Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Serikali imesema inakamilisha Muswada wa Sheria utakaoanzisha chombo cha kusimamia sekta ya milki (Real estate Regulatory Authority), kwa ajili ya kusimamia na kulinda maslahi ya wapangaji.
Pamoja na shughuli zingine chombo hicho kitamlazimisha mwenye nyumba kutoza kodi ya mwezi mmoja mmoja badala ya utaratibu wa sasa ambapo yeye huamua kupokea kodi ya kuanzia miezi sita hadi mwaka mmoja.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.Angelina Mabula, wakati akifungua mafunzo ya wiki moja kwa mawakala wa mali zisizohamishika.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Chuo cha Biashara (CBE) kwa wiki moja na bada ya muda yatakuwa yakifanyika kwa muda wa mwaka mmoja.
Waziri amesema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu wenye nyumba kuwalazimisha kulipa kodi ya miezi sita au mwaka mmoja hivyo sheria hiyo itasaidia kusimamia maelekezo ya Serikali.
Ameipongeza CBE kwa kuanzisha kozi hiyo aliyosema imekuja wakati mwafaka.
“Sheria hii italazimisha mwenye nyumba kupokea kodi ya mwezi mmoja mmoja lakini itaweka nafasi ya majadiliano baina ya mpangaji na mwenye nyumba na wakizungumza na kukubaliana kulipa mwaka au miezi sita kwa hiyari hiyo inaruhusiwa lakini haipaswi kuwa lazima,” amesema.
Dk.Mabula amewataka mawakala nao kuzingatia maadili ili kuifanya kazi sheria hiyo na kuwa na heshima kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika Mashariki kwani uzoefu unaonyesha kwamba madalali wengi wamekuwa wakifanya kazi hiyo kiholela.
Amesema baadhi ya madalali wamekuwa na kawaida ya kupandisha gharama ya nyumba na vyumba vya kupangisha kwa lengo la kupata kamisheni kubwa hali ambayo inaumiza wananchi wengi hasa wenye uwezo mdogo.
“Unakuta nyumba inapangishwa kwa Sh.100,000 kwa mwezi lakini dalali anamwambia mpangaji kwamba inapangishwa kwa Sh. 200,000 sasa mpangaji akijiongeza akaenda kwa mwenye nyumba akaambiwa kwamba inapangishwa kwa Sh 100,000 heshima yako na uaminfu wako unapotea,” amesema Dk. Mabula.
Amesema baadhi yao wamekuwa wakiuza mali ambazo hawajaambiwa kuuza kama viwanja na nyumba hali ambayo imesababisha migogoro mingi huku wao wakikimbia na kusababisha wanunuzi kubaki wakihangaika.
“Ndiyo maana nasisitiza kwenye mafunzo haya muwafundishe maadili. Ukiwa na maadili watu watakuwa mabalozi wako kwamba ukitaka kazi hii ifanikiwe mwone fulani lakini kama ni tapeli hutapata kazi na utaishia kutafutwa kwa wizi,” amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Madalali Tanzania (AREA),Erick Rweikiza amesema dhamira ya chama hicho ni kuweka mazingira bora ya kuelimisha wanachama wake kuhusu taaluma yao na kujenga umoja kibiashara na kutetea maslahi yao.
Amesema nia yao ni kuweka mazingira bora ya kutoa huduma bora kwa wapangaji, wapangishaji, wauzaji na wanunuzi ambao kwa pamoja ndio waajiri wa mawakala hao.
“Pamoja na madalali walengwa wetu wakubwa ni pamoja na watu wote wasio na ajira na nia yetu ni kuwafundisha watu wasio na ajira wajiajiri kupitia taaluma hiyo,” amesema Rweikiza.
Aidha, alisema takwimu zinaonyesha kuwa Jiji la Dar es Salaaam litakuwa na watu milioni 10 ifikapo mwaka 2030 hivyo ongezeko hilo la idadi ya watu itasababisha mahitaji ya makazi kuwa makubwa hivyo kutoa fursa kwa madalali.