Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),Mkoa wa Dodoma Mhandisi Donasiano Shamba ameelezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kupitia Shirika la Umeme mkoa wa Dodoma haswa upande wa Utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza na wa pili ambapo TANESCO ndiye msimamizi wa utekelezaji wake Mkoani Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dodoma amesema mradi wa tatu mzunguko wa kwanza umeweza kuwafikia wateja 20,319 katika vijiji 168 ambao teyari una utekelezaji wa asilimia 98.
Amesema mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili unaendelea hivi sasa kwenye vijiji 159 na unategemewa kufikia wateja 3,498 wanaotarajiwa kuunganishwa ambapo zaidi ya billioni 70.4 zitatumika kuwezesha mradi huu. Mradi umeshafikia asilimia 40 ya utekelezaji wake ambapo TANESCO Dodoma ni msimamizi wa utekelezaji huo Mkoani Dodoma.
“Mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza umeweza kuwafikia wateja 20,319 katika vijiji 168 na wigo wa mradi ni ujenzi wa njia za msongo wa kati umbali wa km 878.73, njia za msongo mdogo kilomita 1118.43 na ufungaji wa mashine 323.
Mradi una utekelezaji wa asilimia 98 na Mradi wa awamu ya tatu mzunguko wa pili una jumla ya vijiji 159 vinavyofikiwa hivi sasa unaojumuisha ujenzi wa njia za msongo wa kati wa kilometa 1617.5, njia za umeme mdogo kilometa 159 na ufungaji wa transfoma 159 na uunganishaji wa wateja 3,498 na ambapo zaidi ya billioni 70.4 zinatumika na mradi umefikia asimimia 40 ya utekelezaji wake”, amesema Meneja Shamba.
Aidha amewatoa hofu wananchi ambao bado hawajafikiwa na miradi hii kuwa watafikiwa watafikiwa na swami zinazofuata kwani Serikali imejikita zaidi kuboresha huduma muhimu za jamii zikiwemo hospitali, shule, visima na maeneo ya taasisi za dini ambapo ndio wanatumia wanachi.
Pia ameshukuru wananchi kwa ujumla kwa muitikio wa kasi wanaoonesha maeneo ya miradi na kujitokeza kwa wingi kuungansihiwa umeme haswa ukizingatia mifumo rahisi ya kuombea huduma hiyo. Kuanzia Juni 2021 Mpaka sasa jumla ya wateja waliokwisha unganishiwa huduma ya umeme ni 63,513.
“…Pia niwatoe hofu wananchi ambao bado hawajafikiwa na miradi ya REA kuwa mtafikiwa sambamba na sera ya kitaifa ya usambazaji umeme ola tu usambazaji wake ni kwa awamu na serikali imejikita zaidi katika meneo muhimu ya Huduma kwa wananchi zikiwemo hospitali, shule, visimani na taasisi zingine zikiwemo za dini.”
“Tunawashukuru sana wateja wetu na wananchi kwa ujumla Mkoa wa Dodoma kwa kasi wanayoionesha na kujitokeza kwa wingi kuunganishiwa umeme maana ukiritimba umepungua kabisa kwani sasa, mteja anaweza kujihudumia mwenyewe kupitia mifumo yetu ya Nikonekt na Nihudumie (0748550000). Karibuni nyote tutumie mifumo hii kwa huduma zenye ufanisi zaidi”, amesema Shamba.