Novemba mwaka jana Watanzania walitaarifiwa kuwa Marekani inakusudia kuzuia “misaada” yake kutokana na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 Visiwani Zanzibar, pamoja na kukamatwa kwa wanaharakati waliokuwa wakikusanya habari za uchaguzi jijini Dar es Salaam.
Tukaonywa kuwa matokeo yake ni kukosa dola takriban milioni 473 kutoka Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC). Onyo hilo la MCC lilikuwa katika barua ya Novemba 19, aliyopelekewa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, ikisema Tanzania haitapata msaada kutoka shirika hilo kama ilivyotarajiwa kwa ajili ya mwaka 2016.
Kinachonishangaza ni kuwa tangu Mei mwaka jana tayari Marekani ilitangaza nia yake ya kuzuia msaada wa MCC. Wakati huo uchaguzi bado na wala Jecha hatumwelewi ni nani. Kisha bodi ya MCC ikachukua uamuzi huo Septemba.
Sababu waliyotoa ni kuwa Tanzania ilikuwa haijachukua hatua thabiti kuzuia rushwa na ufisadi. Wakati huo kashfa kubwa ilikuwa ikivuma; nayo ni ile akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu (BoT). Ilisababisha mawaziri wawili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, kulazimika/shwa kujiuzulu. Vigogo kadha wakafikishwa mahakamani na wengine kupelekwa mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.
Lakini pia baadhi ya vigogo kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliohusika na hizi “senti za mboga” wakapitishwa na chama hicho kugombea nafasi kadhaa za uongozi, ikiwamo ubunge. Leo wako pale mjengoni wanaitwa waheshimiwa.
Yaani inaonekana MCC ilichukua uamuzi wa kuzuia misaada kabla ya uchaguzi. Baada ya uchaguzi ikaongeza sababu ya Zanzibar. Ndipo MCC ikaiandikia Serikali ya Tanzania katikati ya Novemba na kusema kuwa sharti moja la kutoa misaada ni kuwa nchi inayofadhiliwa ni lazima ifuate kanuni za demokrasia na utawala bora.
Si lengo langu kwa sasa kuingia undani wa sababu zilizoifanya Marekani izuie hiyo ‘misaada’ yake kwa Tanzania. Badala yake ningependa kuzungumzia kwa mapana ‘misaada’ inayotolewa na Marekani pamoja na nchi nyingine za Magharibi. Lengo ni kuona iwapo kweli tunafaidika na hizo sadaka wanazotugawia.
Kwani ni dhahiri kuwa kile wanachokiita misaada hutumiwa kama silaha ya kutufanya tutekeleze matwaka ya wakubwa. Si hili sulala la MCC tu, bali mara nyingi siku za nyuma tumewahi kutishwa kuwa tutakosa misaada iwapo hatukufanya hili au lile. Na mara nyingi masharti haya wao huyaita utawala bora. Ni pamoja kutulazimisha tufungue milango ya biashara na kuruhusu bidhaa hata maji ya kunywa kutoka Ulaya. Au hutulazimisha tukubali wawekezaji kutoka huko kwao, hata kama ni kinyume na maslahi ya taifa letu.
Hii ni ishara kuwa nchi yetu ni tegemezi, siyo tu kiuchumi bali hata kisiasa. Miaka nenda miaka rudi serikali zetu zimekuwa zikikimbilia Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wakiomba misaada. Na kila mwaka waziri wetu wa fedha anatakiwa afike Paris ili kutoa ripoti jinsi anavyotumia fedha.
Alimradi ni aibu tupu kwa serikali zetu kuwanyenyekea ‘wafadhili’ na kuwapa ripoti. Hawajui wanawajibika kwa nani, kwa wananchi wa Tanzania au kwa mataifa mababe. Ndio maana hata huyu waziri wa fedha aliyeapishwa majuzi, Dk. Philip Mpango, aliungama akisema ni aibu kutegemea wahisani, Akaongeza: “Inabidi tupambane tuache kuendelea kutegemea misaada. Mimi nilikuwa naongozana na mawaziri walionitangulia wakati wa kuomba misaada. Si kitu kizuri kabisa, kwa kweli inakera.”
Hii ndio maana ya nchi tegemezi. Lakini ni vizuri tukaangalia suala hili kwa mapana na kuona ni nani hasa anayefaidika kutokana na hiyo misaada yao.
Marekani ina Shirika lake la Misaada ya Kimaendeleo (USAID) ambalo lina miradi katika nchi zaidi ya 100. Huko Amerika ya Kusini baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Paraguay mwaka 2012, uamuzi ulichukuliwa na nchi za Bolivia, Cuba, Ecuador, Dominica, Nicaragua, na Venezuela kuifukuza USAID kutoka nchini mwao kwa sababu ilikuwa ikiingilia mambo yao ya ndani. Wakati huo huo Rusia pia iliituhumu USAID kuwa ilikuwa inaingilia mambo ya ndani.
Kilichofanyika ni kuwa USAID ilijiingiza nchini Russi mara tu baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti (USSR). Mara moja ikaanza kuingilia siasa ya Rusia na katika muda wa miaka 20 ilitumia dola bilioni 2.6. Mwaka 2012 peke yake ilimimina dola milioni 50. Sehemu kubwa ya fedha hizi zilitumika katika kile wanachokiita ‘kuendeleza demokrasia’.
Pia kuna mfano wa Indonesia ambako serikali iliwafukuza wakulima wadogo kutoka mashamba yao ili kuruhusu mradi wa umwagiliaji uliofadhliwa na Marekani. Halafu nchini Mali, Misri na Haiti wakulima walikuta bei ya mazao yao ikianguka kutokana na misaada ya chakula kutoka Marekani.
Nchini Misri, USAID ilitoa msaada wa ngano iliyozalishwa Marekani kwa ruzuku ya serikali. Misri ni nchi iliyokuwa inajitosheleza daima kwa ngano yake. Lakini kutokana na kuingiza ngano ya bei rahisi kutoka Marekani wakulima wa ngano nchini Misri walifilisika na wakaachana kabisa na zao hilo. Leo nchi hiyo inanunua ngano zaidi ya tani milioni 10 kutoka nje, asilimia 40 kutoka Marekani. Hivi ndivyo USAID ilivyoua kilimo cha ngano nchini Misri na wakati huo huo ikajitengenezea soko la ngano yake.
Kwa kila dola ambayo Marekani imetoa kwa Misri, tayari Misri imetumia dola 40 kuagiza ngano ya Marekani. Haya ni matokeo ya ‘msaada’ wa kigeni.
Kuhusu Afrika, inakisiwa kuwa Bara hili linapokea misaada yenye thamani ya dola zaidi ya bilioni 50 kila mwaka. Swali la kujiuliza ni iwapo misaada hii imeleta mendeleo. Jibu lake ni kuwa pato la wastani la mwananchi wa Afrika leo hii limeanguka likifananishwa na miaka ya 1970. Yaani watu milioni zaidi ya 350 wanaishi kwa pato la chini ya dola moja kwa siku, na idadi hii inazidi kuongezeka.
Mnamo miaka ya 1990 wafadhili walidai kuwa wanatufutia madeni yetu. Hicho ni kiini macho, kwani Afrika leo hii inalipa karibu dola bilioni 20 kila mwaka kutokana na madeni na riba. Yaani tunachofanya ni kuongeza madeni ili kulipa madeni na riba. Halafu wanasema eti wametufutia madeni!
Ukweli huu unakubaliwa hata na wao wenyewe. Mwaka 2005 wakati nchi tajiri (G8) zilipozungumzia uchumi wa Afrika, IMF liliwaonya wafadhili hao kuwa misaada yao haitasaidia kuboresha uchumi wa Afrika. Ripoti ya IMF iliyoitwa “misaada haitanyanyua uchumi wa Afrika” (Aid Will Not Lift Growth in Africa) ilishauri kuwa ni vizuri bara hili likaachana na misaada kutoka nje.
Kuna wanaosema kuwa misaada huwa inaliwa na wajanja wachache barani Afrika. Ni kweli kuwa tungali tunao watawala wezi kama walivyokuwa kina Mobutu Sese Seko wa iliyokuwa Zaire na Jean-Bédel Bokassa wa Afrika ya Kati. Hata Umoja wa Afrika (AU) ulisema mnamo mwaka 2002 kuwa takriban dola bilioni 150 zinaliwa kama rushwa kila mwaka.
Lakini ni nani wa kulaumiwa? Mei 2004 Profesa Jeffrey Winters wa Chuo Kikuu cha Northwestern (USA) aliwaambia wabunge wa Marekani kuwa WB inawajibika moja kwa moja na rushwa ya dola bilioni 100 iliyotokana na mikopo yake kwa nchi changa. Kina Mobutu na Bokassa wasingefanikiwa bila ya kubebwa na wafadhili.
Nchi ya Congo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilikuwa ikiitwa Zaire wakati ikitawaliwa na Mobutu. Yeye alikuwa akimiminiwa misaada kiasi kwamba IMF lilimteua Irwin Blumenthal kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Zaire. Mwaka 1978 Gavana huyu aliionya IMF kuwa Mobutu na wapambe wake walikuwa wezi wakubwa na kwa hivyo hakuna uwezekano wa wakopeshaji kurudishiwa fedha zao. Hata hivyo IMF iliendelea kumpa Mobutu mikopo zaidi kushinda nchi zote za Kiafrika.
Huyu ndiye Mobutu ambaye kuanzia mwaka 1965 hadi mwaka 1997 alipopinduliwa alikuwa tayari ameiibia Zaire takriban dola bilioni tano. Hizo ni fedha za mikopo ambazo leo zinalipwa na DRC! Hivi ndivyo wafadhili eti wanaisaidia Afrika!
Na huko Malawi aliyekuwa Rais Bakili Muluzi alishitakiwa kwa kuiba fedha za misaada dola milioni 12. Na nchini Zambia aliyekuwa Rais Frederick Chiluba mwaka 1991 hadi 2001 alikuwa akisifiwa sana na wafadhili kwa ‘utawala bora’. Mwishowe akashitakiwa kwa kuiba mamilioni ya dola zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya afya, elimu na miundombinu. Wakati anaingiza fedha hizi katika akaunti yake huko Ulaya wafadhili waliendelea kummiminia misaada.
Asasi za kiraia (NGOs) kutoka Afrika na Uingereza zimefanya utafiti wa pamoja na kutoa ripoti (Honest Accounts: The True Story of Africa’s Billion Dollar Losses) ambayo inaonyesha jinsi bara letu linavyoporwa fedha nyingi kushinda hiyo misaada tunayopokea.
Ripoti hiyo inasema Afrika inapokea dola bilioni 134 kila mwaka kwa njia ya mikopo, zawadi na uwekezaji. Lakini wakati huo huo hao watoaji misaada hiyo wanakwapua dola bilioni 193 kwa njia kadha kama vile ulipaji wa mikopo na riba, ukwepaji wa kodi na usafirishaji wa faida. Kwa maneno mengine bara hili linapata hasara ya dola bilioni 59. Halafu wanatuambia eti wanatupa misaada ya maendeleo!
Moja ya asasi iliyohusika na ripoti hii ni Health Poverty Action. Mkurugenzi wake, Martin Drewry anasema: “Tunaelezwa kuwa nchi kama Uingereza huwa zinatoa ‘misaada’ kutokana na ubinadamu. Utafiti wetu umedhihirisha kuwa huu ni udanganyifu. Ukweli ni kuwa nchi tajiri ndizo hufaidika, na Afrika hupata hasara kutokana na hiyo misaada”
Watafiti hawa wanelewa wasemalo, kwani wamegundua kuwa kila mwaka bara letu linapoteza dola bilioni 17 kutokana na usafirishaji haramu wa magogo. Pia tunapoteza dola bilioni 1.3 kila mwaka kutokana na uvuvi haramu katika bahari za Afrika Magharibi peke yake. Fedha hizi zinakwenda kwa hao wanaodai kuwa wanatufadhili.
Halafu serikali zetu zinawapigia magoti na kuwaomba wasiache kutusaidia. Eti wanatuambia bila ya kukimbilia Washington kuomba hizo fedha za MCC tutakufa njaa.
Waziri wetu wa Fedha amesema hii ni aibu. Sasa tuone ana mpango gani na atasema nini atakapohudhuria hiyo mikutano ya IMF, WB na Paris Club.
0713 562181