*Pinda asema yeye ndiye Mwalimu Mkuu wa Taifa letu
*Afa akidai malipo ya kiinua mgongo, fedha za usafiri
*Serikali yaahidi kuendelea kumtunza mjane wake
Si hivyo tu, bali ni yeye anayetajwa kama kiini cha kumjenga Mwalimu kiimani. Alimshawishi ashiriki mafunzo ya ukristo wa dhehebu la Katoliki hadi kubatizwa. Kadhalika, anatajwa kama mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa wa kumwezesha Mwalimu kufunga ndoa na Mwalimu Maria Gabriel (Mama Maria).
Mara kadhaa Mwalimu Irenge amekiri kwamba ingawa yeye alikuwa mwalimu wa mwanafunzi Kambarage, bado aliweza kufunzwa mengi na mwanafunzi wake huyo wakati wakiwa Shule ya Msingi Mwisenge, na hata baada ya Mwalimu Nyerere kuingia katika siasa. Mwalimu Irenge amefariki dunia akiwa anamsifu mno mwanafunzi wake huyo kwa uwezo mkubwa aliokuwa nao ndani na nje ya darasa, kiasi cha kumfanya arushwe baadhi ya madarasa. Mwishoni mwa Julai, mwaka huu, Mwalimu Irenge alifariki dunia akiwa na umri wa karibu karne moja na robo.
Msiba wake uliwavuta watu wengi wa mjini Musoma, Zanaki na sehemu mbalimbali nchini. Alizikwa kwa heshima kubwa kama mmoja wa watu maarufu waliotoa mchango muhimu katika ujenzi wa Taifa letu. Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliongoza mazishi ya mwalimu huyo yaliyoanzia nyumbani kwake Mtaa wa Mkinyerero, Musoma mjini na kuhitimishwa katika shamba lake lililopo Kijiji cha Busegwe-Nyanza wilayani Butiama.
Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Stephen Wassira, Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa, wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Mara, Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere, Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, Mbunge wa zamani wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo, madiwani, wakurugenzi, maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa madhehebu, wakuu wa taasisi mbalimbali na mamia ya wananchi, waliuhudhuria mazishi hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Mara
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Tupa, akimkaribisha Waziri Mkuu alisema; “Nilipopata taarifa rasmi ya kufariki dunia kwa Mwalimu James Irenge, na kwa kutambua jinsi wewe mwenyewe Mheshimiwa Waziri Mkuu ulivyojiweka karibu sana na Mzee Irenge, sikuchelewa kukupa taarifa. Pia sikuchelewa kuwaunganisha wenzangu na kushirikiana na wafiwa na waombolezaji wengine ili kuhakikisha mzee wetu tunamzika vizuri na kwa heshima.
“Kuna kazi kubwa sana imefanywa na wakuu wa wilaya, hasa hawa wa wilaya hizi mbili za Musoma na Butiama pamoja na waheshimiwa wabunge kama walivyotajwa hapa, na zaidi ya wote Mheshimiwa Mkono ambaye huko tutakakokwenda (eneo la mazishi) kwa kweli aliungana nasi kufanya mambo makubwa kama kiongozi, lakini kama mtu aliyeguswa na msiba huu.
“Nilipokuarifu mheshimiwa Waziri Mkuu, nakumbuka uliyasema maneno yafuatayo, naomba niyanukuu hapa, ulisema, ‘Loo! Mzee Irenge amefariki! Huyu ni mzee wangu, ni babu na rafiki yangu. Nitampa taarifa Mheshimiwa Rais na nitakuja kwenye mazishi yake’.” Mwisho wa kunukuu. Na kweli leo upo hapa wewe pamoja na Mama Tunu Pinda.
“Tunawashukuru kwamba mmefika na tunawakaribisheni sana kwani kuwapo kwenu kumeongeza uzito wa mazishi ya Mzee James Irenge na kumehitimisha vizuri historia ya maisha yake hapa duniani. Kwa nafasi hii basi, nakuomba upate nafasi walau utoe salamu kidogo mheshimiwa Waziri Mkuu karibu.”
Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Pinda alianza kwa kuwashukuru waombolezaji kwa ibada murua ya kumsindikiza Mwalimu Irenge.
“Nawashukurini kwa ibada hii ya kumsindikiza kwenye maisha ambayo kila mmoja lazima aende. Kwa kweli nawashukuruni sana. Mmempa heshima kubwa. Nataka nianze kwa kumpa pole sana mama, kuwapa pole watoto wake wote, wanafamilia kwa jumla, lakini kubwa nadhani kwa wana-Mara wote kwa sababu mzee huyu si maarufu tu bali pia ni mmoja wa wazee ambao ‘hawavumi lakini wamo’. Inawezekana wengi wasijue thamani yake lakini kwa wengine tunaomjua kidogo, tunajua thamani ya Mzee James ni nini.
“Mtakuwa mmeona kwenye maelezo ya maisha yake, mzee huyu ndiye aliyemfundisha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipokuwa shule ya msingi. Na kwa kweli alikaa kwake. Kwa hiyo Mzee Irenge ni mwalimu… mwalimu mkubwa sana wa Mwalimu mnayemjua ninyi kama Baba wa Taifa. Kwa kweli huyu ndiye Mwalimu Mkuu wa Taifa hili kwa sababu amemjengea misingi Baba wa Taifa ambayo baadaye imemfanya kuwa ndiyo kiongozi wetu, kiongozi mzuri, mpendwa, mwadilifu, mchapakazi na mtu wa Mungu.
“Mimi naamini kwa namna moja au nyingine, mzee James, atakuwa definitely (bila shaka) amepanda mbegu zake pale ambazo zimemfanya Mwalimu kuwa alivyo. Kwa hiyo ni kweli kabisa nilipopata taarifa hii Jumamosi, nikakumbuka…kwa sababu nilikuwapo hapa mwezi wa kumi nilikuja ziara Mkoa wa Mara, na nilipata nafasi ya kuonana naye. Mimi kwangu hii ni kama inanikumbusha mambo fulani, na mimi nimesoma Mara hapa sekondari (Mara Sekondari), lakini wakati huo sikujua habari ya Mwalimu James Irenge hata kidogo…mwaka 1960 na 1970.
“Nikaanza kazi Mwanza kama wakili wa Serikali na nikawa nakuja hapa kuendesha kesi za mauaji kama wakili wa Serikali mwaka 1975, 1976 na 1977. Sikuwa namjua Mwalimu James Irenge. Ikatokea tu mwaka 1978 nikaombwa niende Ikulu kama mmoja wa wasaidizi wa Baba wa Taifa. Mwaka 1978, 1979, 1980, 1981 ila kwa kweli sikujua huyu babu ni nani pamoja na kuja kuja yangu Butiama na Baba wa Taifa, nilikuwa nasikia tu Mwalimu Irenge…Mwalimu Irenge.
“Lakini baada ya pale nikaja nikabahatika kumwona kwa sababu alikuwa anamtembelea Mwalimu kama mwalimu wake, alikuwa anakuja kuja siku nyingine pale Butiama katika kipindi hicho wakati akiwa bado na nguvu na ndiyo nikajua huyu ndiye aliyemfundisha Baba wa Taifa. Ndiyo maana siku ile nikasema huyu ni babu yangu, lakini rafiki yangu vilevile. Kwa hiyo, niliona ni vizuri kwa niaba ya Serikali nije niungane nanyi, na nilipomwarifu Rais na leo asubuhi nimemuaga, anawapeni pole sana, sana tu. Naamini siku akipata nafasi ya kuja Musoma atakuja kumwona bibi hapa na kumpa pole pamoja na watoto. Kwa kweli tunawapeni pole nyingi sana.
“Nilipokuja mara ya mwisho nilipomwona, ni kweli alinieleza juu ya tatizo la kijana wake (Nassoro Irenge aliyekuwa kizuizini nchini Mauritius). Mwenyezi Mungu amesaidia kijana amerudi tuko naye, matumaini yangu ni kwamba naye atakuwa ni sehemu yetu asaidie Taifa hili na familia hii. Lakini ni kweli vilevile aliniambia siku ile kwamba anapata tabu kidogo maisha magumu. Nikamwambia mzee na mimi ndugu yako, kijana wako tabu na mimi, lakini acha nitajitahidi. Kwa hiyo nilimwahidi kila mwezi nitakuletea vilaki tatu hivi vikusaidie.
“Kwa hiyo tutaendelea maana bado bibi yupo kwa hiyo lazima tuendelee kusaidia familia kwa kiwango ambacho tutaweza, lakini tulikuwa tunamsaidia yeye na vilevile familia yake. Kwa hiyo ukomo wangu uwaziri mkuu wangu ukiisha mambo yanaweza kuniwia vigumu kidogo…sasa na familia hilo mlielewe, mkiona kimya mjue ule mwenge umezima. Lakini kwa sasa tutajitahidi kwa sababu ilikuwa ni dhamira yangu kuendelea kumsaidia rafiki yangu huyu, sasa Mwenyezi Mungu amefika mahali ameona ni wakati wake kumpenda, lakini bado ana familia kwa hiyo lazima tuendelee kuisaidia.
“Kwa hiyo bibi sisi wenzako tutaendelea kukupa moyo, kukutia moyo, mimi na wajukuu na watoto. Kubwa tu msikate tamaa na dunia. Kuondoka kwa Mzee James si mwisho wa kila kitu. Bado tupo, unao marafiki, unao majirani, kwa hiyo jipe moyo, jipe nguvu, naamini Mwenyezi Mungu atakubariki utaweza kuhimili yote yaliyokupata.
“Nimalizie kwa kuwashukuru sana wazee wangu, Mzee Wasira na Mzee Mkono, wabunge wenzangu wanaotoka mkoa huu. Nimshukuru sana ndugu yangu Vincent Nyerere – mbunge mwenzangu na rafiki yangu sana, pengine tunaparuana kama mnavyojua Bunge lile kali kidogo lakini tukitoka tunaheshimiana.
Nimeshukuru sana kwamba wote wamekuja kumzika Mzee James Irenge, nataka niwahakikishieni kwamba ni kwa niaba ya wabunge wote wa Mkoa wa Mara kwa sababu wasingeweza wote kuja kwa sababu ya purukushani za bungeni bado tunaendelea na bajeti. Nawashukuru sana wazee kwa kazi hii nzuri ambayo leo tunahitimisha pamoja.
“Niliona katika kumalizia niseme tu kwamba na mimi kama kijana wake Mzee James, basi nitamkabidhi kijana wake mkubwa pale kaubani kadogo nilikokuja nako kaendelee kusaidia familia kwa kadri inavyowezekana. Baba Askofu na wachungaji pamoja na watumishi wote wa Mungu mliopata nafasi ya kutusaidia narejea kuwashukuruni sana sana.
Hii ni baraka ya pekee, ni tofauti kabisa pengine na wengine tunapokuja kuzikwa. Ninyi mmembariki, mmemsaidia kumwombea. Imani yangu ni kwamba Mwenyezi Mungu atamsamehe dhambi zake zote aweze kumpokea huko mbinguni ambako ndiko makazi ya kudumu. Nawashukuruni sana, Tumsifu Yesu Kristo, Bwana Asifiwe, nawatakia shughuli njema. Asanteni sana.”
Wasifu wa Mwalimu James Irenge
Mwalimu James Zangara Irenge alizaliwa katika Kijiji cha Busegwe-Nyanza, Musoma Vijijini mwaka 1892. Taarifa hii ni kwa mujibu wa maelezo yake mwenyewe wakati akiwa hai. Kabla ya kifo chake alitamka kuwa ana umri wa miaka 120.
Elimu
Kuanzia mwaka 1924-1925 alisoma Busegwe ambayo kwa sasa ni chekechea. Mwaka 1927 alisoma darasa la pili Mwisenge. Alijiunga na Chuo cha Ualimu Mpwapwa, Dodoma mwaka 1932. Mwaka 1934 alianza kufundisha Chuo cha Ualimu Mpwapwa. Mwaka 1935 alihamia Shule ya Msingi Mwisenge na ndipo alipomfundisha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Alimfundisha darasa la tatu na la nne akiwa anaishi naye nyumbani kwake Mtaa wa Mkinyerero, Mwisenge, Musoma Mjini.
Mwaka 1938 alipelekwa kufungua shule mbalimbali za msingi North Mara (kwa sasa wilaya za Rorya na Tarime). Mwaka 1939 alihudhuria kozi fupi ya ukaguzi wa shule za msingi nchini Kenya. Mwaka 1940-1941 alikuwa Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Kinesi.
Mwaka 1941-1944 alikuwa Mkaguzi wa Shule za Serikali Jimbo la Kanda ya Ziwa. Mwaka 1945-1946 akawa Mkuu wa Mafunzo ya Walimu Shinyanga. Mwaka 1947-1954 akawa Mkaguzi wa Shule za Serikali na Mashirika ya Umma Kanda ya Ziwa. Mwaka 1955 alirejea kufundisha Chuo cha Ualimu Mpwapwa.
Mwaka 1956-1958 akawa Mkaguzi wa Shule za Serikali na Mashirika ya Umma Shinyanga. Mwaka 1959 akawa Mwalimu Mkuu Shule ya Kati ya Nyakabongo, Mwanza. Mwaka 1960-1963 akawa Mkaguzi wa Shule za Msingi Geita na Biharamulo. Mwaka 1964-1969 akawa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Pule, Geita. Mwaka 1977 alijiunga katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupewa kadi namba TFG 636751.
Alioa mke wa kwanza na kuishi naye miaka 22 bila kuzaa mtoto, ndipo mkewe huyo aliporidhia Mwalimu James Irenge aoe mke mwingine. Alioa mke wa pili, Nyang’ama mwaka 1951 aliyebahatika kupata watoto wawili. Mwaka 1952 alioa Josephine Matuba ambaye alibahatika kupata watoto 11. Walio hai hadi sasa ni wanane. Alihalalisha ndoa yake Julai 2, 1997, katika Kanisa Anglikana, Musoma Mjini. Mwalimu Irenge alikuwa mmoja wa waasisi wa kanisa hilo katika Mkoa wa Mara. Waasisi wengine ni marehemu Zephania Owoli na Charles Nyongo.
Kustaafu
Alistaafu utumishi wa umma mwaka 1970 akiwa Geita, Mwanza. Baadaye Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alimshauri aanzishe Kijiji cha Ujamaa. Alianzisha Kijiji cha Ujamaa cha Ihaya Buyaga, Geita mkoani Mwanza. Alirejea nyumbani kwake Mwisenge mwaka 1980. Ameacha mjane na watoto hai 10, wajukuu 35, vitukuu wanne na vilembwe wawili. Alifariki dunia akiwa nyumbani kwake Mtaa wa Mkinyerero, Shina Namba 9 Musoma Mjini. Alifariki dunia Julai 21, 2012 saa nne usiku.
Madai yake hadi anafariki dunia
Hadi anafariki dunia, Mwalimu Irenge alikuwa akidai malipo ya kiinua mgongo na malipo ya usafiri kutoka Geita hadi nyumbani kwake, Musoma. Familia yake imempa kazi hiyo Mbunge Vincent ili kuhakikisha Serikali inawalipa madai hayo.