kubaini upotevu wa makontena 11,884 yaliyolitia taifa hasara ya Sh bilioni 47.4 na magari 2,019 yalitolewa bila kulipiwa kodi au ushuru.

Makontena 11,884 yamebainishwa na Profesa Makame Mbarawa, Waziri mwenye dhamana ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano baada ya uchunguzi alioagiza Massawe.

Kutokana na hali hiyo, Watumishi saba wa bandarini iliamuriwa wakamatwe na Jeshi la Polisi na wengine wanane wakatoroka.

Novemba, mwaka jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alibainisha kuwa ukaguzi uliofanywa Julai 30, mwaka huu uligundua kuwapo kwa mianya mingi ya ukwepaji kodi yakiwamo makontena 2,387 yaliyopitishwa kati ya Machi na Septemba mwaka jana kinyume cha taratibu.

Majaliwa akifanya ziara ya kushitukiza bandarini Dar es Salaam Novemba 27, mwaka jana. Alifichua mwanya wa ukwepaji kodi kwa makontena 329 yenye thamani ya wastani wa Sh bilioni 12. Aliwasimamisha kazi baadhi ya maofisa wa TRA; na muda mfupi baadaye Rais John Magufuli, akamsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade.

Kwa upande wa TPA aliowasimamisha kutoka idara ya usimamizi wa ICD ni Happygod Naftari, Juma Zaar, Mkango Alli na Steven Mtui. Wengine ni Titi Ligalwike, Lyidia Kimaro, John Elisante na James Kimwomwa.

Kwa upande wa viongozi waliotoa ruhusa kwa makontena hayo kuondoshwa bandarini nao wamesimamishwa. Hao ni aliyekuwa Meneja Mapato ambaye alikuwa amehamishiwa Kitengo cha Fedha cha Makao Makuu, Shaaban Mngazija, aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mkuu wa Bandarikavu ambaye pia alikuwa amehamishiwa Makao Makao Makuu kuwa Naibu Mkurugenzi Huduma za Biashara, Rajah Mdoe.

Wengine ni Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Ibin Masoud na Meneja Bandari Msaidizi Fedha, Apolonia Mosha.

Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka kwa kushindwa kusimamia TPA na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).

Pamoja na Mwinjaka, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadhi Massawe. Pia alivunja Bodi ya Wakurugenzi ya TPA na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TPA Profesa Joseph Msambichaka.

Wajumbe wa Bodi waliotenguliwa walikuwa ni Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Haruna Masebu; Dk. Francis Michael, Mhandisi Gema Modu, Mhandisi Musa Ally, Nyamsingwa, Crescentius Magori, Flavian Kinunda na Donata Mugassa.

Uchunguzi unaonyesha kuwa aliyepeleka taarifa za upotevu wa makontena kwa Waziri Mkuu Majaliwa alipiga hesabu za mbali akilenga kumkomoa Massawe aliyekuwa ameshika wadhifa huo ndani ya miezi miwili tangu kuthibitishwa kwake.

Massawe alianzisha safisha safisha Bandari baada ya kupata wadhifa huo kwa kufanya mabadiliko makubwa ikiwamo kuwashusha vyeo ‘waliomchoma’, kurejesha nidhamu bandarini, kuhamisha watumishi 30 katika kitendo cha fedha na kurejesha kazini idadi kubwa ya watumishi waliokuwa wameondolewa na Kipande kwa chuki.

“Huyu mtu alipeleka taarifa hizi kwa Waziri Mkuu, akishirikiana kwa karibu na waliokuwa wasaidizi wa Kipande, na kweli wamefanikiwa maana wamepeleka nusu taarifa, Massawe amewajibishwa kwa kosa lisilo lake na wapambe wa Kipande wanaowasiliana naye kila siku na walioshiriki kupoteza makontena wameteuliwa kukaimu nyadhifa nyeti,” anasema mtoa taarifa wetu.

Kaimu Mkurugenzi wa sasa wa TPA, Injinia Aloyce Matei, aliyeteuliwa kushika wadhifa huo badala ya Massawe imeelezwa kuwa alipelekwa Bandari na Kipande.

“Kipande alikuwa hawezi kufanya uamuzi wowote bila kumshirikisha huyu Matei maana alikuwa mkono wake wa kuume. Kwa vyovyote vile na kwa kuwa Naibu wake, na kwa jinsi wanavyoendelea kuwasiliana kwa ukaribu hata uki-print out mawasiliano yao, basi utaona aliyosema Kipande kuwa atarudi Bandari hata kama kupitia mgogo wa mtu mwingine, hili limefanikiwa,” anasema mtoa taarifa wetu.

 

Chanzo cha makontena kupotea

Kipande wakati akiwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA alipitisha waraka uliozaa matatizo yote yanayoshuhudiwa sasa bandarini.

Awali, Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa ikisimamia upakuaji na upakiaji wa makontena, lakini Kipande akahamishia majukumu hayo makao makuu.

Kipande aliyekuwa na urafiki mkubwa na Waziri wa Uchukuzi wa wakati huo, Dk. Harrison Mwakyembe, Februari 5, 2013 aliiandikia Bandari ya Dar es Salaam kuieleza rasmi kuwa ameunda Kamati Maalumu hivyo jukumu la makontena limechukuliwa na makao makuu.

Katika barua hiyo yenye Kumb. Na DG/3/3/06 (nakala tunayo) Kipande alimtaka Mkurugenzi wa Utumishi, Gawile kwa kushirikiana na wakurugenzi wengine kusimamia kitengo cha makontena hasa TICTS, ICDs na CFS.

Jukumu la Makontena alilikabidhi kwa barua mikononi mwa Mkuu wa Ulinzi – Swange, Mkurunzi wa Fedha – Rajah Mdoe (amesimamishwa), Mkurugenzi wa Mawasiliano na Teknohama –  Phares Magessa (ameshushwa cheo), Mkurugenzi wa Utekelezaji – Hebel Mhanga (Sasa ndiye Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam) na Mkuregenzi wa Huduma za Sheria – Kokutulage Kazaura.

Wakati huo, Massawe alikuwa Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam na kumbukumbu zinaonyesha upotevu wa makontena ulikuwa ni wastani wa makontena manne kwa mwaka, lakini baada ya Kipande kuunda Kamati hiyo, kwa mwaka 2014 upotevu wa makontena ulifikia karibu 14,000 kwa mwaka.

Katika barua hiyo, Kipande alidai anaipunguzia Bandari ya Dar es Salaam mzigo, anaiepusha na mgongano wa masilahi na uamuzi wake huo ulilenga kuongeza ufuatiliaji, utendaji na mapato.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa mwaka 2013 baada ya uamuzi huo wa Kipande, makontena 4,200 na magari 919 vilipitishwa bila kulipiwa ushuru. JAMHURI ina nyaraka za ripoti ya uchunguzi zinazothibitisha madai hayo.

Kipande, aliondolewa kwenye wadhifa huo na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, kutokana na tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Wataalam wa masuala ya sheria waliozungumza na JAMHURI, wameeleza mshangao wao kwa nini hadi leo Kipande hajakamatwa.

“Haiwezekani mtu aliyefanya uamuzi wa ovyo kiasi hiki, leo aendelee kuwa kazini. Wanasulubiwa watu wengine, lakini yeye anaendelea kucheka tu yuko uraiani. Hili haliwezekani,” alisema mmoja wa watu waliohojiwa na kutaka Kipande akamatwe haraka kwani amelitia taifa hasara kubwa.