Na Anthony Ishengoma,JamhuriMedia,Dodoma
Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwan Kikwete amewataka Wataalam wa Mipango miji kutambua kuwa zoezi la utwaaji ardhi ni la ushirikishwaji tofauti na baadhi ya wataalam wanavyofanya bila kushirikisha wananchi.
Ameongeza kuwa vitendo hivi havikubaliki na kuitaka bodi ya wataalam wa mipango miji kutoa elimu kwa wataalam hao kuacha tabia hiyo inayochangia kuleta migogoro mikubwa kwa wananchi hususani katika maeneo ya miji ambapo miradi ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi imekuwa ikiendelea.
Kikwete amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Usajili wa Wataalam wa Mipango miji na kuonya kuwa ni vibaya kwa wataalam hao kukiuka taratibu za kitaaluma suala linalopekea kuchochea migogoro.
Kikwete ameonya tabia ya kutosimamia mipango miji waliyoiweka inasababisha miji kuvurugwa kwani kwa sasa kila mahali kuna ujenzi wa vyumba vya maduka au vituo vya mafuta na baa katika makazi ya watu.
‘’Haya ni mambo ambayo bodi inapaswa kuyasimamia kwani uzinduzi wa Bodi hii ni suala muhimu sana katika mustakabali wa ukuaji wa taaluma ya mipangomiji, kwani bodi ya wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya Bodi ndizo pande mbili ambazo zinaungana pamoja katika kuikuza na kuisimamia taaluma ya mipangomiji nchini’’ amesema Kikwete.
Naibu Waziri Ridhiwani Kikwete alisema sekta ya ardhi ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa na kwa kila mwananchi akiongeza kuwa Ardhi ni msingi wa kipekee wa maendeleo na ni rasilimali isiyoongezeka.
Akitolea mfano wa Nchi yetu Naibu Waziri Kikwete amesema Tanzania ina eneo lenye ukubwa wa takribani kilometa za mraba 948,132.89, ikijumuisha kilometa za mraba 62,032.89 za maji uku eneo la nchi kavu lina ukubwa wa kilometa za mraba 886,100, ambapo Tanzania bara ni kilometa za mraba 883,600, na Zanzibar ni kilometa za mraba 2,500.
Aliongeza kuwa kuna ongezeko la watu kutoka watu 43,625,354 Sensa ya watu 2012, hadi kufikia watu 61,741,120 Sensa ya Watu na Makazi 2022 wakati idadi ya watu ikiongezeka, ukubwa wa ardhi bado ni uleule.
Kikwete aliongeza kuwa kwa kuzingatia ukweli huo, Wataalam wetu pamoja na kampuni za upangaji miji ni muhimu ziendelee kupanga ardhi kwa weledi wa hali ya juu kwani ikifanyika vinginevyo, tutashuhudia ongezeko la migogoro ya ardhi baina ya watumiaji mbalimbali wakiwemo wakulima, wafugaji, wachimbaji madini na hifadhi za Taifa.
Naye Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo Prof. John Lupala akitoa mwelekeo wa bodi yake amesema Bbdi yake kwa mwaka wa fedha ujao itaanzisha mfumo wa kufuatilia wataalamu wa mipangi miji ili kuweza kuwafuatilia kwa akaribu ili kuwazawadia wanaofanya vizuri na kutoa adhabu kwa awale wanaokiuka taratibu.
Prof. Lupala ameongeza kuwa mfumo huu pia utawezesha bodi kuona kwa karibu kinachoondelea kwa wataalamu wa mipango miji lakini pia kuhakikisha wanaanza taratibu za usajili kwa wataalamu wa wapya kuanzia taratibu za awali mpaka usahili kwa wataalamu hao.