Rais Dk. John Magufuli ametikiswa na ripoti ya rushwa katika mahakama za Tanzania. Ameanza kulivalia njuga suala hilo kwa kasi ya ajabu.
Mbali ya madai ya kubambika kesi kunakofanywa na Jeshi la Polisi, taarifa mpya zilizotua mezani kwa Rais Dk. Magufuli au JPM zinasema kumekuwa na matukio yasiyoridhisha dhidi ya wananchi wanaosaka haki zao mahakamani.
Huko kunaelezwa kuwa na mwenendo mbaya wa kesi unaokwenda sambamba na kuwanyima haki watu, kesi kusikilizwa muda mrefu hali inayochochewa na watendaji wa mahakama kudaiwa kula rushwa.
“Mheshimiwa Rais, hataki kusafiri. Anasoma mafaili. Moja ya mafaili yaliyomsononesha ni namna mahakama inavyofanya kazi. Hasa upande wa waendesha mashtaka. Hawa nao huendesha kesi muda mrefu,” anasema ofisa mmoja mkuu wa Serikali.
Katika Mahakama za Tanzania, Serikali imepeleka waraka kwa Majaji na Mahakimu kumaliza kesi za muda mrefu hususasi za madai. Wameagizwa kesi hizo zifike mwisho kabla ya Desemba 31, mwaka jana.
Hata hivyo, Hakimu mmoja katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani, anasema ameshindwa kufikia mwisho huo na kwamba baadhi ya kesi zitaendelea kusikilizwa huku akitaka mawakili na wahusika wengine kwenye kesi kuhudhuria mahakamani.
“Napeleka kesi hii, hadi Januari 14, mwaka huu, lakini tayari tuna waraka hapa uliotutaka kumaliza kesi hizi kabla ya Desemba 31, mwaka 2015,” anasema hakimu huyo.
Anasema: “Serikali inapata hasara ya kuita mashahidi kila wakati wa kuendesha kesi kubwa. Mahakimu na majaji nao wanaingia kwenye lawama, wameagizwa kesi zisikilizwe kwa wakati. Rais alikwisha agiza kwamba kesi zote zilizofunguliwa chini ya mwaka 2012 zifikie uamuzi kabla ya Desemba 31, mwaka jana.”
Matatizo kama hayo ambayo husababisha baadhi kuachia kesi zao njiani wakati kuna mashahidi hupoteza maisha na kesi kuanguka, zimemsukuma Rais Dk. Magufuli kufanya mazungumzo na vigogo kadhaa akiwamo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga na kuwapa majukumu yatakayokwenda na kasi ya Hapa Kazi Tu.
Mwingine aliyekutana naye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad aliyeagizwa kuangalia njia sahihi itayosaidia kupunguza gharama za matumizi ya kuendesha Serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Kuhusu mahakama, taarifa zinasema baina ya wageni wote waliomuona Rais Dk. Magufuli ni kuwa DPP Mganga alikaa muda mrefu na mkuu wa nchi akitaka kujua sababu za kesi nyingi kubwa hasa za dawa za kulevya na rushwa kuchukua muda mrefu.
Mbali ya kujadiliana hayo, taarifa zinasema DPP alipewa taarifa namna ofisi yake inavyozungukwa na watuhumiwa wakubwa wa kesi mbalimbali kiasi kwamba Serikali inashindwa kesi nyingi mahakamani.
Inadaiwa kuwa upande wa mashtaka ama hupeleka ushahidi dhaifu kiasi cha watuhumiwa kupata mwanya wa kushinda kesi dhidi ya Serikali ambazo mwisho wa siku, huacha maswali mengi kwa wananchi.
Kadhalika watuhumiwa hao hufungua kesi za madai dhidi ya Serikali ambayo huingia adhabu ya kulipa faini kubwa.
Mtoa taarifa wa gazeti hili anasema vyombo vya uchunguzi vya Serikali vimeanza kufanyia kazi taarifa kuwa baadhi ya watuhumiwa kwenye kesi za matumizi mabaya ya ofisi na rushwa zilizofunguliwa mwishoni mwa mwaka jana, nao wameanza kuwazonga maofisa kutoka ofisi ya DPP.
DPP Mganga anathibitisha kukutana na Rais Dk. Magufuli na kuzungumza naye kwa kina kuhusu mikakati ya namna ofisi yake inavyopaswa kufanya kazi ili kuendana na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”
“Sisi ndio tunaowajibika kwa wananchi. Ofisi ya DPP ni daraja kubwa la haki kati Serikali na wananchi. Kwa hiyo lazima tuifanye kazi,” anasema DPP alipozungumza jijini Dar es Salaam baada ya kuteta na Rais Dk. Magufuli.
DPP hakutaka kuzungumza suala hilo kwa kina, zaidi ya kusema: “Tumezungumza umuhimu wa kuwahimiza Watanzania kufuata sheria, na kwamba ofisi yangu itatekeleza wajibu wake bila kumwonea mtu. Hatutamwonea mtu ni haki tu.”
Ripoti hiyo pia imemfikia Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye naye kwa moto uleule, amekiri kuwa na mazingira ya rushwa katika mhimili huo wa dola akisema, “Ni vema wakajitakasa kabla ya kutakaswa kisheria.”
“Ni vigumu kumnyooshea kidole mtu mmoja-mmoja kuhusu tuhuma za rushwa, lakini taarifa zipo na wanaohusika ni vema wakajisafisha. Au wakajitumbua kabla ya kutumbuliwa,” anasema Dk. Mwakyembe.
Anasema njia ya kukabiliana na tuhuma za sasa za mahakama ni kutekelezwa kwa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) juu ya uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi ili iwe rahisi kupambana na vitendo vya rushwa.
Watumishi walionyooshewa kidole kwa ujumla wao ni makarani, washauri wa mahakama au wazee wa baraza, mahakimu, maofisa wa magereza, polisi pamoja na waendesha mashitaka wanaofuatilia mwenendo wa kesi kuanzia mwanzo hadi wakati wa hukumu. Amesema baadhi ya watumishi (ambao hakuwataja kwa majina) wanachunguzwa na hatua hiyo ikifika, basi watatimuliwa kazi. Aliahidi kuboresha maslahi kwa wanasheria ili watimize kazi zao vema badala ya kuingia majaribuni.
Dk. Mwakyembe alikwenda mbali zaidi akitaka kuboresha ofisi ya DPP na maofisa wake, ili angalau kuwajengea mazingira ya kutoingia kwenye majarubu hasa sehemu ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Kesi ya hivi karibuni iliyotikisa vichwa vya habari ni kuhusu baadhi ya Watuhumiwa wa kesi ya dawa za kulevya ‘unga’ aina ya heroin kulalamika kucheleweshwa kwa shauri wakidai linachukua muda mrefu tangu lilipoanza mwaka 2013.
Watuhumiwa hao wanamlalamikia Jaji wa Mahakama Kuu, Upendo Msuya baada ya kuirusha kesi hiyo hadi mwakani wakati ilibidi iendelee mwezi Desemba, mwaka jana.
Watuhumiwa kwenye kesi hiyo waliokutwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito kilo 50 ni; Ismail Shebe mwenye hati ya kusafiria Na. AB 293433 na Rashid Said Salum, mwenye hati ya kusafiria Na. AB 012971. Wote wakazi wa Dar es Salaam.
Mbali ya watuhumiwa hao, yumo pia raia wa Iran, Majed Armand, mwenye hati ya kusafiria Na. 214488959 aliyezaliwa Chabahar, Agosti 25, 1973.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa kwa hatua za awali mwaka 2013, lakini Jaji Msuya aliiahirisha Novemba 30, 2015 lakini akairusha tena hadi Desemba 7, mwaka jana.
Ilipofika siku hiyo Jaji Msuya aliiahirisha tena kesi hiyo huku akijenga hoja ya kuiahirisha kwa sababu ya kuikataa hati ya upekuzi iliyofanywa na Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Lubbe, aliyewakamata watuhumiwa hao.
Katika tarehe na siku isiyojulikana mwaka 2013 ASP Lubbe, Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi cha Kabuku mkoani Tanga, alikamata gari lenye namba za usajili za Kenya KAW 276 G aina ya Mitsubishi Pajero likiwa na watu wawili. Pia kilelezo cha gari kilikataliwa mapema, lakni baadaye kilikubaliwa.
Watu hao – Shebe na Salum – ambao ni watuhumiwa wa kwanza na pili katika kesi hiyo, walikutwa na dawa za kulevya kilo 50. Zilifahamika kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin baada ya kupimwa katika maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Baada ya mahojiano na Polisi ndipo watuhumiwa hao walipomtaja Armand, mkazi wa Mikocheni B, Dar es Salaam, aliyeunganishwa kwenye kesi hiyo. Kabla alifuatwa nyumbani kwake ambako alipekuliwa na kugundulika kuwa na dawa nyingine za kulevya zaidi ya gramu 900.
Bila kutaka kufahamika nani hasa aliyekuwa kinara wa kulalamika, watuhumiwa hao wanaona kuwa hizo ni dalili za kuidhoofisha kesi hiyo dhidi ya watuhumiwa ambao wako ndani kwa sasa wakisubiri kesi hiyo iendelee tena hapo mwakani mara itakapopangiwa tena na Msajili wa Mahakama.
Mbali ya walalamikiwa katika kesi hiyo, pia mashahidi wanalalamika usumbufu kwani wamekuwa wakiitwa mara kwa mara bila kesi hiyo kuendelea na malipo yao kucheleweshwa.
Hii si kesi ya kwanza ya ‘unga’ kuendeshwa na Jaji Msuya, kwani kumbukumbu zinaonesha kwamba alipata kutoa dhamana kwa watuhumiwa wanne wakiwamo raia wawili wa nje, waliokuja kutoroka baadaye.
Watuhumiwa hao walikamatwa Februari 21, 2011 huko eneo la Jogoo, Mbezi Beach, Dar es Salaam wakiwa na kilo 179 zilizokuja kuthibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin.
Waliokamatwa na mzigo huo ni Watanzania – Fred Chonde na Zuberi Mbwana – wakati wale raia wa nje ni Shabaz Malik Muhammad, raia wa Iran. Ana hati mbili za kusafiria. Hati hizo ni PQ 5144792 ya Iran na nyingine KE611868 ya kutoka Pakistan. Mwenzake ni Adbulghai Pirbaksh, raia wa Pakistan, ambaye hati yake ya kusafiria ni ZF410415.
Wakati kesi hiyo ikiendelea, Jaji Msuya ndiye aliyewapa dhamana watuhumiwa hao Julai 5, 2011 kwa dhamana ya Sh milioni 10 katika dawa zenye thamani ya Sh bilioni tatu.
Taarifa zinasema kwamba watuhumiwa hao walitoroka kwani hawakutokea Julai 23, 2011 wakati Jaji Msuya anafuta kesi hiyo akisema kwamba kulikuwa na kasoro upande wa mashtaka.
Mara baada ya upande wa Serikali kukata rufaa, kesi hiyo ilirudi tena mwaka jana na kusikilizwa kuanzia Agosti 4 hadi Agosti 8, ambako ilitolewa hukumu.
Mahakama ilimtia hatiani Fred Chonde na kumhukumu kifungo cha miaka 20 jela na kulipa faini ya Sh bilioni 15.6 huku ikimwachia huru Zuberi Mbwana aliyejitetea akisema kwamba alikwenda kwa Chonde kumsabahi hivyo hahusiki.
Pamoja na utetezi huo ulioacha watu midomo wazi kwenye maelezo ya awali ya mashtaka ilielezwa mahakamani kwamba watuhumiwa walikutwa na mifuko ya kilo moja na kujazwa kwenye “pipi” zilizopimwa kwenye uzito mdogo ya gramu 10 kila mmoja. Watuhumiwa hao walikamatwa kwenye nyumba ya Diana Jacob Namfua.
“Hivi kilo 179 zingeharibu vijana wangapi wa Tanzania kiasi kwamba kuna adhabu zinatolewa na kutiwa shaka. Wageni wanakuja kuharibu Watanzania. Sijui kama Rais John Magufuli analijua hili,” anasema mmoja wa mashahidi.