bomoa-559x520Kama tujuavyo, Tanzania imepata Rais mchapakazi. Ni Dk. John Pombe Magufuli.

Kupata Rais mchapakazi hapana shaka ni baraka. Lakini inaweza ikawa ni laana. Kwa vipi?

Tuna viongozi tunaoendelea nao tangu Serikali ya Awamu ya Nne. Wengi wao hawakuwa wachapakazi. Walikuwa mizigo kwa Taifa. Leo bila ya shaka mbele ya Rais mchapakazi watapenda nao waonekane kuwa ni wachapakazi. Kwa hiyo watafanya mambo ya kuwanyanyasa na kuwaweka roho juu wananchi ili wao waonekane kwamba nao wamo; kwamba wanakwenda na wakati.

Kwa vyovyote vile, Rais Magufuli asingependa kuonekana mbele ya wananchi kwamba ni mbaya wao kiasi cha wale waliomchagua kujuta kwa nini walimchagua. Kwa maneno mengine, viongozi wanatakiwa wawe waangalifu katika utendaji wao wa kazi. Wasilinde nafasi zao za kazi kwa kufanya mambo yanayomharibia sifa yake Rais mbele ya wananchi. 

Tuna hili jambo la bomoabomoa. Tujadiliane kama jambo hili lina umuhimu wowote pia kama lina uhalali.

Kwa upande wa umuhimu wa tendo la bomoabomoa bila ya shaka lina umuhimu wake. Serikali inayoheshimu haki haiwezi kubomoa nyumba za raia wake bila sababu. Jambo hili lina sababu.

Serikali haibomoi nyumba holela. Inabomoa nyumba zilizojengwa kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kujengwa. Bomoabomoa inakumba maeneo ambayo yamekatazwa kujengwa kwa sababu, ama ni eneo hatarishi kama mabondeni, au ni chanzo cha maji, au ni eneo lililotengwa kwa sababu maalumu na watu wamelivamia, au ni kando kabisa ya barabara.

Kama watu wamejenga maeneo hayo, hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kuilaumu Serikali ikiamua kuwabomolea. Basi, bomoabomoa hii ina umuhimu wake na ina sababu zake maalumu. Inawaepusha wananchi wasichukuliwe na maji na inalinda mazingira. Lakini pamoja na ukweli huo wote tujadili uhalali wa kufanyika tendo hili.

Ukweli ni kwamba hili linaloendeshwa kibabe na kinyama halina uhalali wowote wa kufanyika pamoja na umuhimu uliopo wa kulinda maisha ya wananchi na kulinda mazingira. Jambo hili limeanzishwa kwa pupa bila kufuata utaratibu. Linaendeshwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na linalenga watu waliojenga kinyume cha sheria.

Kihistoria, NEMC ilianzishwa zaidi ya miaka ishirini iliyopita. Lakini katika muda wote huo NEMC imekuwa ikifanya kazi ofisini. Haikuwahi kwenda mitaani wala vijijini kuwaelimisha wananchi juu ya shughuli zake na wajibu wa wananchi kushiriki katika utunzaji wa mazingira. Imeibuka ghafla kwenda mitaani kuweka alama za X nyumba za wananchi na kuwataka wazibomoe mara moja.

NEMC ipo lakini mazingira ya Tanzania nzima yamekuwa machafu mpaka Desemba 9 mwaka jana, wananchi waliposhiriki kusafisha mazingira ya maeneo yao. Ni kwa uongozi wa Rais Magufuli si kwa maelekezo ya NEMC.

Ni muhimu pia kuzingatia kwamba wananchi walijenga katika maeneo hayo kabla haijatungwa sheria inayodaiwa kuwa wameivunja. Kwa hiyo, hawakuvunja sheria kujenga maeneo hayo. Kilichotakiwa ni NEMC kutambua kuwa wananchi walijenga maeneo hayo kabla haijatungwa sheria inayozuia kujenga maeneo hayo. Kwa hiyo wasingechukuliwa kuwa ni wahalifu moja kwa moja.

Ilibidi NEMC iende mitaani na vijijini kukaa na wananchi kwamba hawakuvunja sheria kwa kujenga maeneo waliyojenga kwa kuwa hapakuwa na sheria iliyowazuia kufanya hivyo. Lakini sasa kuna sheria. Kwa hiyo, NEMC ingepanga na wananchi wahame lini na wahamie wapi. Hilo halikufanyika kwa makosa ya NEMC. 

Halafu NEMC inawafanyia wananchi mambo ya kinyama kana kwamba wana makosa kuishi maeneo hayo. Hawana makosa kuishi maeneo hayo kwa sababu hapakuwa na sheria iliyowazuia kujenga maeneo hayo.

Na hata kama wananchi wamejenga maeneo hayo baada ya kutungwa sheria ya kuzuia ujenzi maeneo hayo, NEMC ilikuwa wapi? Haikuwaona wananchi walipokuwa wakianza kujenga wakawazuia? Ni vyema Rais Magufuli akaliona na kutambua kwamba katika jambo hili la bomoabomoa wananchi wameonewa na kunyanyaswa.

Hakuna anayeweza kuwahurumia wakazi wa Jangwani pale kando ya Barabara ya Morogoro. Hawa wangeweza kupata hata siku moja kuhama. Hili si jambo geni kwao.

Lakini ubinadamu uko wapi? Watu wanapewa robo saa kuhama mahali walipoishi zaidi ya miaka ishirini. Tena wanaopewa robo saa hiyo ni akina mama kwa sababu waume zao wapo kazini. Ni Serikali gani hiyo ya wananchi isiyofikiria wananchi?

Halafu NEMC inakwenda na polisi kutia alama  za X nyumba za wananchi ambao wamekaa maeneo yao zaidi ya miaka hamsini na hawajaambiwa kuwa wamefanya makosa kuendelea kuishi maeneo hayo. Unawapa watu maskini majuma mawili kuhama maeneo yao. Familia nyingine ni za wajane tu wasio na mbele wala nyuma. Unasema wana makosa na lazima wahame na huwaoneshi wahamie wapi wala kiwanja! Wana makosa gani? Na kama walijenga baada ya kutungwa sheria NEMC hawakuwa wanawaona? NEMC ni wazembe?

Inatisha. Kila mahali roho za wananchi ziko juu. Hawana fedha za kununua viwanja vya kujenga nyumba. Nyumba zao zinabomolewa kama mchezo na bila huruma. Haya ni maafa ya Taifa. Watu 32 wamepoteza maisha kwa mshtuko wa kubomolewa nyumba zao.

Tufike mahali Serikali ione kwamba NEMC imefanya kaazi hiyo kinyama. Serikali isitishe kazi hii na iwachukulie hatua kali watu wa NEMC kwa kunyanyasa wananchi bila kuwaelimisha.

Kwa bahati mbaya sana CCM na Serikali yake hawajatambua kuwa wananchi wamechoka kuwa wavumilivu. Na hili ni jambo la hatari. Huwezi kuwabomolea watu nyumba zao na kuwaona kwamba ni wahalifu wakati walijenga kabla haijatungwa sheria ya kuzuia kujenga maeneo hayo.

Serikali ya wananchi ikae na wananchi ijadiliane nao kifanyike nini kwa kuwa sasa kuna sheria inayowazuia kuendelea kuishi maeneo hayo. Si suala la kutekeleza kinyama jambo hili kwa kutumia polisi. Kwa kweli polisi wa Tanzania wanatumiwa vibaya. Nani anabisha?