Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,Wilbert Chuma ametembelea mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma huku akitoa rai kwa wananchi kutembelea maonesho hayo ili kupata elimu ya usuluhishi kufahamu kwa kaulimbiu ya Wiki ya Sheria ya mwaka huu inayohusu masuala ya usuluhishi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kutembelea mabanda kadhaa ya Maonesho leo Januari 24, 2023 , Msajili Mkuu, Chuma amesema kuwa kaulimbiu ya mwaka huu imewekwa mahsusi lengo likiwa ni kutoa elimu kwa umma ili kufahamu umuhimu wa suala ya usuluhishi ambalo lina faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuleta utengamano katika jamii.
“Maonesho haya yana umuhimu mkubwa kwa umma, moja ni kujenga uelewa wa wananchi na wadau kuhusu masuala ya Mahakama tasnia ya Sheria kwa ujumla. Mabanda haya yamesheheni wadau mbalimbali, hivyo ni muhimu wananchi kufika na kupata uelewa wa masuala mbalimbali,” amesema Chuma.
Aidha, baada ya kutembelea mabanda hayo, Msajili Mkuu ameonesha kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa Wadau mbalimbali wa Mahakama waliojitokeza kushiriki kwenye maonesho ya wiki ya Sheria pamoja na Mahakama ya Tanzania.
Miongoni mwa mabanda yaliyotembelewa na Msajili Mkuu ni pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Tume ya Kurekebisha Sheria, Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (DPP), Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OAG), RITA na Wakili Mkuu wa Serikali (OSG).
Maonesho haya ya Wiki ya Sheria yanaendelea kufanyika nchi nzima hadi tarehe 29 Januari, 2023 ambapo kilele cha Siku ya Sheria nchini itakuwa tarehe 01 Februari, 2023.
Kauli mbiu ya Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka huu ni; Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.