Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imelipa kiasi cha shilingi milioni 40 ikiwa ni kifuta jasho/machozi kwa wananchi 198 wa Vijiji vya Chemchem, Tungufu, Tampori, Mulua na Iyoli wilayani Kondoa kutokana na kupata madhara yaliyosababishwa na wanyamapori.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Kondoa Mjini ,Ally Juma Makoa aliyetaka kujua wananchi walioharibiwa mazao yao na tembo na kuhakikiwa watalipwa lini kifuta jasho/machozi.
Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii ilifanya uhakiki wa madai ya kifuta jasho/machozi tarehe 25 hadi 28 Septemba,2022 kwa wananchi 274 wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa walioharibiwa mazao yao na tembo lakini baada ya uhakiki wananchi 198 ndio waliolipwa.
Aidha, amesema Wizara inaendelea kufanyia kazi malipo ya kifuta jasho/machozi ya wananchi waliowasilisha madai mapya.