Jeshi la Polisi Tanzania limesema kuwa hali ya ulinzi na usalama wa nchi ni shwari kwani matukio makubwa yanayoweza kuleta hofu kwa wananchi yanaendelea kudhibitiwa,
Kwa mujibu wa taarifa ilitolewa kwa vyombo vya habari leo Januari 26, 2023 na msemaji wa Jeshi la Polisi,SACP David Misime, amesema kuwa Polisi wanaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ambapo limewakamata wahalifu katika matukio mbalimbali yaliyotokea nchini.
Amesema kuwa makamanda wa Polisi mikoa na vikosi wanaendelea kutoa taarifa za kila mara na Polisi wanaendelea kuimarisha ulinzi na mikakati yake ya kuhakikisha wanazuia uhalifu kwa kiwango kikubwa zaidi kwa mwaka huu wa 2023.
“Miongoni mwa mikakati hiyo ni kutoa elimu kwa jamii kama tunavyofanya katika shule za msingi hadi vyuo,vijiwe vya bodaboda, maeneo ya masoko, nyumba za ibada na katika vyombo vya habari,lengo ikiwa ni kuwajengea uelewa wananchi ili wawe karibu zaidi na Jeshi la Polisi.
“Pia kubaini na kuzuia uhalifu kuliko kusubiri utokee ndipo tuanze kupambana kupitia ushirikiano wa wananchi utafiti umeonyesha tutaweza kuwa na vyanzo vingi zaidi vya kupata taarifa nyingi za kusaidia kuzuia uhalifu,” amesema.
Amesema kuwa Januari 25, 2023 katika baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii kuliwa na taarifa ya tahadhari kutoka Ubalozi wa Marekani hapa nchini kwa wananchi wao wakiwatahadharisha uwezekano wa kutokea uhalfu wa kigaidi maeneo yanayopendwa kutembelewa na watu wengi hapa Tanzania wakiwemo wageni.
“Jeshi la Polisi Tanzania tulianza kuifanyia kazi taarifa hiyo kwa kina toka iliponza kusambaa katika vyombo vya habari, hivyo wananchi waendelee kuwa watulvu na kuendelea na shughuli zao kama kawaida,” amesema.
Aidha Kamanda Misime amesema amewataka wananchi pindi wanapomtilia mashaka mtu kutokana na mienendo yao ni vyema taarifa hizo zikatolewa kwa Jeshi la Polisi haraka ili ziweze kufanyiwa kazi.