Na Israel Mwaisaka,JamhuriMedia,Nkasi

Imeelezwa kuwa Mkoa wa Rukwa una wanafunzi wa shule za msingi wapatao 24,000 ambao hawajui kusoma,kuandika na kuhesabu.

Hayo yamebainishwa na Ofisa elimu wa mkoa huo, Samson Hango wilayani Nkasi wakati Katibu Tawala wa mkoa, Rashid Mchata akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari na maofisa wa Serikali yenye lengo la kuwajengea uwezo kufahamu kuhusu mradi wa shule bora unaotekelezwa mkoani humo.

Amesema kuwa kutokana na utafiti uliofanyika Desemba mwaka jana ilibainika kuwa katika mkoa huo kuna wanafunzi 24,000 kati ya 300,000 wa shule za msingi ambao hawajui kabisa kusoma,kuandika na kuhesabu.

“Kutokana na utafiti uliofanyika Desemba mwaka jana ilibainika kuwa kuna wanafunzi 24,000 kati ya zaidi ya wanafunzi 300,000 wa shule za msingi ambao hawajui kabisa ‘K’ tatu, hali ambayo inatulazimu tupambane ili wanafunzi hao wazijue hizo K tatu ambao ndio msingi wa elimu” amesema.

Akifungua mafunzo hayo Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Mchata amesema kuwa vyombo vya habari mkoani humo bado havijaripoti vya kutosha kuhusu changamoto zilizopo katika sekta ya elimu.

Amesema kuwa sekta hiyo bado haijafanya vizuri sana hivyo ni wajibu wa wanahabari kuibua changamoto zinazo ikabili ili zitafutiwe ufumbuzi hali ambayo itasaidia kukuza kiwango cha ufaulu mkoani humo.

Katibu tawala huyo amesema kuwa kupitia mradi wa shule bora unaotekelezwa mkoani humo itasaidia kumaliza changamoto ya wanafunzi hao wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu kwani ni moja ya malengo ya mradi huo.

Awali akitoa taarifa ya mradi wa shule bora mkoani Rukwa mratibu wa mradi huo, John Shindika amesema kuwa mradi huo unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa ufadhili wa serikali ya Uingereza na ulianza kutekelezwa mwaka 2021 na utafika mwisho mwaka 2027.

Amesema kuwa kwa kupitia mradi huo mkoa wa Rukwa utakua na shule bora zitakazo kidhi mahitaji huku zikifanikisha azma ya Serikali ya kuongeza ufaulu sambamba na idadi ya wanafunzi watakaojiunga na shule kwa ajili ya kupata elimu.