Michuano ya Ligi Kuu ya Soka ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, inaanza kutimua vumbi kwenye viwanja saba tofauti, Jumamosi wiki hii. Agosti 31, mwaka huu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitoa ratiba inayoonesha kuwa bingwa wa ligi hiyo atapatikana Mei 18, mwakani, wakati timu zote 14 zinazoshiriki zitakapokuwa uwanjani kuhitimisha mechi zake 26 kila moja.

Msimu uliopita, Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club ya Dar es Salaam ilinyakua ubingwa huo kwa kujikusanyia pointi 62 kutokana na kushinda mechi 19, kutoa sare tano, kupoteza mbili, kufunga mabao 17 na nyavu zake zilizokuwa zikilindwa takribani siku zote na kipa Juma Kaseja, zilitikiswa mara 12.

 

Azam FC pia ya Dar es Salaam ilishika nafasi ya pili kwa pointi zake 56 baada ya kushinda mara 17, kutoa sare mechi tano, kupoteza mechi nne, kufunga mabao 41 huku yenyewe ikifungwa 15. Katika hali hiyo, Simba ndiyo itakayoiwakilisha Tanzania Bara kushiriki Michuano ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2012/2013 huku Azam ikicheza Kombe la Shirikisho la Kandanda Afrika (CAF).

 

Dar es Salaam Young Africans (Yanga) yenye makao yake makuu mitaa ya Jangwani na Twiga jijini, iliyokuwa ikitetea ubingwa wa ligi hiyo ilitupwa nafasi ya tatu baada ya kuishia na pointi 49. Ilishinda mechi 15, ikatoka sare nne, ikapoteza saba, ikafumania nyavu za timu pinzani mara 40 huku yenyewe ikiokoteshwa mipira mara 27.

 

Timu nyingine zilizoshiriki kwa mtiririko wa nafasi zilizoshika na pointi zake zikiwa kwenye mabano ni Mtibwa Sugar ya Morogoro (42), Coastal Union ya Tanga (39) na JKT Oljoro ya Arusha (35) iliyoshika nafasi ya sita.

 

Zilikuwapo pia JKT Ruvu ya Kibaha, Pwani (32), Ruvu Shooting Stars pia ya Kibaha, Pwani (31), African Lyon ya Dar es Salaam (27), Toto African ya Mwanza (26), Villa Squad ya Dar es Salaam (26), Moro United ya Morogoro (19) na Polisi ya Dodoma iliyoambulia pointi 17.

 

Mpangilio huo wa ushindi na nafasi uliziacha timu tatu za Villa Squad, Moro United na Polisi ya Dodoma zikirudi Daraja la Kwanza na kuzipa nafasi timu za Prisons ya Mbeya, JKT Mgambo ya Tanga na Polisi ya Morogoro zikipanda kucheza Ligi Kuu msimu huu.

 

Tayari mbwembwe za usajili zilizoambatana na majigambo, furaha, huzuni na vilio zimeshapita na sasa mashabiki hasa wa Yanga, Simba na Azam angalau roho zao sasa zimeanza kutulia ingawa siku ya mwisho ya usajili kwa wachezaji wa kulipwa kutoka nje ya nchi ni Jumamosi wiki hii.

 

Simba iliyokuwa ikimtegemea zaidi mshambuliaji Emmanuel Okwi kuifungia mabao msimu uliopita, safari hii imenasa mastreika wapya kama Abdallah Juma na Daniel Akuffo, raia wa Ghana aliyefanya vizuri katika mechi mbili za maandalizi kwa kufunga bao moja kila anapokuwa uwanjani.

 

Imesajili pia mabeki wawili wa kati na pembeni ambao ni Mkenya Pascal Ochieng na Komalmbil Keita, raia wa Ivory Coast – watakaoshirikiana vyema na walinzi waliowakuta ndani ya timu hiyo inayonolewa na kocha Milovan Cirkovic kutoka Serbia.

 

Kwa upande wake, Yanga – wapinzani wakubwa wa Simba, imefanikiwa kusajili washambuliaji wapya walioonesha umahiri mkubwa dimbani. Hao hasa ni Saidi Bahanuzi aliyetokea Mtibwa Sugar na Didier Kavumbagu kutoka Atletico ya Burundi. Watasaidiana kwa karibu na kina Haruna Niyonzima kutoka Rwanda na Khamis Kiiza, raia wa Uganda walioichezea tangu msimu uliopita.

 

Kama ni majaaliwa, Yanga pia itakuwa na ukuta imara wenye mabeki mahiri kama Kelvin Yondani na Mbuyu Twite, lakini tu kama watathibitishwa na TFF kuvaa jezi za njano na kijani kutokana na mvutano uliotokea kati ya timu hiyo na Simba. Imepata pia kocha mpya, Tom Saintfeit kutoka Ubelgiji anayetazamiwa kuleta changamoto kubwa kwa ligi hiyo nchini.

 

Kati ya vigogo vitatu vya soka Tanzania Bara, Azam ndiyo pekee ambayo haikufanya usajili wowote mkubwa, lakini pia imempoteza mmoja wa washambuliaji na wafumania nyavu wake mahiri – Mrisho Ngassa – iliyempeleka kuichezea Simba kwa mkopo.

 

Hali hiyo imeifanya timu hiyo iendelee kumtegemea zaidi mshambuliaji John Bocco, lakini atakosa krosi maridadi kutoka kwa Mrisho Ngassa na Ramadhan Chombo Redondo, kiungo mwingine mahiri aliyekwenda Simba, lakini yenyewe ikisisitiza kuwa bado ni mchezaji wake.

 

Mechi za ufunguzi wa ligi hiyo Jumamosi wiki hii na viwanja vyake kwenye mabano zitazikutanisha Simba vs African Lyon (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Polisi Morogoro vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro), Prisons vs Yanga (Sokoine, Mbeya) na Mgambo JKT vs Coastal Union (Mkwakwani, Tanga).

 

Nyingine ni JKT Ruvu vs Ruvu Shooting Stars (Azam Complex, Dar es Salaam), Kagera Sugar vs Azam (Kaitaba, Bukoba) na Toto African itakayopepetana na JKT Oljoro (CCM Kirumba, jijiniMwanza).

 

Je, ni timu gani itakayoibuka kuwa klabu bingwa ya kandanda Tanzania Bara msimu ujao na ushindani utakuwaje? Wapenzi wa soka tunasubiri kwa hamu kubwa kuiona timu hiyo.