Ofisi ya Makamu wa Rais imepanga kufanya ufuatiliaji wa gawio kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) pamoja utekelezaji wa Taasisi za Muungano katika kipindi cha Januari 2023 hadi Juni 2023.
Pia amesema Ofisi imepanga kutoa semina kuhusu usimamizi wa fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo kwa wabunge 50 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wanaotoka Zanzibar.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais kuanzia Julai 2022 hadi Desemba 2022 kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria leo Januari 24, 2023 katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.
Amesema kuwa Serikali inatarajia kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo inayotekelezwa pande mbili za Muungano ikiwa ni pamoja na kuratibu utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo kwa Majimbo ya Zanzibar.
Katika kuhakikisha inaendelea kutatua hoja za Muungano zilizosalia Dkt. Jafo amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kuratibu Vikao vya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na SMZ vya kushughulikia masuala ya Muungano.
Aidha, Waziri Jafo ameongeza kuwa ili kuhakikisha utekelezaji unafanyika ipasavyo Serikali inatarajia kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Kamati ya Pamoja na yale masuala 22 ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, katika muendelezo wa utoaji wa elimu ya Muungano tumefuatilia Ithibati ya Kitabu cha Historia ya Muungano ili kiweze kutumika kama Kitabu cha ziada kwa shule za Msingi na Sekondari pia kutoa elimu ya Muungano mashuleni na katika vyuo vya elimu ya juu,” amesema.
Kwa upande wake Makamu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ameitaka Ofisi ya Makamu wa Rais kuendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya Muungano ili wananchi wapate uelewa.