Serikali imetoa agizo kwa wafugaji wote nchini kupeleka mifugo yao katika majosho ya serikali yaliyojengwa katika maeneo mbalimbali nchini huku lengo kuu likiwa kuzisaidia jamii zilizoathirika na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo mikoa ya Dodoma,Singida huku ikiwaasa kutunza mazingira ili kuruhusu uoto wa majani ambacho ni chakula cha wanyama.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Chilo wakati akizungumza na jamii ya wafugaji katika Kijiji cha Machenje, wilayani Kongwa jijini Dodoma ambapo pia alishuhudia zoezi la ng’ombe kupita katika majosho hayo pamoja na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo uchimbaji wa visima katika maeneo ya vijiji vya Mtanana, Chigwingwili, Soiti, Ndalibo, Ugogoni, Machenje, Nguji, Ibwaga na Chitomolo.
“Tunawaomba wananchi wanaomiliki mifugo ya miguu minne wa maeneo haya na maeneo yote yenye mifugo nchini wapeleke mifugo yao katika majosho hayo ili kuweza kuwakinga Wanyama hao na magonjwa mbalimbali lakini pia nawaasa mtunze mazingira kwani Wanyama hao hutegemea mazingira yanayowazunguka kwa chakula kwa hiyo kutotunza mazingira hayo kutapelekea wanyama hao kukosa majani kwa ajili ya chakula” amesema Naibu Waziri Khamis Hamza Chilo
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji waliofika kwa zoezi hilo la kuogesha mifugo yao,mmoja wa wafugaji hao ,Abdi Juma ameishukuru serikali kuwaletea huduma hiyo ya majosho kwani itaenda kuwaondolea hasara waliyokua wanaipata ikiwepo vifo kwa mifugo yao huku akishukuru miradi mbalimbali iliyoletwa na serikali ili kuwasaidia kurudisha uoto wa asili kwa maeneo yao.
“Tunaishukuru serikali kwa miradi hii,tumekua tukipoteza mifugo yetu maana mazingira kama mnavyoona yamekua jangwa,kwa hiyo miradi hii ikiwemo manywesheo ya mifugo yetu,majosho ya kuwakinga na magonjwa yamesaidia sana na tunaomba serikali iendelee kutuangalia katika mambo mengine pia” amesema Abdi Juma
Mradi wa kukabiliana na na mabadiliko ya tabia nchi kwa jamii za wakulima na wafugaji katika wilaya ya Kongwa ilizinduliwa rasmi mwaka 2021 huku ukitarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu hadi mwaka 2024 huku takribani wafugaji na wakulima zaidi ya 45,000 wakitarajiwa kunufaika na mradi huu.