Seif_hamad(17)Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, ametajwa kuwanyima usingizi viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Taarifa ambazo gazeti hili imezipata zinasema Maalif Seif ambaye ni Makamu Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), amekuwa na msimamo unaotokana na chama chake kinachong’ang’ania hoja kutangazwa matokeo badala ya kurudia uchaguzi wa Zanzibar.

Kutokana na hali hiyo, Maalim Seif, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, amekutana na viongozi wasiopungua saba wa CCM kuzungumzia uchaguzi huo na uamuzi uliochukuliwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

“Sawa, mazungumzo yanaendelea. Watu wasimsikie mtu yeyote na wasubiri tamko hapo baadaye, lakini kubwa tunataka matokeo yatangazwe,” anasema Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya CUF, Ismail Jussa Ladhu.

Ladhu anasema katika vikao vyote vilivyofanyika mwishoni mwa mwaka jana kwa nyakati tofauti, vikimhusisha Maalim Seif, yeye amekuwa akitoa nyaraka za matokeo halisi baada ya kukusanywa kwenye vituo na majimbo.

Ladhu hakutaka kufafanua zaidi, ila mmoja wa viongozi wa CUF wa makao makuu ya chama hicho yaliyopo Buguruni, anasema: “Maalim Seif kawashika maana yeye anachokifanya ni kuwaonesha ushahidi wa matokeo ambayo yeye Maalim anaona kuwa ni halisi, ndiyo maana vikao hivi vinakwenda na kuahirishwa kila wakati, ila mwisho upo. Tusubiri.”

Anasema ofisi zote kuu za Dar es Salaam na Zanzibar wamemwagiza Maalim Seif kutogeuka nyaraka zake na kama itatokea hivyo awe na jibu thabiti la kuwaambia wapiga kura wa Zanzibar hususani wana-CUF, Tanzania nzima na dunia ambayo inafuatilia kwa karibu mwenendo wa siasa za Visiwani humo.

Mchana wa Oktoba 28, mwaka jana, Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika pamoja na ule wa Muungano, Oktoba 25 kwa hoja mbalimbali ikiwamo ya Maalim Seif kujitangaza mshindi mapema kabla ya majimbo 21 kutangazwa. Wakati matokeo hayo yanafutwa, majimbo 33 yalikwisha kutangazwa.

CUF inayodai kwamba imekuwa ikiporwa ushindi na CCM tangu kurejeshwa uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, safari hii wameutangazia umma kwamba hawatakubali.

Mwishoni mwa mwaka jana Rais Magufuli na Maalim Seif walikutana katika kikao cha faragha Ikulu, Dar es Salaam.

Rais Dk. Magufuli amekuwa kiongozi wa saba kukutana na Maalim Seif kuzungumzia kuhusu mwafaka wa uchaguzi wa Zanzibar. Vigogo wengine ambao tayari wameshakaa na Maalim Seif katika vikao vya mashauriano ya mgogoro wa kisiasa Zanzibar, ni Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi.

Wengine ni Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma.

“Na nikwambie kwamba Maalim Seif hakuomba kuonana na Rais Magufuli bali kilichofanyika ni kwamba Maalim Seif ndiye aliyeitwa Ikulu kwenda kufanya mazungumzo na Rais Magufuli,” anasema mtoa habari huyo.

Anaeleza kwamba siku mbili kabla Maalim Seif haijaitwa Ikulu, aliitwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha, na alipoulizwa alikiri kwamba alitoa uamuzi huo baada ya kubanwa na hali ya mambo.

Habari zinaeleza kwamba siku hiyo Jecha aliitwa Ikulu usiku na Dk. Magufuli na alipelekewa ndege ya Serikali kufanikisha safari yake ya kwenda kufanya mazungumzo na Dk. Magufuli.

Habari za uhakika kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa kikao hicho zimeieleza JAMHURI kuwa mazungumzo yamefikia pazuri na kwamba uchaguzi hauwezi kurudiwa kwa sababu kwa hali halisi Maalim Seif amewashinda hoja CCM.

“Maalim Seif yuko so simple (kawaida tu) katika kikao chake anachoketi na vigogo hao kila wanapotoa hoja za CCM kuishinda CUF, yeye amekuwa akiwatoa jasho kwa jambo moja tu kubwa, nalo ni kuwaonesha kielelezo cha matokeo ya mwisho ya uchaguzi yaliyosainiwa na mawakala wakuu wa Dk. Shein, Mohamed Ramia Abdiwawa, ambaye alisaini kukubali matokeo yaliyoonesha Dk. Shein kapata kura ndogo ikilinganishwa na Maalim Seif na wakala wake mkuu, Nassor Ahmed Mazrui (Naibu Katibu Mkuu wa CUF) upande wa Zanzibar.  

“Haya mambo ya vikao bwana ni mambo ya siri sana…kwa sababu Maalim Seif ana watu wake confidents, very few (wasiri na wako wachache) katika mambo haya yanavyokwenda na ninapokwambia wachache pengine hawawezi kufika hata watano.

“Sasa si rahisi wewe ukampata mmoja wao akakwambia kila kitu, lakini yako mengine wanaweza kusema hili waambie lakini ni vitu vya siri sana. Mimi vingine ukiniuliza siwezi kujidanganya kuwa navijua…

“Najua wanakwenda vizuri na kufikia leo (Jumatano iliyopita) siku si nyingi jambo hili litafikia mwisho wake kwa sababu miezi miwili karibu mitatu ni muda mrefu,” anasema.

Alipobanwa zaidi juu ya mwenendo mzuri wa mazungumzo, mtoa habari huyo anasema: “Vizuri ndiyo hivyo kwamba ushindi kwa Maalim Seif upo na uchaguzi hautakuwapo…

“…Hii ni kwa sababu hoja ya uchaguzi hautakuwapo ukisikia, ooh! anayo mamlaka sijui nini ni vitu vya kutengeneza tu, mamlaka yanawekwa kwenye sheria sasa yako wapi. Wanavyovitaja wao ni vitu ambavyo havipo ni kufanya confusion (kuchanganya), ni kuyachanganya mambo,” amesema na kuongeza;

“Unajua, wanasheria wanapolumbana huko mahakamani yule ‘anasubmit’ anataja kifungu hiki na yule ‘anasubmit’ anakipinga kile anataja kingine, lakini sheria haipo ya kutotangaza matokeo.

“Kwa sababu hakuna sheria inayosema hivyo. Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1984 wala kifungu chochote haimpi mamlaka Mwenyekiti wa ZEC wala Tume yenyewe kuamua alivyofanya.

“Kwa sababu hakuna namna ambayo siku ya uchaguzi imefika halafu ukatangaze kuwa uchaguzi umeharibika, haiwezekani. 

“Uchaguzi utakuwa umeharibika Songea, unaweza kuwa umeharibika Mbinga, unaweza ukawa umeharibika Chake Chake na utakuwa umeharibika na maeneo hayo na maeneo hayo hayako juu ya Tume bali yako juu ya wasimamizi kwa mujibu wa sheria, dhamana ni msimamizi wa eneo hilo ambako wakipatikana washindi hutangazwa na wasimamizi hao na kutoa cheti kwa mujibu wa sharia,” anasema.

Anahoji: “Kabla ya Oktoba 28, Jecha hakujua kama uchaguzi uliharibika? Alikuwa hajazipata taarifa kama umeharibika? Wakati kufika tarehe 25 saa 2 usiku kura zote zilibandikwa vituoni usiku vituo vyote vilikuwa vimeshabandikwa matokeo.

“Kwa sababu amefuta matokeo tarehe 28 mchana ndiyo ukafuta uchaguzi. Zile zilikuwa mbinu za CCM kuibaka demokrasia. Yaani wewe ulishatangaza matokeo ya uchaguzi hadharani na dunia nzima ikakusikia na hayo pia yameharibika? Zile zilikuwa mbinu za utawala CCM kuibaka demokrasia,” anasema.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, ilipofika Oktoba 25, 2015 jioni walipobaini kwamba wameshindwa wakaanza kuhangaika kujaza matokeo na hiyo ndiyo iliyokuwa njia ya mwisho kwao.

Anadai kwamba CCM ilishindwa katika Uchaguzi Mkuu kwani matokeo ya mwisho ya urais yaliyosainiwa na mawakala yalionesha chama tawala kimepata kura chache dhidi ya Maalim Seif.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamekuwa wakizungumzia hali ya siasa Tanzania na kusema CCM ilishikwa vibaya, kwani miaka yote ya nyuma CUF walikuwa wakijitangazia ushindi, lakini kulikuwa na kupokwa.

Habari zinaeleza kwamba kikubwa kilichosaidia kwa mwaka huu CUF wakasimama kifua mbele, ni hatua ya kuibwa kura ambako kumekuwa tofauti na miaka mingine kwa sababu matokeo ya vituo yalibandikwa hadharani.

“Katika vikao vyote vya kujadili mwafaka huo wa uchaguzi, CCM wanajikuta kuwa hawana hoja kwani kila hoja walizoziwasilisha kikaoni zilipigwa chini

“Safari hii CCM walimwibia Maalim Seif wakashindwa kuziba mianya yote na sababu kubwa iliyosababisha hayo ni hatua ya mambo kuwekwa hadharani, kwani Maalim Seif safari hii hakutaka kufanya ajizi,” amesema mtoa taarifa mwingine.